PWANI YAPAA KIUCHUMI: Viwanda 247, Bandari kavu ya Kwala yazidi kuleta mapinduzi

0

SERIKALI imeeleza kuwa, uwepo wa Bandari Kavu ya Kwala katika eneo la Vigwaza, Mkoa wa Pwani, umeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uchukuzi.

Kutokana na mapinduzi hayo, msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam umepungua na kurahisisha usafirishaji wa shehena kupitia reli na barabara kuu.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliyasema hayo Machi 16, 2025, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika bandari hiyo.

Alibainisha kuwa Bandari Kavu ya Kwala tayari imepokea makontena 700, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha miundombinu na kuimarisha biashara.

Mbali na mafanikio hayo, Msigwa pia alipongeza Mkoa wa Pwani kwa mafanikio makubwa katika sekta ya viwanda, ambapo chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge, mkoa huo umepokea miradi 369 ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na viwanda 247 vyenye uwekezaji wa jumla ya Dola Bilioni 4.6 (zaidi ya Shilingi Trilioni 11).

Sekta ya viwanda pekee inachangia Dola Bilioni 2.8, ikithibitisha kuwa Mkoa wa Pwani ni kitovu cha maendeleo ya viwanda nchini.

Kuhusu Kongani ya Viwanda ya Sinotan, yenye ekari 2,500, Msigwa alieleza kuwa mradi huu wa Dola Milioni 327 unatekelezwa kwa awamu tano, ukitarajiwa kuwa na viwanda vikubwa 200 na vidogo 300.

Awamu ya kwanza tayari imekamilika kwa asilimia 80, huku mradi ukitarajiwa kutoa ajira 100,000 za moja kwa moja na 500,000 zisizo za moja kwa moja.

Maendeleo haya yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kukuza uchumi wa viwanda na kuboresha miundombinu ya nchi kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here