Mbeto: Maelekezo ya Mwenyekiti CCM ni maagizo ya utekelezaji kwa chama

0

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitahakikisha kinayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan katika kupitisha wagombea udiwani, uwakilishi na Ubunge.

Pia, CCM kimesema huu ni wakati sahihi wa kuwang’amua mapema ni wagombea gani waaminifu na wazalendo kwa chama na nchi.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamisi alisema, maelekezo yakitolewa na Mwenyekiti katika mkutano mkuu wa Taifa, ni maagizo ya utekelezaji toka matawi hadi Taifa.

Alisema, CCM kina uzoefu wa kutosha kutokana na tabia ya kukatwa kwa majina ya wanachama wenye utiifu na nidhamu kuachwa na kupendekezwa wagombea wasiokubalika katika jamii.

Alisema, ni lazima sifa za kila mgombea zitokane na juhudi binafsi kwa chama, uzalendo, historia na upendo alionao kwa nchi na chama kama vigezo na vipaumbele muhimu.

“Kwa ngazi zote toka matawi hadi Taifa tutayafanyia kazi maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Rais Samia. Tutakuwa makini kupitisha wagombea udiwani, uwakilishi na ubunge,” alisema Mbeto.

Mwenezi Mbeto alisema, ni lazima wakaaangalie mwenendo wa kila mwanachama kabla ya uteuzi na kujua kama mgombea huyo ana nidhamu, mtii wa siasa, sera na Itikadi ya chama anayeishi kimaadili na muaminifu.

“Tunampongeza sana Mwenyekiti wa chama Dkt. Samia kwa maelekezo yake kwetu. Tunakwenda kuyasimamia yote na kutenda haki bila kufanya kinyume chake,” alibainisha.

Alisema, kuteua au kupitisha wanachama mamluki, wasio na uzalendo kwa nchi na si wenye imani na sera, wamekuwa wakiwapa lawama na majuto.

“Wakati wa TANU tulipoteza Jimbo la Mbulu, Alipitishwa Chifu Amri Dodo akaachwa Padri Herman Serwat aliyeongoza kura za maoni. Karatu akaachwa Dkt. Wilbroad Slaa akateuliwa Patrick Qorro tukapoteza,” alieleza.

Mbeto alisema, hata Iringa Mjini Chama kilipitisha jina la Monica Mbega akaachwa Fredrick Mwakalebela aliyeongooza kura za maoni jimbo pia likaenda upinzani.

“Mwenyekiti ametukumbusha kwa nia njema tutende haki kwenye vikao vyote vya maamuzi.
Upendeleo, ubinafsi na rushwa uwe mwiko wa milele,” alisisitiza katibu huyo Mwenezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here