Mfumo wa BPS ulivyoleta Mapinduzi sekta ya mafuta nchini

0
Erasto Mulokozi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja ( Petroleum Bulk Procument Agency - PBPA).

Na Iddy Mkwama

MIAKA kadhaa iliyopita, biashara ya mafuta wakati soko lilipoachwa huru, kulijitokeza changamoto nyingi ambazo zilisababisha usumbufu mkubwa na taharuki nchini.

Ni wakati huo ambao hakukuwa na sheria na kanuni thabiti ya kusimamia sekta hiyo na kusababisha uhaba wa mafuta na kuibuka kwa wimbi la uwekezaji ulio chini ya kiwango katika miundombinu ya mafuta.

“Vituo vilikuwa vinajengwa chini ya kiwango na kulikuwa na uchakachuaji wa mafuta kwa kuchanganya mafuta ya taa na mafuta ya dizeli kwa sababu mafuta ya taa yalikuwa yanatozwa kodi ndogo kuliko dizeli na kuyauza kama dizeli,” anasema Erasto Mulokozi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja ( Petroleum Bulk Procument Agency – PBPA).

Mulokozi anasema, changamoto nyingine ni kampuni za mafuta zilikuwa zinauza mafuta bei ya juu kwa kisingizio cha kupanda kwa bei ya nishati hiyo kwenye soko la dunia wakati wafanyabiashara hao walikuwa na akiba ambayo walinunua kwa bei ya chini.

“Hata hivyo pale ambapo bei ya mafuta ilikuwa inashuka waliendelea kuuza mafuta kwa bei ya juu; vile vile waagizaji wa mafuta walikuwa wanaweka gharama kubwa za uagizaji (premium) ambazo zilikuwa hazina uhalisia wa bei halisi katika soko,” anasema.

Aliendelea kusema kuwa, kipindi hicho cha soko huria la mafuta, Kampuni zilikuwa zinaleta shenena ndogo ndogo za tani 5,000 hadi tani 10,000 hivyo kusababisha mlundikano wa meli zinazosubiri kupakua mafuta “Meli zilikuwa zinasubiria kati ya siku 30 mpaka 60.”

Mulokozi anasema, changamoto nyingine iliyogubika sekta ya mafuta kwa kipindi hicho, ni vitendo vya ukwepaji kodi kupitia udanganyifu wa kiasi na aina ya mafuta iliyotetwa pamoja na kuuza mafuta ya ‘transit’ katika soko la ndani.

“Wamiliki wa hifadhi za mafuta walikuwa wananaweka bei kubwa za utunzaji wa mafuta zilizofikia hadi Dola za Marekani 20 kwa mita za ujazo kwa waliohitaji kutunziwa mafuta katika hifadhi hizo,” anasema na kuongeza kuwa, yote hayo yalijitokeza kwasababu hakukuwa na uratibu mzuri kwa wadau muhimu wa sekta ndogo ya mafuta.

Katika jitihada za kutatua changamoto hizo, Serikali ilianzisha mifumo mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa EWURA, kutunga Sheria ya Petroli, kuanza utaratibu wa kupanga bei za mafuta, kuanzisha mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, kuongeza kodi katika mafuta ya taa na kuanzisha utaratibu wa kuweka vinasaba katika mafuta.

Wakati utekelezaji wa mifumo mingine ukiendelea, mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja (Bulk Procurement System – BPS) umeonekana kuleta mapinduzi makubwa zaidi kwenye sekta ya mafuta na sasa umekuwa kivutio kwa nchi nyingine za jirani.

“Ili kuhakikisha kwamba ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini iliandaa Kanuni za Kusimamia Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum (Bulk Procurement) Regulation-2011). BPS ni mfumo wa usimamizi wa uagizaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kwa pamoja (Bulk Importation),” anasema Mulokozi.

Ni mfumo ambao unasimiamiwa na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja ( Petroleum Bulk Procument Agency – PBPA), ambao nao ulianzishwa mwaka 2015, kwa Kanuni ya Wakala wa Serikali, ya mwaka 2015 kupitia Tangazo la Serikali Na. 423 la Septemba 25, 2015.

“Kanuni hii iko chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agencies Act, Cap. 245); ndipo PBPA ikachukua majukumu ya iliyokuwa PICL na kuanza kusimamia mfumo wa BPS kuanzia Januari 2016,” anasema.

