RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo Juni 13, 2026, amejumuika na wanafamilia, ndugu, jamaa, wasanii, na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya msanii mkongwe, marehemu Issa Joseph Mohamed, maarufu kwa jina la Mzee Onyango, yaliyofanyika Kawe, Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, pamoja na wasanii wa fani mbalimbali na wananchi waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.
Mara baada ya kuwasili, Rais Dkt. Mwinyi alisaini kitabu cha maombolezo na kutoa mkono wa pole kwa wanafamilia.
Marehemu Issa Joseph Mohamed alizaliwa Aprili 14, 1950 na kufariki dunia Juni 11, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Jijini Dar es Salaam.
Wakati wa uhai wake, marehemu alipata umaarufu mkubwa kupitia kazi zake za filamu na maigizo na kujizolea heshima kubwa miongoni mwa Watanzania kwa jina la Mzee Onyango.
Marehemu amezikwa katika Makaburi ya Kondo, Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe. Amina.