Mbeto: Upinzani umekosa Sera za kukishinda CCM Oktoba 29

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema upinzani hauna uwezo wa kukishinda CCM kwakuwa Sera zao zinahimiza Siasa za Ubaguzi, kuvunja Muungano uliopo na kuvuruga Amani.

CCM kimesema, kwa muktadha na tathmini ndogo iliofanyika kuelekea Oktoba 29 Mwaka huu, upinzani umeshindwa kabla wananchi hawajapiga kura.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis amesema, upinzani unaozungumzia sera za migwanyiko katika jamii, umeshindwa kueleweka mbele ya Watanzania Milioni 70.

Mbeto alisema, Watanzania kwa miaka 61 wamekuwa wakiishi chini ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, kuheshimu misingi ya Umoja, Udugu, Utulivu na Mshikamano, hivyo hawatakichagua chama chenye sera za kuwagawa.

Akisema na kukitolea mfano ACT Wazalendo ambacho kimekuwa mstari wa mbele kuhubiri sera za ubaguzi, ukabila na asili za watu, alisema kutaja masuala hayo kwa watanzania Wazalendo ni zaidi ya matusi.

“Watanzania wako tayari kusikiliza sera yoyote lakini isiwe sera za kibaguzi na kuvuruga Amani ya Taifa. Siasa za Ubaguzi, ukabila na udini kwa Watanzania ni sawa na laana,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema, Watanzania hawajui tabia za kuuana wenyewe kwa wenyewe, hawatamani kubaguana kwa rangi, kabila wala kwa dini zao, kwani wamezoea kuishi kwa salama na amani.

“Hayupo Mtanzania ambaye ni bora mbele ya watanzania wenzake. Anayefikiri yeye ni mbora kuliko wenzake, aidha kwa rangi yake, asili na kabila lake, huyo kwa Watanzania ni zaidi ya kituko,” alieleza.

Mbeto kwa kuthibitisha hilo, alisema ndio maana toka Mwaka 1995 hadi 2020 kwa nyakati, Serikali za CCM zimekuwa katika juhudi za kuunda kamati mbalimbali zilizokuwa zikitafuta mkakati wa kufikia miafaka ya kisiasa.

“Alipoingia madarakani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkakati wake wa kwanza aliirudisha nchi katika reli yake ya umoja na mapatano. Alifanya hivyo na kufanikiwa kuiweka nchi katika jamvi moja la maridhiano,” alifafanua.

Mbeto alisema, Mkuu huyo wa nchi alikwenda mbali zaidi, akaibuka na kanuni ya R Nne, ambazo zimekuwa ufunguo na dira ya kuliiongoza Taifa katika shime moja ya kudumisha udugu na maelewano.

Hivyo basi, Katibu Mwenezi huyo alisema, upinzani unapokwenda kinyume na utamaduni wa sera zinazoviza umoja, wananchi wanaviona vyama hivyo vinatamani shari badala ya maendeleo na kutaka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here