Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwa mujibu wa Sheria hakuna chama chochote cha siasa, vyombo vya habari au taasisi yoyote yenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi bila idhini ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
Pia chama hicho kimesisitiza kuwa Uchaguzi katika nchi yoyote duniani, huongozwa kwa kanuni na taratibu za kisheria si kwa mtindo holela.
Msimamo huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, wakati akijibu hoja zilizotolewa na mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman.
Othman mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania Urais, amesikika akiikosoa sheria ya kura ya mapema akitishia na kutaka isitumike.
Mbeto akijibu hoja hiyo alisema, sheria hiyo haikutungwa aidha na malaika, majini au mashetani, bali imetungwa na binadamu waliopewa dhamana ya kutunga na kuzipitisha.
Alisema, sheria hiyo itaendelea kutumika Zanzibar hadi pale Baraza la Wawakilishi Zanzibar, litakapofanya mabadiliko mengine kwa utaratibu halali .
“Hakuna Sheria nzuri au mbaya ikiwa imeshatungwa pia imepitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Sheria ya kura ya mapema imeridhiwa na chombo hicho. Haikutungwa katika ofisi ya chama chochote cha siasa,” alisema Mbeto.
Katibu mwenezi huyo alisema, ni wazi ACT kupitia mgombea wake wa Urais, imebaini kushindwa kwa kuona maendeleo yalivyoshamiri huku wananchi wakisifu uongoozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
“Hayupo mwenye ubavu wa kuzuia watu wasipige kura ikiwa sheria inataka hivyo. Atakaewatisha, kuwazuia au kutaka kuwapiga wapiga kura wasifike vituoni watadhibitiwa na mkono wa sheria,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu Mwenezi huyo aliongeza kusema, ikiwa Othman ameshajua kuwa hawezi kushinda, si kosa kwake kutangaza amekubali kushindwa.
“Sheria anayoipinga imetungwa na wajumbe halali wa Baraza la Waawakilishi Zanzibar. Inawezaje kufutwa leo ikiwa chombo hicho kimevunjwa kisheria?” alihoji Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, anachokitaka Othman kuwashawishi vijana wa ACT ili walete ghasia na fujo.