Mfuko wa madeni, Hatifungani za SUKUK hesabu ngumu kwa ACT

0

Na Joseph Zablon

WAKATI Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), 2020 ilipotaka ridhaa ya wananchi kuunda Serikali, ilinadi sera kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), chini ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kwenye uchaguzi huo, mgombea Urais wa chama hicho tawala alipata ushindi wa asilimia 76.27 na mpinzani wake Maalim Seif Sharrif Hamad wa ACT Wazalendo aliambulia asilimia 19.

Baada ya uchaguzi huo, iliundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo.

Kulingana na takwimu za ilani ya chama hicho hadi sasa imetekelezwa kwa asilimia 100 na kupitiliza, jambo ambalo linaibadili kabisa Zanzibar na kuifungua kiuchumi maradufu.

Miradi yote inahitaji fedha katika utekelezaji na jinsi ya kupata pesa ndio kipimo cha kinara wa utekelezaji na timu yake ambayo ni baraza la mawaziri, mabaraza ya miji na wananchi kwa ujumla.

Kasi ya utekelezaji, mabadiliko makubwa yanayotokana na ujenzi wa barabara, shule za msingi na sekondari za ghorofa, maabara na vifaa vya kisasa vya kujifunza na kufundishia, zikiwemo kompyuta vinachochea maendeleo ya Zanzibar.

Aidha, kwa kipindi alichoingia madarakani Dkt. Mwinyi, nyumba za watumishi wa afya na walimu, masoko ya kisasa yamejengwa, huku boti za uvuvi, mikopo kwa vikundi vya vijana na kinamama ikitolewa.

Vile vile, uwekezaji unaofanywa katika ujenzi wa hoteli kubwa, nyumba za kisasa za makazi, maji, umeme na miundombinu mingine inavutia uwekezaji kwa wageni.

Pia, ujenzi na uwekezaji katika visiwa ambavyo awali havikuwa vinatumika au kukaliwa na watu, uchumi wa bluu, umefungua fursa za ajira kwa wananchi.

Kuna wanafalsafa ambao wanaamini hesabu ni ngumu na wapo wanaoamini kuwa hakuna somo rahisi kama hisabati.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Othman Soud Othman, haieleweki iwapo kwake hesabu ni ngumu au rahisi.

Sio kwake tu, hata Makamu Mwenyekiti wake, Jussa Ismail Ladhu naye bado haijaeleweka yupo kwenye kundi gani kati ya hayo mawili; wanaoamini hesabu ni ngumi au rahisi.

Hata hivyo, kinara wa mabadiliko makubwa ya maendeleo Zanzibar Dkt. Hussein MwinyĆ­ anasema, anajua nia ya wanasiasa hao wa upinzani.

Wananchi wengi visiwani Zanzibar, wanaonekana kumshangaa Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo, ambaye anaibeza miradi hiyo na kudai mikopo kwa ajili ya utekelezaji wake, imezua madeni makubwa ambayo hayaimiliki.

Anaenda mbali zaidi katika hotuba yake anazibeza hata barabara zenyewe kuwa hazina hadhi, ni vichochoro tu; nadharia ambayo inazua maswali mengi kuliko majibu.

Kulingana na hesabu za Mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Makamu wake Jussa, zinadai deni la Taifa limepanda na halimithiliki.

Mwenyekiti Othman anasema, mwaka 2020/2023 deni la Taifa lilikuwa Shilingi Bilioni 887 na sasa limefikia Shilingi Trilioni 2.3, ongezeko ambalo sawa na upandaji kwa asilimia 208.

Mwanasiasa huyo anaenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa kulingana na ilivyo kila Mnzanzibari hadi mtoto mchanga, anadaiwa kiasi cha Shilingi 119,000 madai ambayo yanakanushwa.

Rais Dkt. Mwinyi anasema, madai hayo ni propaganda zisizo na maana zinazotiwa uongo ili ziwe tamu.

Anasema, wakati wanaingia madarakani deni la Taifa lilikuwa Shilingi Bilioni 800 na sasa limepanda hadi Shilingi Trilioni 1.2 sawa na asilimia 50 na si asilimia 208 kama inavyodaiwa.

Kiwango hicho cha deni ni himilivu na nchi inaweza kukopa zaidi ikitaka, pia kuna mfuko wa madeni ambako SMZ kila mwezi inaingiza Dola za Kimarekani Milioni 250 (Bilioni 600).

Anabainisha kuwa, kama Serikali ikikusanya kutoka kwenye mfuko wake kwa miezi miwili, ina maana wanaweza kulipa deni lote kwa wakati mmoja, hivyo haoni kwanini wasiendelee kukopa.

Dkt. Mwinyi anasema, Serikali kuu kila mwezi inakusanya Shilingi Bilioni 300 na uzinduzi wa karibuni wa Hatifungani za SUKUK zisizo na riba, zinafungua wigo mwingine zaidi wa mapinduzi ya kifedha Zanzibar.

Hatifungani hizo zinafungua fursa pana zaidi ya Serikali kukopa na zitaiwezesha kifedha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) hivyo watakuwa na uwezo wa kutoa mikopo mikubwa kwa makampuni na taasisi.

Benki hiyo ambayo Jussa awali alidai inaenda kuuzwa, itakuwa na uwezo wa kutoa mikopo mikubwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwa wafanyabiashara na watu binafsi.

Wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida wana nafasi ya kuwekeza, kiwango cha kuanzia ni Shilingi Milioni 1.

Hatifungani hizo, zinatoa faida asilimia 10 na faida yake mara mbili kwa mwaka na baada ya miaka saba mwekezaji anaweza kuondoa mtaji wake ama kuwekeza zaidi na ni wazi kwa watu wa dini zote.

Hatifungani hizo ni faraja kwa waliokuwa wakitatizwa na riba zinazotozwa na mabenki ya biashara jambo ambalo ni kinyume na imani ya dini yao.

Miradi hiyo ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii, miundombinu, uwekezaji, mazingira mazuri ya kibiashara na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mara kadhaa Rais Dkt. Mwinyi anajivunia kutimiza ahadi zake kwa wananchi, lakini upande wa pili miundombinu inavutia uwekezaji.

Ndio maana, kuna wanaoamini hakuna somo gumu kama hesabu na pia wapo wanaoona hakuna somo rahisi kama hisabati na upotoshaji pia upo, lakini hesabu hazidanganyi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here