WIZARA ya Fedha imeendelea na mchakato wa kupitia upya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, kwa lengo la kuioanisha na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kupitia kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.
Wizara imeendelea na mchakato huo ikiwa ni kikao kazi cha pili kufanyika ambapo wadau mbalimbali walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Sheria hiyo, katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Hazina, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Emma Komba, alisema mapitio hayo yanalenga kujenga mfumo wa kisasa unaojumuisha hatua zote za mnyororo wa ugavi, kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi, upokeaji na ugomboaji, uhifadhi na utunzaji, usambazaji, hadi uondoshaji wa mali.
Alisisitiza kuwa mapitio hayo ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha kuwa masuala yote yanayohusu mnyororo mzima wa ugavi yanajumuishwa kikamilifu katika Sheria mpya, na kwamba mageuzi hayo yatakuwa chachu ya kuchochea maendeleo ya Taifa.
Komba aliwahimiza wadau wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni na kukisisitiza kuwa ushiriki wao ndio utakaohakikisha Sheria mpya inakuwa bora, jumuishi na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.
Kikao hicho, kilichoratibiwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, kiliwakutanisha pamoja wadau mbalimbali kutoka Sekta ya umma na binafsi.
Kwa upande wa sekta ya umma, taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), TANROAD, SUMAJKT pamoja na Benki ya Maendeleo ya TIB.
Kwa upande wa sekta binafsi, walishiriki walikuwa Benki ya NBC, Soft tech consultancy, Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Cross World Travel Agent Limited, Masasi Construction, pamoja na Perfect Infotech International, ambao walipata fursa ya kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya biashara na ushiriki wao hasa kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za ununuzi wa umma na ugavi.