Na Dkt. Raymond Mgeni
KINGA ni bora kuliko tiba. Kuzuia ni kitendo cha ‘kufanya kitu kisitokee’. Kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya kuambukiza au yasiyoambukiza yalivyo na njia za kujikinga, ndivyo hata kwa magonjwa ya akili yanaweza kuzuiwa.
Ukiachilia mbali magonjwa ya akili yanayosababishwa na sababu za vinasaba vya kurithi na kimazingira, ila zile za kimazingira zinaweza kuzuilika kabisa za watu wasiingie katika kuugua akili.
Katika taaluma ya afya ya jamii ‘public health’ imejikita zaidi katika kuzuia kwa daraja zipatazo tatu. Daraja ya msingi au awali, daraja ya pili na daraja ya juu zaidi. Daraja la awali linagusia kuzuia kabisa utokeaji wa tatizo.
Daraja la pili ni kupunguza visa vya ugonjwa kwa kutoa matibabu au elimu na huku daraja ya juu zaidi linagusia pale ambapo mtu ameshapata athari za ugonjwa na hatua zinazohitajika ni kuzuia athari mbaya zaidi au ulemavu zaidi wa ugonjwa.
Mtu anapopitia changamoto za kuugua akili, basi hupata athari za dalili ambazo zinaweza kuleta udumavu wa utendaji kazi wa kawaida, ufikiri na hata kushiriki shughuli mbalimbali na jamii inayomzunguka.
Mikakati ya uzuiaji wa magonjwa hujikita zaidi katika kuepusha visababishi au mazingira hatarishi yanayoweza kuwa sababu ya utokeaji wa magonjwa.
Kuchelewa kushiriki katika kuzuia ugonjwa kunaweza kuwa na gharama kubwa kimatibabu, ingawa mtu anaweza kupata ugonjwa na zikatumika njia za kupunguza athari zake zaidi; Mfano matumizi ya dawa.
Katika uzuiaji wa msingi au wa awali hugawanyika katika makundi matatu; Uzuiaji wa jumla ambao unagusa jamii nzima kwa wakati mmoja. Huenda ni utoaji elimu juu ya ugonjwa kwa jamii kwa njia kama radio, magazeti, luninga na kadhalika.
Pili, uzuiaji unaolenga makundi mahususi hasa makundi yaliyo katika hatari ya kupata magonjwa ya akili mbali na ujumla wa jamii na tatu kuzuia kwa kulenga mtu mmoja mmoja mwenye athari ya ugonjwa.
Njia za uzuiaji zimegawanyika kulingana na makundi ambayo yapo katika hatari ya kupata magonjwa ya akili. Kundi la kwanza Mama wajawazito; mama aliyetoka kujifungua ni makundi ambayo yanaweza kujikuta katika changamoto ya matatizo ya akili mfano kupata sonona au uchanganyikiwaji wa akili kipindi cha mimba au baada ya kujifungua.
Mahudhurio ya kliniki ni muhimu kuangalia viashiria vyovyote vyenye kusababisha mama mjamzito kupata changamoto. Si hilo tu hata watoto kipindi cha ukuaji wao ni muhimu kuzuia vitendo vyote vya ulezi mbaya au manyanyaso ambayo huchangia kwa wengi wanapokua kuwa na wasiwasi au shambulio la kuumiza linamjengea jeraha hadi ukubwani.
Pia, ushauri wa mama katika kuangalia ukuaji wa mtoto mfano unyonyeshaji, ukaribu wa mama na mtoto, kupata virutubisho vyote unaweza kuepusha udumavu na changamoto za ujifunzaji wa watoto. Pia, angalizo la mama kutotumia pombe kipindi cha ujauzito kunaepusha athari za magonjwa ya udumavu kwa mtoto maana vilevi hupelekea athari kwa mtoto toka akiwa tumboni.
Kwa kundi la watoto, wakubwa na vijana ni la pili ambapo pana umuhimu wao kufahamu au kujikinga na vishawishi vya matumizi ya vilevi, matumizi ya bangi, madawa ya kulevya na huku bila kusahau malezi yasiyo na manyanyaso ambayo yanaweza kuchangia matatizo ya kihisia, sonona na kihaiba kwa watoto au vijana.
Pia, kundi hili linaweza kujizuia kufanya vitendo vya kujinyonga, matumizi ya vilevi kwa kupata elimu mapema kuhusu masuala ya afya ya akili.
Watu wazima na wazee linafuata, ambapo kunahitajika kuhimizwa kuepuka matumizi ya vilevi kupitiliza kwa kutumia njia ya kampeni za umma, utoaji wa dawa za watu wa sonona kupunguza uwezekano wa watu kujiua, kutoa elimu kwa mtu kugundua dalili za awali za magonjwa ya akili.
Elimu ya uvaaji wa vifaa vya usalama kama kofia za pikipiki au kuvaa mkanda ili kuepusha majeraha yanayoweza kuharibu ubongo na yakapelekea ulemavu au magonjwa ya akili. Jingine ni utoaji wa elimu ya mawasiliano mazuri baina ya wapenzi kuepusha migogoro ya kimahusiano ambayo huchangia matatizo mengi ya mfadhaiko, visasi na matukio ya kujitoa uhai.
Kundi la wazee pia ni muhimu elimu ya kabla ya kustaafu ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kukosa maandalizi ya kimaisha na kiuchumi pindi wanapostaafu.
Inaonesha kwa asilimia kubwa wastaafu ambao hawakujiandaa kimaisha huangukia kupata matatizo ya afya ya akili hasa sonona. Mtu akiandaliwa mapema itapunguza uwezekano mkubwa wa utokeaji wa matatizo ya akili baada ya kustaafu.
Maeneo ya kazi pia ni muhimu kutoa ujuzi wa udhibiti msongo wa mawazo na kundi la watu hapa ni kama watu wa afya, madereva, walimu kwa kuepusha kupata uchovu mkubwa kutokana na kazi zao kunakoweza kuchangia kudorora kwa afya ya akili na kukaibua matatizo ya akili.
Lengo mama la kuweka juhudi katika uzuiaji wa magonjwa ya akili ni kusaidia watu kuwa na afya ya akili bora, kuzuia changamoto ambazo hujitokeza mtu akishapata matatizo ya akili na tatu ni kuzuia kuzidiwa kwa ndugu wa wagonjwa katika kumhudumia mtu muathirika wa matatizo ya akili.
*Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu wa Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya, Idara ya Afya ya Akili, anapatikana kwa Simu:+255 676 559 21, barua pepe: raymondpoet@yahoo.com.