TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) inaendelea na jitihada zake za kuhakikisha elimu ya Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inafika kwa jamii kwa kuwajengea uelewa wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 (PDPA) na namna bora ya kulinda faragha zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Agosti 1,2025 wakati wa hafla fupi ya utiaji saini hati ya makubaliano ya miaka mitatu (3) kati ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dkt. Emmanuel Mkilia, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC alisema, PDPC inaendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu dhana ya Ulinzi wa Taarifa binafsi sambamba na kugusa maeneo yote muhimu ambayo yatashughulika na PDPA.
“Maridhiano haya ni ya muhimu sana katika utekelezaji wa Sheria hii. Wakati tunaitekeleza tunatakiwa kuhusisha sekta zote muhimu ambazo zitashughulika na usimamizi wa Sheria hii. Muhimili mkuu na muhimu sana ni muhimili wa Mahakama kwasababu ndio unaohusika na usimamizi wa haki, hivyo kwa maridhiano haya itatusaidia sana katika ufikishaji wa elimu ya Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa umma,” alisema Dkt. Mkilia.
“Katika suala zima la kuangalia haki, Mahakama ni chombo muhimu sana na maamuzi ambayo wanaweza wakayatoa ni lazima wazingatie matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili PDPC iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi” aliongeza Dkt. Mkilia
Kwa upande wake Dkt. Paul Kihwelo, Jaji wa Rufani na Mkuu wa IJA alisema, makubaliano haya ni ya kimkakati na yamefanyika wakati muafaka hivyo yatasaidia kwenye kutoa elimu kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi sambamba na kuitafsiri.
“Sheria hii ni mpya na watu wengi hawaielewi ikiwemo maafisa wa Mahakama, na wanaweza ikafika mahali wakatafsiri ndivyo sivyo. Bunge linatunga Sheria, Mahakama tunaachiwa wajibu wa kuitafsiri Sheria hiyo ikiwemo kutoa haki. Hivyo sisi kama maafisa wa mahakama tusipoijua inaweza kurudisha nyuma jitihada zote za ulinzi wa taarifa nchini,” alisema Dkt. Kihwelo.
Makubaliano hayo ya PDPC na IJA ni moja ya njia ya PDPC kuhakikisha uelewa wa dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi unawafikia watu wote na ulinzi wa faragha za watu nchini kupitia taarifa zao binafsi.