Ni lazima tujitegemee na tujenge uchumi imara

0

Na Elius Ndabila

TUNAPOZUNGUMZIA uhuru kama dhana ya Kifalsafa, mara nyingi huwa tunafikiria uwezo wa mtu binafsi wa kufanya uamuzi, kujijua, kujiendesha kujirekebisha, lakini pia huwa tunatia maanani mkondo ambao upo nje ya nafsi. Mkondo huu wa nje huwa na uwezo wa kuathiri na wakati mwingine huongoza moja kwa moja na kutoa kauli ya mwisho kuhusu jambo la kutenda.

Wakati mwingine nguvu za ndani au utashi wa nafsi ya mtu, unaweza kuwa na nguvu zaidi ya mkondo wa nje. Kwa muda mrefu katika historia ya falsafa ya Kimagharibi kulikuwa na imani iliyotawala kwamba, uwezo wa kutoa sababu au utumiaji wa akili ndilo jambo linalomtofautisha binadamu na mnyama.

Kufuatana na falsafa hii, binadamu anatakiwa kuzitawala hisia zake kwa kutumia akili. Hisia zikiachwa peke yake haziaminiki, kwa sababu mara nyingi huongoza kwenye njia ambayo hatima yake ni madhara.

Taifa huru ni Taifa ambalo kwa kiwango kikubwa linajitegemea katika masuala yake mengi. Uhuru wa Taifa huamuliwa na uwezo wa Taifa hilo kujiamulia mambo yake kwa kiwango kikubwa bila kuingiliwa na utashi wa Taifa jingine. Kunapokuwa na kuingiliwa kwenye maamzi basi kunakuwa na ukoloni mambo leo.

Hayati Nelson Mandela Rais wa Afrika Kusini alipozungumzia kesi yake mwaka 1964 alisema “nimepambana dhidi ya utawala wa weupe, na nimepambana dhidi ya utawala wa weusi. Nina thamini wazo la jamii ya kidemokrasia na jamii iliyo huru ambayo watu wote wataishi pamoja kwa maelewano na fursa sawa. Ni wazo ambalo natumai kulisimamia na kuhakikisha kuwa linatimia. Lakini ikibidi, ni wazo ambalo niko tayari kufa nikilitetea”

Pia, wakati mwingine hayati Nelson Mandela alisema “Mara zote huonekana kama hakiwezekani, hadi pale kitakapofanyika. Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi ambayo unaweza kutumia kuibadilisha dunia. Nimejifunza kwamba ujasiri haumaanishi kuwa hakuna hofu, lakini ni ushindi dhidi yake. Mtu jasiri sio yule ambaye hatishiki, lakini ni yule anayeshinda.”

Mandela alitumia maneno hayo kuwapa hamasa watu wa Afrika Kusini na Waafrika wengine akiwasisitiza umuhimu wa kujitawala na kuacha kuwategemea Wazungu ambao walikuwa wanalitumia bara la Afrika kujinufaisha. Afrika ni bara ambalo Mungu ametubariki kuwa na kila kitu, Lakini bado tumenyimwa maarifa ya kuzitumia rasilimali zetu kutuletea Maendeleo.

Afrika tunalia na umaskini wakati tumekalia utajiri. Ufahamu wetu unaamuliwa na elimu ambayo kwa kiasi kikubwa unaamuliwa na watawala wetu. Waliotutawala mwanzo ndio waliohusika kutuandikia historia yetu na vitu vya kusoma. Hivyo, ukoloni mambo leo haupo kwenye kutusaidia kwenye Uchumi tu, lakini pia mifumo ya elimu inatuandaa kuwasoma zaidi wao kuliko kuusoma utajiri tulionao na namna unavyoweza kutusaidia.

Ili Afrika tuweze kujitegemea, kwanza tunapaswa kubadilisha mfumo wetu wa elimu ambao kwa kiasi kikubwa hautuandai kujitegemea. Nchi tajiri Duniani ndizo zinatupangia nini tufanye na nini tuache. Bado tunatawaliwa na ukoloni mpya ambao umegubikwa na teknolojia ya maarifa.

Uhuru wetu ni wa kwenye fikra, lakini si uhuru ule ambao umetukomboa katika nyanja zote. Ni uhuru gani ambao Afrika hatuwezi gundua hata dawa ya kutibu mafua? Yaani kibaya zaidi hata miongoni mwetu akigundua bado hata sisi wenyewe hatuiamini. Tunaamini kilichotoka nje ndicho bora.

