KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman (OMO) alilenga kupotosha umma kuhusu mradi wa ujenzi wa mji wa michezo wa AFCON unaojengwa Fumba.
Mbeto ametoa kauli hiyo leo Julai 28, 2026 wakati akifafanua mambo mbalimbali, yanayoendelea nchini ikiwemo kauli ya OMO ambaye hivi karibuni wakati akihojiwa na kituo kimoja cha luninga alisema, mradi huo wa AFCON hauna tija.
Mbali na hilo, OMO alidai kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ni Shilingi Trilioni 1.6, jambo ambalo imeelezwa halina ukweli, kwani mradi huo unagharimu takribani Shilingi Bilioni 300 na utahusisha miundombinu mbalimbali.
Inaelezwa, mradi huo unajumuisha Uwanja wa Kisasa wa mpira wa miguu, viwanja vya michezo mbalimbali, hoteli, nyumba za makazi, kumbi za mikutano pamoja na huduma nyingine ambazo zitaiwezesha Zanzibar kuwa mwenyeji wa mashindano na matukio makubwa ya Kimataifa.
“Nadhani alifanya makusudi, yeye si mgeni, anajua uchumi unajengwa vipi, anajua kama kazi ya Serikali sio kufanya biashara, ni kutoa huduma na kujenga miundombinu,” alisema Mbeto.
Alisema, hata OMO akiwa kiongozi atafanya kama anayoyafanya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi ya kujenga miundombinu ya Barabara na michezo. “Huwezi kuwaacha wananchi wako bila kuwajengea miundombinu ya michezo wakati wana historia ya michezo, hauwezi kuwaacha wananchi wako wanatembea kwenye barabara mbovu, atafanya tu kama anavyofanya Mwinyi.”
Mwenezi Mbeto aliendelea kusema, kinachofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Mwinyi ni sahihi na lengo ni kuibadilisha nchi na kila anachofanya ndicho kinachofanyika kwenye nchi nyingine duniani.
“Ukienda Dubai au China hakuna majumba mabovu, kila jimbo linalishinda jingine kwa ujenzi wa miundombinu ya Barabara, usafiri mbalimbali na majengo ya kisasa, sasa unataka mji uwe vile vile kama ilivyokuwa enzi za mabibi zetu? Au tucheze uwanja ule ule wa zamani Mnazi Mmoja wenye michanga na mabonde?” alihoji Mbeto.
Aidha, Mbeto alimtaka Rais Dkt. Mwinyi kuendelea kufanya maendeleo kwa vitendo kama anavyofanya hivisasa, ambapo ameibadilisha Zanzibar kwa kiasi kikubwa.