Mbeto: Wenye malalamiko ya mchakato wa kura za maoni wawasilishe kwenye mamlaka husika

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeelekeza malalamiko yoyote kuhusiana na mchakato wa kura za maoni uliofanyika Agosti 4, 2025 yawasilishwe kwa barua kwa mamlaka husika.

Akizungumza kuhusiana na mchakato wa kura na maoni na wanahabari, Katibu Kamati Maalum (NEC), Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, hatarajii kitu kama hicho kutokana na maandalizi na utaratibu mzima ulivyo na jinsi wasimamizi na wagombea walivyoandaliwa.

Mbeto alisema, utaratibu ulivyo baada ya kura kupigwa, zitamwagwa na kila mgombea atahesabu kura zake.

“Sitarajii malalamiko na ikitokea malalamiko yoyote kwa wagombea waandike barua mamlaka husika,” alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa, anaamini maofisa uchaguzi wa chama wametekeleza kwa uadilifu na kutenda haki.

Mbeto alisema, wajumbe wamekuwa na jukumu kubwa la kuwawakilisha wananchi wote kupata mgombea mzuri anayetakiwa na watu wote.

“Nilisema wachaguliwe wachapakazi, waadilifu, wanaokubalika na watu watakaoenda kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema Mwenezi Mbeto.

Ingawa Mbeto alisema, anajua kuwa kuna watu wamegeuza uchaguzi kuwa gulio la kununua na kuuza kwa baadhi ya wana CCM, lakini anaamini wajumbe wamewapigia kura watu ambao wakisimamishwa mbele ya wananchi watakubalika.

Alisema, hilo litawapunguzia kazi viongozi wa juu kwani kati yao wawakilishi na wabunge ndio wataunda baraza la mawaziri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here