KAMATI ya Siasa ya Wilaya ya Kibaha imefanya ziara leo, Februari 12, 2025, kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya halmashauri na kuonyesha kuridhishwa na usimamizi wake.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha, Mkali Said Kanusu, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Regina Bieda, kwa umakini wake katika kusimamia miradi hiyo, akibainisha kuwa itaongeza fursa kwa vijana na kuchochea uchumi wa Kibaha Vijijini.

Kwa upande wake, Bieda ameahidi kuendelea kushirikiana na wataalamu wa halmashauri na wakandarasi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na stendi mpya ya Mlandizi iliyopo Kata ya Matambani, Shule ya Ufundi (Amali) katika Kata ya Ruvu, Kongani ya Viwanda ya Kwala, Mradi wa Vijana wa Ufugaji Kuku, pamoja na Hospitali ya Wilaya.

Katika hitimisho la ziara hiyo, Bieda ametoa wito kwa kamati ya siasa kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura, linaloanza Februari 13 hadi 19, 2025, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni.