Kama kweli ni yeye, Polepole ameikosea mamlaka ya uteuzi – Mbeto

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimesema kama habari zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii kuhusiana na kuacha kazi kwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole zina ukweli wowote, atakuwa ameikosea mamlaka ya uteuzi iliyompa nafasi hiyo.

Akizungumza na wanahabari Julai 14, 2025, akiwa ofisini kwake Kisiwandui Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema Polepole alipaswa kuomba kuacha kisha akasubiri jibu la mamlaka iliyomteua.

“Kama ndio yeye kweli katuma hizo taarifa katika mitandao amekosea sana,” alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa, hawezi kuzungumzia kwa undani sakata hilo kwani hata yeye amesikia lipo mtandaoni na kwa kuwa yupo kwenye vikao vya mchujo wa watia nia, anasubiri kusikia zaidi ama kutoka kwa mamlaka ya uteuzi au Polepole mwenyewe.

Alisema, kama kaandika barua kuomba kuacha kazi na kabla hajajibiwa anaituma mitandaoni, ni ajabu kwasababu kuomba kuna kukataliwa au kukubaliwa. “Tusimhukumu ngoja tusubiri kauli ya mamlaka iliyomteua.”

Mwenezi Mbeto anabainisha kuwa, anachojua yeye chama hakijawahi kukiuka misingi yake na maamuzi yote yamekuwa yakifanywa kwenye vikao halali vya chama.

“Polepole ingawa hana wadhifa wowote katika chama, lakini anaujua ukweli kuwa CCM hakijawahi kutoka kwenye misingi yake,” alisema na kuongeza kuwa, Polepole sio kiongozi wa kwanza kuachia nafasi, tena wengine ni wenye hadhi kubwa kuliko ubalozi, lakini walifuata utaratibu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here