NIC na jitihada za mageuzi kwenye soko la bima nchini

0
Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt. Elirehema Doriye.

Na Iddy Mkwama

LICHA ya watanzania wengi kuhamasika kukata bima kwa ajili ya mali zao na hata bima ya maisha, lakini kuna malalamiko mengi yanayoelekezwa kwa baadhi ya kampuni za bima nchini kwa kile kinachodaiwa kutotenda haki kwa wateja wao.

Wateja wengi waliojiunga na kampuni mbalimbali za bima nchini, wanalalamikia kucheleweshewa malipo yao licha ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa, matokeo yake ubabaishaji huo wa watu wachache, unaonekana kuchafua taswira ya soko la bima.

Watanzania wengi kwasababu ya kusikia malalamiko yanayotolewa kila kukicha kwenye vyombo vya habari na wanaposhuhudia mateso wanayoyapata ndugu na watu wao wa karibu waliopata ajali, wanakata tamaa ya kujiunga na bima kwa ajili ya majanga na hata bima ya maisha.

Hivi karibuni, kupitia kwenye vyombo vya habari, kuliibuka sakata la mtu mmoja ambaye jina lake na kampuni anayoilalamikia haikuwekwa wazi; akiomba msaada ili alipwe madai yake anayodai kampuni husika.

Mtu huyo anasema, licha ya kukamilisha taratibu zote, suala la malipo limekuwa gumu na kampuni anayoilalamikia imemuweka wazi kwamba, kwasasa hawana fedha, hivyo asubiri hadi watakapopata uwezo wa kumlipa.

Ikumbukwe, huyu ni mteja ambaye amelipia fedha zake kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kujiandaa na majanga mbalimbali ikiwemo ajali, lakini linapofika suala la kunufaika na kile alichochangia, anapigwa danadana na kukatishwa tamaa.

Sakata hili limeacha maswali mengi, wengine wanahoji imekwenda wapi michango ya mteja huyo? Huku wakifika mbali zaidi kuhoji uwezo wa kiuchumi wa kampuni nyingi za bima na kufikia hatua ya kuitaka Serikali kuzifanyia uhakiki kampuni hiyo ili kuepuka usumbufu wanaoupata wateja wao.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa, moja ya sababu zinazochangia danadana hizi za kuwalipa wateja, ni pale kampuni ya bima inapokuwa na ukwasi mdogo, hivyo linapofika suala la kulipa wateja madai yao, wanatafuta sababu za aidha kutolipa kabisa madai hayo au kuchelewesha malipo.

“Kuna ndugu yangu ni mwaka wa pili sasa anahangaikia madai yake ya bima, alipata ajali ya gari, amekamilisha taratibu zote na imethibitika dhahiri anatakiwa kulipwa, lakini hadi sasa anazungushwa,” alisema Simon Matanda, mkazi wa Pugu.

Matanda anasema, mbali na ndugu yake huyo, ana rafiki yake ambaye amekata tamaa kufuatilia madai yake kwa sababu kila anapokwenda kwenye kampuni husika, anakutana na mambo mapya yanayompa mashaka ya kulipwa haki yake.

“Kuna wakati aliambiwa kuna nyaraka zake zimepotea, akapeleka nyingine, akaambiwa asubiri atapigiwa simu, alipoona muda unakwenda aliamua kufuatilia, lakini kila akienda anakutana na mambo mapya ambayo yamemkatisha tamaa na anaona wazi kwamba, anatafutiwa sababu ili asilipwe madai yake,” anasema Matanda.

Malalamiko kama hayo yapo mengi na kampuni zinazolalamikiwa nyingine ni zile zile, ingawa ukifuatilia kwa makini, katika orodha ya kampuni hizo, Shirika la Bima la Taifa (NIC) halimo, hii maana yake ni kwamba, ni moja ya Mashirika ambayo yamejipanga vizuri kuwahudumia watanzania na kuthibitisha hilo, taarifa zinaonyesha kuwa hakuna mteja yeyote anayelidai Shirika hilo.

