Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kupitia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote.
Akiwasilisha taarifa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge la Bajeti Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, Mei 6, 2026 bungeni jijini Dodoma amesema, mafanikio makubwa yaliyofikiwa, changamoto zilizojitokeza pamoja na mikakati kabambe ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini unachagizwa na juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mchengerwa amesema, utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ulianza rasmi Januari 26, 2026, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kikwazo cha uwezo wa kifedha.
Amesema kuwa, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, Serikali ilipanga kusajili jumla ya kaya 276,004 zisizo na uwezo, ambapo hadi mwezi Aprili, 2026 kaya 172,297 tayari zimesajiliwa ambayo ni sawa na asilimia 62 ya lengo
Aidha, amesema zaidi ya wananchi 463,000 tayari wamenufaika na mpango huo, huku zoezi la usajili likiendelea ili kuwafikia wananchi zaidi ya 500,000 waliobaki katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema, Serikali imechukua hatua za kuongeza kasi ya usajili kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa kwa ufanisi zaidi.
Katika eneo la fedha, Mchengerwa amesema, Serikali imekusanya asilimia 72 ya fedha ambazo zinatumika kugharamia bima ya afya kwa kaya zisizo na uwezo.
Amefafanua kuwa, asilimia kubwa ya fedha hizo imeelekezwa moja kwa moja katika kugharamia huduma za afya kwa wananchi, huku sehemu nyingine ikitumika kwa huduma za magonjwa sugu, dharura pamoja na shughuli za uendeshaji na utoaji wa elimu kwa umma.
Aidha katika mageuzi ya kidijitali, Waziri Mchengerwa amesema Wizara inaendelea kuunganisha mifumo ya huduma za afya na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, kupunguza udanganyifu na kuharakisha malipo ya madai kwa watoa huduma.
Ameongeza kuwa, mfumo wa Health Data Universal (HDU) umeanza kutumika katika vituo mbalimbali vya afya nchini, ukiwezesha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa za wagonjwa kwa wakati na kwa usahihi zaidi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na malipo kwa watoa huduma unafanyika kwa wakati, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga na kulinda imani ya wananchi kwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.