Akitaja baadhi ya majukumu ya PBPA, Mulokozi anasema ni kusimamia mfumo wa Uagizaji wa Pamoja wa mafuta nchini na kuhakikisha mafuta yanaletwa kwa njia yenye ufanisi (efficient procurement) na kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya nchi wakati wote.

“Majukumu ya msingi ya Wakala ni kusimamia mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS); kukusanya mahitaji ya mafuta na kutangaza zabuni kwa ajili ya kuleta mafuta nchini, kusimamia mikataba ya uagizaji mafuta na kuhakikisha mafuta yaliyoagizwa yanafika nchini kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kulingana mikataba husika,” anasema.

Aliendelea kutaja majukumu mengine ya PBPA ni kuhakikisha mafuta ya kutosha yanakuwepo nchini wakati wote (security of supply), kusimamia taratibu za uagizaji zenye ufanisi katika kuleta mafuta nchini.

“Taratibu hizi hujumuisha usajili wa Kampuni za Biashara ya Jumla ya Mafuta nchini (OMCs), usajili wa Wazabuni (Prequalification of Suppliers); upokeaji wa mahitaji ya mafuta kutoka kwa OMCs, uchakataji wa mahitaji yaliyopokelewa, utangazaji na ufunguzi wa zabuni za kiushindani wa Kimataifa,” anasema.

Majukumu mengine kwa mujibu wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa PBPA ni kusimamizi wa utekelezaji wa mikataba, kupanga ratiba za meli zinazoleta shehena za mafuta nchini, kutunza taarifa za meli zilizoleta mafuta.

Kutokana na kuanzishwa kwa PBPA na kusimamiwa kikamilifu kwa mfumo wa BPS, sekta ya mafuta imeopata manufaa makubwa ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa wakati wote (security of supply).

Manufaa mengine ni kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta (premium) Kutokana na Uagizaji wa Pamoja (economies of scale) kwa wastani Zaidi ya Dola za Marekani Milioni 200 sawa na Shilingi Bilioni 500 huokolewa kila mwaka kupitia mfumo wa BPS.

“Kwenye soko bei ya mafuta imepungua kutokana na Uagizaji wenye ufanisi, pia mapato ya kodi yameongezeka kutokana na kupungua kwa vitendo vya vitendo vya ukwepaji kodi kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya OMCs,” anasema Mulokozi.

Manufaa mengine ni kuthibiti udanganyifu katika gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uletaji wa mafuta, kupunguza msongamano wa meli bandarini.

“Katika hili wastani wa Dola za Marekeni Milioni 170 sawa na Shilingi Bilioni 425 huokolewa kila mwaka ikilinganishwa na gharama za demurrage zilizokuwa zikilipwa kabla ya mfumo wa BPS,” anasisitiza.

Mbali na manufaa hayo, nchi za jirani nazo zinatumia mfumo huo katika ununuzi wa mafuta, hivyo kuipatia Serikali mapato kutokana na Kuongezeka kwa matumizi ya bandari.

“Kwa sasa Uagizaji wa mafuta kwa ajili ya nchi Jirani umefikia wastani wa asilimia 55% ya kiwango cha mafuta kinachoagizwa kupitia BPS kutoka wastani wa asilimia 33 za awali,” alifafanua na kuongeza kuwa, hata upotevu wa mafuta wakati kwa kupakua mafuta kutoka melini umepungua kwa kiasi kikibwa.

“Wastani wa tani 1100 (sawa na lita 1,300,000) huokolewa kila mwezi, sawa na takriban Shilingi Bilioni 4.16 kwa bei kikomo za Disemba 2023. Hivyo kwa mwaka takriban Shilingi Bilioni 49.9 huokolewa,” anasema.

Akizungumzia uwezo wa uwezo wa Maghala ya kuhifadhi Mafuta nchini, Mulokozi anasema, Tanzania ina maghala 22 yenye uwezo wa kupokea mafuta kutoka kwenye meli katika Bahari ya Hindi, ambapo Maghala hayo yana uwezo wa kupokea jumla ya takribani lita bilioni 1.31 kwa aina nne za mafuta ya petroli (dizeli, petroli, mafuta ya ndege & mafuta ya taa).

Hata hivyo, kila penye mafanikio hapakosi changamoto, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja Erasto Mulokozi anasema, mfumo wa BPS unakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo wanajitahidi kukabiliana nazo.

Moja ya changamoto hizo ni wakati wa kipindi cha janga la UVIKO-19, mahitaji ya mafuta mafuta yalipungua kutokana na kusimama shughuli nyingi za kiuchumi.