NIC ni Shirika la kwanza ambalo lilianzishwa na Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Oktoba 16, 1963 na moja ya shabaha yake, ni kuhakikisha linaongeza ufanisi katika kuwafikia wananchi, na ukweli ni kwamba, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza lengo hilo.

Aidha, Januari Mosi, 2010 yalitolewa maelekezo ya kuwekeza katika TEHAMA, kulipa madai na kufanya biashara katika mazingira ya ushindani, ingawa mabadiliko hayo hayakuzaa matunda.

“Mwaka 2018, Desemba, miaka 10 baada ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Serikali ikaamua kuondoa kabisa maamuzi yake ya kulibinafsisha Shirika, kuanzia mwaka huo, Shirika lilikuwa huru kufanya biashara.” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt. Elirehema Doriye.

Dkt. Doriye anasema, NIC kwa sasa ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, na inaendeshwa kisasa tofauti na miaka ya nyuma ambako lilionekana ni Shirika la kizamani.

Anasema, NIC kwa sasa inafanya biashara katika maeneo mawili; biashara ya bima za kawaida, “Mara nyingi hizi ni bima za mwaka mmoja, lakini zinagawanyika katika kipindi hicho katika eneo la mradi.”

“Eneo la pili ni bima za maisha, bima ya maisha mara nyingi ni ya muda mrefu, inawezekana unataka kupata bima ambayo unataka kuongeza kiwango chako cha maisha. Bima za maisha mara nyingi zinaangalia katika eneo la uhai, na ni sehemu ya uwekezaji ili kupata kiwango fulani cha fedha.”

“Kupitia bima hii, mtu anapata faida. Niseme wazi kwamba, NIC ni moja kati ya makampuni ya bima nchini, lakini, sisi ndiyo bima, tunasema sisi ni bima ya mambo mbalimbali. Hii ni kampuni ya kibiashara ya bima ya Serikali.”

Anasema, kuanzia mwaka 2019 walianza kulisuka upya Shirika hilo na kulifanyia mabadiliko makubwa ya Kiutendaji ili kujiimarisha zaidi Kibiashara, ambapo hivi sasa wameona matunda yake.

Mabadiliko waliyoyafanya ni kwenye uongozi ili kuongeza ufanisi, weledi na tija, pia wamewekeza kwenye rasilimali watu kwa kuajiri wafanyakazi wenye sifa stahiki, wenye weledi na wabunifu.

“Tulihakikisha kwamba, kila mfanyakazi anafanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu na weledi, pia eneo la tija lilipewa kipaumbele. Kwamba kwa kiwango gani, kila mfanyakazi anaweza kuchangia mafanikio ya Shirika, kuanzia mfanyakazi wa chini hadi wa juu, tulihakikisha kwamba kila mmoja anakuwa na mchango katika shirika,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, waliangalia namna ya kuwaendeleza wafanyakazi wake; eneo jingine ni kuwekeza katika rasilimali watu. “Ili kuwapata wafanyakazi ilibidi kuwekeza kiasi kikubwa kwa wale wafanyakazi ambao tulikuwa nao, na kuongeza kama asilimia 25,”

“Lakini uwekezaji mkubwa tuliufanya kwa wale ambao walikuwepo awali kuhakikisha kwamba wanaleta tija, na weledi unaotakiwa, sambamba na kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA ambayo imetusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza Mapato.”

Mbali na kuongezeka kwa mapato baada ya uwekezaji kwenye TEHAMA, anasema wameondoa matumizi ya karatasi, kupunguza muda wa kulipa madai hadi kufikia siku saba na kurahisisha utoaji wa huduma.

“Kwa sasa tumeamua kuachana na matumizi ya karatasi, tunatumia teknolojia, kwa sasa madai yako ukiwasilisha na nyaraka unalipwa ndani ya siku saba, haizidi siku saba, tofauti na huko nyuma hadi siku 30,” anasema.

Mafanikio mengine yaliyopatikana baada ya kufanyika kwa mabadiliko ndani ya Shirika hilo, ni kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 76.45, mwaka 2019/2020 Shilingi Bilioni 103.94 mwaka 2021/22. “Ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.98 kwa mwaka.

