Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Chama Mapinduzi (CCM) kimewataka vijana wa kitanzania kutambua thamani ya amani, umoja na maendeleo katika Taifa lao hivyo wasikubali kuipoteza kwa ushawishi toka nje au ndani ya Taifa lao.
Aidha, CCM Serikali za CCM zimeapa kuendelea kusimamia misingi ya kulinda Amani, Umoja na Usalama dhidi ya tishio lolote.
Tamko hilo limetamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis ameeleza hayo kabla ya uzinduzi wa mechi ya wiki ya Amani visiwani Zanzibar.
Mbeto alisema, kuna fununu za kuwepo kwa maandalizi ya upinzani kufanya maandamano Julai 7 mwaka huu ambayo hayana kibali wala ruksa ya kisheria toka polisi.
Alisema, kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, maandamano au mkusanyiko wowote ambao hauna kibali ni haramu, hivyo akawataka vijana kutojihusisha na maandamano hayo.
“Watanzamia wanatambua thamani ya Amani, Umoja na Maendeleo ya Taifa lao. Hawatakubali kuifisidi nchi yao kwa ushawishi aidha toka nje au ndani,” alisema Mbeto.
Katibu huyo aliongeza kusema kuwa, ni wazi upinzani ulishindwa kuwashawishi wananchi ili kuwaunga mkono, hivyo wameamua kuchagua njia haramu ya vurugu na ghasia kinyume na demokrasia.
“Tunaekewa kutokana na mizizi mirefu ya kuimarika kwa CCM kisiasa upinzani umeshindwa kufurukuta. Hawana uwezo wa kuishinda CCM kwa demokrasia ya kupiga kura,” alieleza.
Hivyo, alisema njia pekee ambayo upinzani umeamua kupita ni kufanya maandamano ya kuvuruga Amani na Utulivu uliopo nchini wakidhani hiyo ndio maana ya domokrasia.
“Maendeleo ya haraka yaliyopatikana Tanzania Bara na Zanzibar yametokana na kuwepo kwa amani na utulivu. Vijana wa kitanzania msikubali kuiweka nchi yenu rehani,” alisisitiza.