Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimewataka makada ndani ya chama hicho ambao majina yao hayatarudi kuwania Ubunge na Uwakilishi kutokuwa na kinyongo badala yake wawaunge mkono wenzao waliopitishwa kuwania nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu, ujao Oktoba mwaka huu 2025.
Majina ya waliopitishwa na CCM kuwania Ubunge na Uwakilishi yanatarajiwa kutangazwa rasmi Agosti 20, 2025.
Akizungumza katika kipindi cha Ana kwa Ana cha Zenjibari Televisheni, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, iwapo kuna ambaye jina lake halitarudi akubali matokeo kwani miaka mitano sio mingi.
Alisema, iwe ulikuwa mbunge au mwakilishi hata wewe jimbo ulilikuta, alikuwepo mtu akatoka ukakaa wewe.
“Sioni haja ya kuwa nongwa na mtu kuzunguka nchi nzima akiwasema vibaya vingozi kwani jimbo ulilikuta, utaliacha na kama ukitaka tena wakati ukifika utaomba tena ridhaa ya chama,” alisema mwenezi Mbeto.
Alisema kuwa, chama kimekuwa makini kuhakikisha kinampata mtu anayekubalika na jamii kwani kuna baadhi ya wabunge na wawakilishi badala ya kuwahudumia wananchi walikuwa wanawahudumia viongozi wa chama na walitengeneza mtandao hadi kwa mabalozi wa Mashina.
“Hapo ndipo ambapo unakuta kapita kwa kura nyingi lakini wananchi hawamtaki, chama kina vyombo vyake ambavyo vilikuwa vinasimamia mchakato mzima, hivyo haki itatendeka,” alisema.
Aliongeza kuwa, kuna malalamiko sehemu zingine, unakuta mbunge wa siku nyingi na pengine alikuwa waziri kazidiwa kura na kada wa kawaida halafu analalamika.
“Ukipita mtaani wananchi wanamlalamikia hiyo ni wazi kuwa hukubaliki” alisema Mbeto na kuongeza kuwa kuna ambao pesa za mfuko wa jimbo walikuwa wanatumia na mtandao wao kwa mambo yao binafsi.
Mwenezi huyo alibainisha kuwa kila mwaka kila jimbo linapata Tsh.Mil 30 kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lakini cha ajabu wanashindwa kutatua changamoto jimboni ya TSh.Mil.2.
Alisema Mbeto matokeo yake ni malalamiko kutoka kwa wananchi na chama hakitampitisha mtu wa namna hiyo ni lazima awe anakubalika kwa jamii.