WATUMISHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wamepongeza jitihada za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Regina L. Bieda, kwa kuratibu mafunzo maalum ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yaliyofanyika leo katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Utumishi Edward Masona aliishukuru menejimenti ya PSSSF kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu na kuwataka watumishi kusikiliza kwa makini ili kujiongezea uelewa kuhusu haki na manufaa yao ya kisheria.
“Mfuko wa hifadhi ya jamii unagusa moja kwa moja maisha ya mtumishi wa umma, wakati wa utumishi na baada ya kustaafu. Ni muhimu kila mmoja kupata weledi wa kutosha ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye,” alisema Masona.
Kwa upande wake, Afisa Mafao kutoka PSSSF, Abraham Kiishwako, alieleza kuwa PSSSF hutolewa mafao makuu matano ambayo ni Mafao ya Muda Mrefu, Mafao ya Uzeeni, Mafao ya Ulemavu, Mafao ya Kifo na Mafao ya Wategemezi.
Aidha, aliwasisitiza watumishi wapya kujiandikisha kidigitali kupitia PSSSF Portal ili kupata taarifa za michango yao kwa urahisi na kuendelea kunufaika na huduma za kisasa za mfuko huo.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Ramadhani Mang’walu na Tutindaga Ngomale, walimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa fursa hiyo, wakibainisha kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kupanga maisha yao ya kikazi na baada ya kustaafu kwa ufanisi zaidi.
Akihitimisha mafunzo hayo ya siku moja, Masona aliwataka watumishi wote kuzingatia maelekezo ya maafisa wa PSSSF ili kuondoa usumbufu wa madai ya mafao katika siku zijazo.