“Vilevile usimamizi madhubuti wa matumizi pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kumeongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo na tija, jambo lililoshusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida,” anasema Dkt. Doriye.

Dkt. Doriye anasema, katika kipindi cha miaka mitatu, NIC wamefanikiwa kulipa madai ya bima za wateja, ambapo hadi kufikia Juni 2022, wamelipa Shilingi Bilioni 33.79 kwa bima za Maisha na Shilingi Bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.

“Tumeweza kulipa kodi ya mapato Serikalini kutokana na faida inayopatikana, ambapo ulipaji huo umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 11.86 mwaka 2019/20 hadi Shilingi Bilioni 15.14 mwaka 2021/22 sawa na wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka,” anasema Dkt. Doriye.

Akizungumzia faida iliyopatikana kwa kipindi hicho, Dkt. Doriye alisema, faida ghafi imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 33.65 hadi Shilingi Bilioni 63.21 ambayo ni sawa na asilimia 43.91.

“Kutokana na faida mfululizo, tumeweza kupata malimbikizo ya faida ya Shilingi Bilioni 45.74 kufikia Juni 2022 kutoka kiasi cha malimbikizo ya hasara ya Shilingi Bilioni 19.31,” anasema.

Mbali na hayo, alizungumzia kukua kwa mali za NIC; kutoka mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 350.36, hadi kufikia mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 423.99, ambapo ukuaji huo ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10.51 kwa mwaka.

“Ufanisi katika uendeshaji umewezesha ukuaji wa mtaji wa wanahisa kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 72.16 hadi Shilingi Bilioni 217.07, ukuaji huu ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 100.40 kwa mwaka,” anasema Dkt. Doriye.

Katika kipindi cha miaka mitatu, NIC pia imefanikiwa kuongeza uwekezaji katika hati fungani za Serikali, kutoka Shilingi Bilioni 51.58 hadi Shilingi Bilioni 105.64, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 52.40 kwa mwaka.

“Uwekezaji katika amana ya benki umefikia Shilingi Bilioni 32.23 ukilinganisha na Shilingi Bilioni 19.53 kilichokuwepo mwaka 2019/20, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 32.54 kwa mwaka,” anasema Dkt. Doriye na kuongeza kuwa, mwaka uliopita 2022 wametoa gawio la Shilingi Bilioni 2.0 kwa Serikali, ukilinganisha na gawio la Shilingi Bilioni 1.5 walilotoa mwaka 2021.

Katika hatua nyingine, Dkt. Doriye anasema, ili kukabiliana na uwezo mdogo wa kuhimili hasara inayoweza kutokea (low underwriting capacity) wamefanikiwa kuongeza mtaji wa Shilingi Bilioni 12.05 Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 408.47.

“Hii ni kutoka mtaji uliokuwepo wa kiasi cha Shilingi Bilioni 2.95 na kufikia mtaji wa Shilingi Bilioni 15, kilichopo sasa,” alisema Dkt. Doriye na kusisitiza kuwa, NIC itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya bima nchini na kutoa elimu ya bima kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili watanzania wengi wajiunge na huduma zinazotolewa na Shirika hilo.

Akizungumzia katika eneo la kuendelea kutengeneza mwonekano mzuri zaidi wa Shirika hilo, Dkt. Doriye anasema, mwaka 2019, Shirika lilionekana kuwa na taswira tofauti, kukosa ubunifu, hivyo lilionekana la kizamani.

“Tukaangalia namna ya kufanya ‘branding refresh,’ kubadili dhana potofu kuhusu Shirika, tukaanza kutengeneza muonekano mpya wa Shirika ambao uliwezesha sisi kupewa chata ya Superbrand ikiwa ni kampuni ya kwanza inayomilikiwa na Serikali,” anasema.

Hakika, kama anavyosema Dkt. Elirehema Doriye kwamba, licha ya kuwepo kwa Makampuni mengi ya bima nchini, lakini ukitaka bima ya uhakika, utaipata NIC, bila shaka mageuzi yanayoendelea kufanyika, Shirika hili kongwe linaloendeshwa kisasa, litaendelea kuwa mfano kwenye soko la bima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here