Mbeto: Hakuna anayekataliwa kuandikishwa Zanzibar

0

Na Mwandishi Maalum, Pemba,

CHAMA Cha Mapinduzi kimesema kila mtanzania iwe amezaliwa Zanzibar, Mwanza, Mkokotoni, Mtwara, Mkanyageni au Katavi hawezi kupiga kura Zanzibar bila kutimiza vigezo vilivyotajwa kwa mujibu wa sheria

Aidha, kwa matakwa ya katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, mpiga kura kwanza awe mzanzibari aliyeishi jimboni miezi thelathini na sita ikiwa mzaliwa wa Tanzania Bara aishi Zanzibar miaka kumi pia awe mkaazi wa shehia husika kwa miezi thelethini na sita.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis, alipozumgumza na waandishi wa habari huko Chachani Wilaya ya Chake Chake Mkoa Kusini Pemba.

Mbeto alisema, haki ya kupiga kura haitokani na mtu kuwa na cheti cha kuzaliwa Zanzibar kuwa na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi au Kitambulisho cha uraia wa Mtanzania.

Alisema, mwananchi yeyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye kitambulisho cha Taifa cha uraia pia kwa mzaliwa wa Zanzibar, ana haki kuwa na ZAN ID na kwa mtanzania mwenye Kitambulisho cha TAN ID, hivyo bado si vigezo vya kuwa mpiga kura.

Alisema, baadhi ya watu kwa nia ovu hupotosha sheria na matakwa ya katiba ili kufikia matlaba yao kisiasa, kinyume na katiba na kudai kuna watu wanakataliwa kuandikishwa kwenye Daftari la Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) .

“Sheria inamtaja anayeruhusiwa kuandikishwa na kuwa Mpiga Kura ni mtu yoyote aliyezaliwa Zanzibar na kuwa Mkaazi wa miezi thelathini na sita jimboni. Kwa mzaliwa wa Tanzania Bara aishi miaka kumi Zanzibar na kuwa mkaazi wa eneo husika kwa miezi thelathini na sita.” alisema Mbeto.

Pia, Katibu huyo Mwenezi alisema kuna baadhi ya viongozi wa upinzani kwa makusudi, wamekuwa wakieneza propaganda hasi ili kupotosha ukweli, ionekane Zanzibar kuna watu wanakataliwa kuandikishwa.

“Kuna Vyama vimekuwa vikiidanganya dunia kila wakati wa uandikishaji. Sheria ya ukaazi ipo wazi ikimtaja mtu ambaye si Mkaazi na aliyekosa vigezo kisheria hataandikishwa na kuwa mpiga kura,” alieleza.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, Mbeto alielezea taratibu zitakazotumika katika mapokezi ya mgombea mteule wa urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya CCM, atakaewasili Pemba na kutambulishwa kwa wana CCM.

“Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi atawasili Pemba na kutambulishwa kwa wana CCM wenzake . Wakati wa kumtambuliisha mbele ya wananchi haujawadia. Anakuja ili kupongezwa na wana CCM kwa kuteuliwa,” alieleza Mwenezi huyo.

Vilevile, Mbeto amewatolea wito wana CCM katika Mikoa miwili ya Pemba, Kusini na Kaskazini, kujitokeza katika ofisi za CCM ili kumlaki mgombea huyo mteule wa urais mwaka 2025.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here