Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinajivunia ziara ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwimyi aliyerejea toka Uingereza huku akiwa amelata mafanikio na matumaini ya kuendelea kufanyika kwa mageuzi ya kiuchumi na kimaendeleo.
CCM kimeitaja ziara hiyo ni ya aina yake ambayo italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya umma na sekta binafsi kimaendeleo.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo ofisini kwake Kisiwandui, alipotakiwa kutaja dhana na mantiki ya ziara ya Rais Dkt. Mwinyi nchini Uingereza.
Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi akiwa Uingereza amehudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Madola wa Masuala ya Biashara na Uwekezaji uliojikita katika Agenda ya Uchumi wa Buluu.
Aidha, Mbeto alisema kwa namna kubwa, Uchumi wa Zanzibar utaendelea kukua kila Mwaka ambapo sasa umefikia zaidi Asilimia 7.
Kadhalika ameutaja Ukuaji huo wa Uchumi, utakua zaidi kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kuwa na Sera Bora, sanjari na utangazaji wa fursa na kuwakaribisha Wawekezaji toka Mataifa mbalimbali duniani.
Mbeto alisema, Sekta tatu mama kwa Uchumi za ni Utalii, Uchumi wa Buluu na Utafutaji wa Mafuta na Gesi , ambapo kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kukaribisha Wawekezaji wengi ambao wameonyesha ni ya kuwekeza Zanzibar.
“Serikali za CCM zipo kwa ajili ya kutumikia wananchi. Serikali zetu zitafanya kila linalowezekana kuinua uchumi wa nchi zetu ,kuboresha maisha ya watu kwa kuwavutia wawekezaji kuwekeza miradi mikubwa,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi, alibainisha akisema Wawekezaji wengi hususan toka Uingereza, wameweka azma ya kuja kuwekeza, kuliongezea thamani zao la Mwani, kuongeza mnyororo wa thamani, Uzalishaji wa mbegu bora, masuala ya tafiti na kwajengea uwezo Wakulima.
“Sera za chama chetu zimejiegemeza katika kuhangaika kuinua ustawi wa maisha ya watu. Tumeeleza haya katika ilani ya chama chetu. Tutasimamia masuala yote na kuwafanya wananchi waishi katika maisha nafuu na yenye neema tele,” alisisitiza.
Mbeto aligusia pia sekta ya Mafuta na Gesi, akisema kampuni nyingi zimeiingia mikataba na Serikali kuhusu utafutaji wa Data za Mafuta na Gesi , kwa kuzitangaza Duniani ili kupata Wawekezaji Zaidi.
Hata hivyo, Mbeto akielezea kuhusu Nishati ya Umeme, alisema SMZ amewakaribisha Wawekezaji wengi toka Uingereza kuja na kuwekeza katika Umeme wa upepo ,takataka na jua
Akizungunzia Utalii alisema, Zanzibar imekuwa ikisisitiza Sera ya Utalii endelevu , ambapo hadi sasa tayari imewavutia Wawekezaji katika uhifadhi wa Mazingira kwani Zanzibar inahitaji Watalii wenye Uwezo watakaoongeza pato na Fedha nyingi badala ya idadi ya Watalii.