Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema sera zake tokea enzi za ASP na TANU, si za kibaguzi wa aina yoyote iwe ni kutokana na rangi, kabila, asili au na sababu za watu.
Vile vile, kimesisitiza kina wanachama wenye asili zote wakiwemo Wahindi, Waafrika, Waarabu, Wachina, Washirazi na Wangazija ambao kila mmoja ana haki sawa ndani ya CCM .
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akiwahimiza watendaji, wagombea au mwanachama, atakaetumia maneno ya kibaguzi, chama hakitamvumilia .
Mbeto alisema, chama cha ASP visiwani Zanzibar hakikuungwa mkono na Waafrika peke yao bali makundi yote ya kijamii bila kujali asili na rangi zao, walikipigia kura kuanzia uchaguzi wa mwanzo mwaka 1957 hadi sasa.
Alisema, Mwanachama yeyote akiwa Baniani, Kumbaru, Mwarabu anayetokea Oman au Yemen, Mshiraz wa Iran au Muafrika toka Tanganyika, Kenya, Malawi, Uganda, Zanzibar au Comoro wote ni wana CCM.
“Hatuwezi kwenda kinyume na sera zetu za msingi. Moja kati ya imani yetu ni kuamini kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja. Ndio maana CCM kina viongozi, Wawakilishi, Wabunge na wanachama wa rangi na kabila zote,” alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa, mwanachama atakaebainika anatumia lugha ya ukabila, rangi na kufanya upendeleo katika uchaguzi wa chama, ataadhibiwa kwa mujibu wa katiba ya CCM, kinidhamu na kimaadili.
“Vyama vyenye sera za Ubaguzi wa rangi, asili na nasaba vinafahamika na viongozi wake hujifaharisha kwa kutoa matamshi ya ubaguzi.
“Siasa hizo ndani ya CCM hazina nafasi,” alieleza
Katibu huyo mwenezi na kuongeza kuwa vyama vyenye sera za ukanda, udini na ukabila, haviwezi kuungwa mkono na watanzania wenyewe huku vyama hivyo vikikaribia kufa baada ya Watanzania kuvishtukia.
Mbeto amezielekeza Kamati zote za uchaguzi kuanzia ngazi za Matawi, Wadi, Majimbo, Wilaya hadi Mikoa, zitimize wajibu wa kikatiba na kikanuni kwa kusimamia haki na maadili.
“CCM kimeziandikia taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya rushwa ikiziomba zifuatilie chaguzi zake zote. Mwanachama, mgombea au kiongozi atakayekamatwa akitoa au kupokea rushwa atafikishwa mahakamani,” alisema Mbeto.