Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema mchakato mgumu wa Uchaguzi ndani ya chama, zoezi la kura za maoni, uteuzi wa wagombea ni kipimo kinachotathmini na kupima uaminifu na utiifu wa kila mwanachama.
Pia, kimeitaja dhana ya Uchaguzi si ombwe la watu kununua uongozi kwa rushwa, bali tafsiri yake iwe ni kukomaa kwa ustawi wa demokrasia ndani ya CCM.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo baada ya kutangazwa majina ya waliopitishwa na mapokeo ya wanachama wengine ambao kura zao hazikutosha.
Mbeto alisema, kila Mwanachama wa CCM aliyewania aidha Ubunge, Uwakilishi, Udiwani au kupitia makundi maalum, Vijana na Wanawake, anapaswa kufuata Kanuni ya RNne.
Alisema, Mwanasiasa au Kiongozi ambaye hajui maana ya RNne, atakosa uvumilivu, anaweza kupoteza shime ya kuamini katika dhana ya mapatano au kushindwa kufikia muafaka wa aina yoyote wa ndani au nje ya chama.
“Mchakato mgumu wa Uchaguzi ndani ya chama ni kipimo cha umakini wa kila mwanachama jinsi alivyopevuka na kuheshimu maadili. Ustahamilivu, kushukuru na kukubali matokeo ni sehemu ya ukomavu,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM, kushusha majina zaidi ya matatu ni ishara ya kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama, pia kipimo cha utiifu kwa kila mwanachama.
“Kila mwanachama anapoingia kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi lengo huwa kushinda. Mwanachama mtiifu hujiandaa kushinda au kushindwa. Lazima kila mmoja ajiandae kisaikolojia kupata au kukosa,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, chama bado kinafuatilia kwa karibu kauli, matamko na matamshi ya wanachama walioshinda na ambao kura zao hazikutosha ili kubaini kauli zao iwapo zimejiegemeza kimaadili.
Vile vile, Mbeto alisema uchaguzi ni shughuli za makundi, hivyo kila uchaguzi mgumu, lazima utoe matokeo chanya au hasi, kupanda kiwango cha nidhamu, demokrasia na ushindani ndani ya chama
“Chama chetu kina kazi nyingi. Si lazima kila mwanachama apate ubunge, Uwakilishi au Udiwani . Subira, nidhamu, uvumilivu na utii humpandisha chati ya heshima mwanachama mtulivu,” alisisitiza Mbeto.