Mbio za kukinadi Chama cha Mapinduzi Mkoani Geita zaanza kwa kishindo

0

📌 Majimbo 7 kati ya 9 yapita bila kupingwa

📌 Kata 92 kati ya 122 zapita bila kupingwa

📌 Maelfu wakusanyika kusikiliza Ilani ya CCM 2025-2030

📌 Dkt. Biteko awasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan

📌 Asisitiza mshikamano kabla na baada ya uchaguzi

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita leo Septemba 2, 2025 kimezindua kwa kishindo kampeni za kuinadi Ilani ya CCM 2025-2030 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo imeelezwa kuwa mpaka sasa tayari Majimbo 7 kati ya 9 ya Ubunge yamepita bila kupingwa huku kata 92 kati ya 122 zikipita bila kupingwa.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe, Mkoani Geita ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo, Nicholaus Kasendamila amesema Chama cha Mapinduzi kinaingia kwenye kampeni kikiwa na mtaji mkubwa wa uadilifu, uaminifu, uchapakazi na busara ya mgombea Urais wa kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kupitia kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, CCM inazo sababu za kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza nchi akisema kuwa amefanya maendeleo mengi ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kubwa la biashara kwaTanzania na nchi jirani, amejenga daraja refu la Busisi, amekamilisha ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere (MW 2,115) na reli ya kisasa imeshaanza kufanya kazi.

Kasendamila amesema kuwa katika Mkoa wa Geita, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 imetekelezwa kwa mafanikio ambapo ameeleza kuwa shule mpya za msingi 151 zimejengwa, Shule za sekondari mpya 118 zimejengwa, zimejengwa hospitali mbili za rufaa, hospitali za wilaya mpya 4 na vituo vya afya 17 vipya vimejengwa.

Ameongeza kuwa, kupitia Ilani ya CCM 2020-2025, zahanati 69 zimejengwa, leseni za madini 7600 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na kuhusu umeme, kabla ya kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Sita kulikuwa na vijiji 362 tu vyenye umeme lakini sasa vijiji vyote 486 mkoani Geita vina umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here