“Hali hii ilisababisha meli kutumika kama hifadhi za mafuta, hivyo kuchangia uhaba wa meli na kufanya gharama za usafirishaji kuongezeka kwa kanuni ugavi na uhitaji (Supply and Demand). Aidha, katika kipindi hicho bei ya mafuta (FOB) ilishuka kwa kiwango kikubwa sana,” anasema.

Anasema, changamoto nyingine ni vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine imesababisha bei ya mafuta (FOB) na gharama za kuyafikisha nchini (premium) kuongezeka kwa kiwango kikubwa.

“Hivi sasa kuna uhitaji mkubwa wa Dola za Marekani kuliko uwezo uliopo na kusababisha kiasi kikubwa cha mafuta kuwa kwenye ‘financial hold’ na hivyo gharama za kuleta mafuta zimeongezeka,” anasema.

Mulokozi anasema, kwasasa kuna ongezeko la kiasi cha mafuta kinachoagizwa kutoendana na uwezo wa miundombinu ya upokeaji mafuta, ambapo miundombinu iliyopo imekuwa ikitumika toka kuanza kwa BPS wakati kiasi cha mafuta kilichokuwa kinaagizwa kwa mwezi ilikuwa ni wastani wa tani 200,000 hadi 250,000.

“Kwa sasa kiasi cha mafuta kinachoagizwa kwa mwezi ni wastani wa tani 450,000 – 600,000; Kutokuwepo kwa ghala kubwa la kupokelea mafuta kwa pamoja hivyo kupelekea meli kuchukua muda mrefu kupakua mafuta. Dar es Salaam pekee ina Jumla ya maghala 19,” anasema.

Aidha, alitaja baadhi ya hatua ambazo zimechukuliwa ili kukabiliana na changamoto hizo ambapo Wizara ya Nishati imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ili kupunguza makali ya uhaba wa Dola za Marekani ambapo maamuzi kadhaa yamefanyika na kuleta unafuu.

“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi atayeboresha miundombinu ya upokeaji mafuta katika bandari ya Dar es Salaam. TPA inatarajia kusaini mkataba na mkandarasi huyo mwezi huu wa Disemba 2023,” anasema Mulokozi.

Anasema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha nishati ya mafuta inapatikana wakati wote na kwa bei nafuu.

“Serikali imetoa ruzuku kwenye gharama ya mafuta kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2022 hadi Disemba 2022 ili kupunguza bei ya mafuta kwa wananchi iwe stahimilivu, hii ilifanyika baada ya athari ya bei ya mafuta kupanda sana katika soko la dunia kutokana na vita baina ya Urusi na Ukraine,” anasema.

Mchango mwingine wa Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa ikitoa kiasi cha Dola za Marekani kwa benki za biashara ili ziweze kulipia mafuta yanayotumika nchini na baadhi ya miongozo ya udhibiti wa Dola za Marekani ilibadilishwa ili kuwezesha benki za biashara kupata fedha hizo kutoka sokoni.

“Serikali kupitia PBPA ilibadilisha mikataba ya uagizaji mafuta na kuruhusu matumizi ya fedha nyingine za kigeni katika ulipiaji mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi; Serikali kwa kupitia taasisi wadau imefanya mapitio ya nyaraka mbalimbali zinazosimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ili kuimarisha usimamizi wa Sekta ndogo ya Mafuta,” anasema.

Anaendelekea kusema: “Serikali kupitia Mamlaka zake imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala ya kuhifadhia mafuta ili kuhakikisha taratibu za uendeshaji wa maghala hayo zinazingatiwa; Serikali imewezesha ushirikiano mzuri baina ya taasisi wadau katika Sekta Ya Mafuta ili kuboresha ufanisi wa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta Kwa Pamoja. Taasisi hizo ni Pamoja na TRA, EWURA, WMA, TBS na PBPA.”

Mbali na hayo, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umeendelea kuboresha mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS) ili kuendelea kupata bei halisia kutoka kwenye soko la dunia, kuongeza kiwango cha mafuta kupitia Mfumo wa Uagizaji kwa Pamoja na kuvutia waletaji wengi zaidi kushiriki katika mfumo huu, hasa nchi zilizotuzunguka (land locked countries) ambazo zinategemea bandari za hapa nchini.

“Wakala utaendelea kushirikiana na taasisi wadau katika kuboresha zaidi mfumo huu ili uendelee kuongeza tija kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla,” alimaliza Erasto Mulokozi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), wakati akizungumza kwenye kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here