Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesifu juhudi na umakini wa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliingizia Taifa Shilingi Trilioni 9.21 waka 2025 kutoka Trilioni 3.12 mwaka 2020 kwa mauzo ya mazao nje ya nchi.
CCM kimejigamba kwa kuifanya sekta ya kilimo kufikia lengo hilo na juhudi za serikali kwa kukifanya kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khams, aliyesema Serikali ya awamu ya sita imetimiza wajibu wake kwa vitendo nchini.
Mbeto alisema, kupanda mauzo ya mazao ya kilimo nje kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 mwaka 2019 /2020 sawa na kufikia Shilingi Trilioni 3.12 hadi Dola za Marekani Bilioni 3.54 sawa na Shilingi Trilioni. 9.205 Mwaka 2023/2024.
Alisema, ongezeko hilo linaonyesha mkakati kabambe wa serikali katika kuimarisha kilimo kupitia uwekezaji kwa miundombinu ya umwagiliaji, utafiti, pembejeo bora na upanuzi wa masoko ya nje ya nchi.
“Tunaposema Serikali ya Awamu ya sita imechapakazi huwa tuna maanisha si domo mtindi. Sekta ya kilimo imeimarika kutoka asilimia 2.6 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 4.2 mwaka 2023, “alisema Mbeto.
Mbeto aliutaja ufanisi huo umetokana na mikakati ya kisera na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kilimo na ukuaji unaotarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 5 mwaka 2025.
“Kilimo kinatarajia kukua hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2030 ikiwa ni sehemu ya malengo ya muda mrefu ya Serikali na kukua kwa Uchumi kupitia Mapinduzi ya kilimo” alieleza.
Mbeto akizungumzia uzalishaji wa zao la korosho, alisema Tanzania imekuwa kinara wa uzalishaji katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.
“Katika Awamu ya sita korosho uzalishaji umepata msukumo katika na ongezeko kutoka tani 210,786 msimu wa 2020/2021 hadi kufikia 528,263.82 msimu wa 2024/2025, sawa ongezeko la asilimia 150.6,” alisema.
Katibu huyo Mwenezi alitaja ongezeko hilo linaifanya Tanzania kuongoza kwa uzalishaji wa korosho Afrika Mashariki na kuwa ya pili barani Afrika huku ikiwa ya Tano Duniani.
“Mafanikio haya yamatokana na juhudi za Serikali katika kuongeza upatikanaji wa pembejeo bora na huduma za ugani. Serikali imewawezesha Wakulima kupitia mifumo ya Ushirika na Masoko ya uhakika,” alisema Mwenezi Mbeto.