WAZIRI Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unapaswa kulindwa na Watanzania wote kwani ni Tunu ya Taifa ambayo imeifanya nchi kuwa na Umoja na Ushirikiano.
Waziri Masauni ameyasema hayo Aprili 22, 2025 wakati wa mahojiano maalumu kwenye kipindi cha ‘Jambo Tanzania’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambapo amesema Muungano huu umekuwa na mafanikio makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
“Kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi, hivyo katika hoja 25 zilizokuwepo hadi sasa hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na hoja tatu zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi.
“Tunatambua vijana wengi wamezaliwa baada ya Muungano ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa na utaratibu wa utoaji wa elimu kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari, Midahalo na Semina,” alisema Masauni.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu inasema ‘Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025’.