Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya watendaji, makada na viongozi wa chama wanaojiona si wahusika dhidi ya shutuma zisizo na msingi wanazotupiwa viongozi wakuu wa chama na serikali.
Aidha, CCM kimewataka viongozi wenye dhamana ndani ya chama na jumuiya zake kujibu kwa wakati hoja zinazoelekezwa kwa chama na kutoa ufafanuzi wa kisera na kimsimamo badala ya kukaa kimya kama vile haziwahusu.
Ushauri huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis aliyewataka viongozi wenye dhamana za kisiasa, kujua kuwa siasa ni uwanja wa ushindani wa hoja kwa nguvu ya hoja.
Mbeto alisema, viongozi wakuu wa chama akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan au Makamu wake Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakitupiwa shutuma ni kazi ya viongozi wahusika kuzijibu na kuzitolea ufafanuzi bila kuchelewa kwani uongo ukiachwa bila kujibiwa zinawakanganya wananchi na kuwaacha njiapanda.
Alisema, licha ya kwamba dhamana ya kujibu na kufafanua masuala anuai ya kisiasa kuwa chini ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo pia kuna viongozi wa wilaya, mikoa na jumuiya za chama ambao pia wanawajibu katika jambo hilo.
“CCM ina jumuia tatu kabambe ambazo ni UWT (Umoja wa Wanawake) UVCCM (Umoja wa Vijana) na Wazazi (Umoja wa Wazazi), wapo pia viongozi wa mikoa na wilaya hadi wajumbe wa Nec na MCC.Tusikubali viongozi washambuliwe na sisi tukae kimya,” alisema Komredi Mbeto.
Pia, Katibu huyo Mwenezi alifafanua kuwa kazi ya ufanyaji wa siasa katika zama za sasa zenye kuambatana na mitandao ya kijamii imebadilika, siasa za leo kwa kiasi kikubwa zimehamia kwenye majukwaa ya mitandao.
“Tujue zama zimebadilika, tumehama kutoka kwenye mfumo wa Anolojia, tunaishi katika Dijitali, wepesi wa kupata na kueneza taarifa umekuwa wa haraka mno. Tukishambuliwa bila kujibu itakula kwetu,” alieleza.
Mbeto aliwahimiza makada, viongozi na watendaji wenye dhamana wa chama katika kujibu hoja zao, lazima wajielekeze katika kujenga nguvu ya hoja , kuongozwa na sera chini ya miongozo ya chama.
“Haiwezekani mwenyekiti wa CCM au makamu wake wanashambuliwe na wapinzani wetu lakini wanaCCM wanashindwa kutetea au kujibu hoja. Uhai wa chama lazima uambatane na utoaji wa majibu dhidi ya upotoshaji wowote,” alisema Komredi Mbeto.