Labda niwakumbushe tu kuwa 30% ya madini yote duniani yanapatikana Afrika huku (asilimia 40 ikiwa ni dhahabu) Nusu ya almasi yote duniani, ikitoka kusini na Afrika ya Kati. Lakini, haya madini bado yametuacha na umaskini wa kutupwa.

Hatuwezi kusema tupo huru kama bajeti ya nchi tunategemea wafadhili. Hatuwezi kusema tupo huru kama dawa za kulinda afya zetu tunategemea nje. Hatuwezi kusema tupo huru kama mbegu bora za kupanda tunaagiza nje n.k, hapo uhuru wetu unabaki kuwa wa maneno na si kwa vitendo.

Mwalimu Nyerere alikuwa anatuandaa kujitegemea walau kwa kiasi kikubwa. Alitambua kuwa nchi haiwezi kujitegemea kwenye kila kitu na aliamini kuwa kidole kimoja hakivunji chawa. Katika imani yake hiyo alianzisha kitu kinachoitwa siasa ya kujitegemea. Mtu alifundishwa kujitegemea/ kupambana na mazingira yake tangu darasa la tatu.

Nyerere aliamini kwenye viwanda na kilimo akijua ndivyo vitaleta mapinduzi ya Uchumi kwa watu wake. Leo hatuna viwanda hata dawa ya kuulia wadudu tunaagiza nje wakati tuna Pareto. Mchele tunaagiza nje wakati tuna mashamba. Yote haya ni matokeo ya ukoloni mambo leo ambao ulileta elimu ambayo haitoi mwanya wa kufikiria zaidi kuwa bila msaada tunaweza hasa tukiwekeza kwenye Elimu ya vitendo na si vyeti. Ndiyo maana Afrika watu wanapata kazi kwa GPA hata kama hiyo GPA ulinunua badala ya kutoa kazi kwa maarifa aliyo nayo mtu.

Afrika ndilo bara ambalo nchi zake zinakopa sana katika benki ya Dunia na Mashirika mengine Duniani. Kutokana na mikopo hiyo Afrika inaishia kulipa Madeni hayo kwa riba kubwa na kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo. Ni wakati sasa kwa bara la Afrika kuungana na kauli ya Rais Yoweli Museveni ambaye aliwahi kusema, sasa ni wakati wa Afrika kufungua milango ya soko la Afrika.

Museveni alisema, Afrika tukiimarisha soko la pamoja itarahisisha kuuza bidhaa zetu na kukuza uchumi wa Afrika. Sina uhakika kama hili lilieleweka. Lakini, ni wazi kuwa ukisoma mawazo ya waasisi wa Afrika kwa mfano Mwalimu Nyerere, Nkurumah, Mandela, Robert Mugabe na wengine walitamani kujenga Afrika inayojitegemea. Waliamini kuwa ili Afrika iweze kupambana na Mataifa mengine Duniani, ni lazima kujitegemea na kujenga uchumi imara.

Hatuwezi kujitenga na Dunia, lakini tunapaswa kuwa makini. Mambo haya yanabadilika kulingana na wakati ndio maana mwanzo utandawazi ulikuwa ni wa kutafuta Watumwa kwa ajili ya mashamba ya Wazungu. Lakini, baadae ugunduzi wa teknolojia nyingine ya viwanda Mataifa makubwa yaliachana na utumwa na kuamini kuwa Afrika ni bara kwa ajili ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vyao.

Leo hii pamoja na kutegemea malighafi za Afrika bado hata soko wanategemea Afrika. Je, Afrika imejiandaa kupambana? Hayati Magufuli alijitahidi kuonyesha kutaka kutunishiana nao misuli kuwa Tanzania tunaweza kujitegemea. Aliishia kukutana na vikwazo mbalimbali na hata Watanzania wengine kuwa washirika wa hao ambao ni watesi wa Afrika.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hivi, ‘Ni vipi tunaweza kutegemea mikopo na uwekezaji wa kigeni na makampuni ya kigeni bila kuhatarisha uhuru wetu? Ili tujenge nchi ya kujitegemea ni lazima tuwe na viwanda vingi. Ulaya walilitambua hilo ndio maana wamejiimarisha kwa viwanda.

Hakuna mjomba wa kumtegemea atupe misaada ya bure. Lazima tujitegemee. Duniani kuna kujitegemea. Unaweza kutegemea. Na kutegemea popote ni kubaya sana, lakini kutegemea (kubaya) kupita kote kabisa kabisa ni kumtegemea mtu mwingine kwa mawazo. Ni kutegemea kwa hovyo sana. Kuna kunyima utu wako.”

0768 239 284

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here