WAZIRI Mkuu wa Namibia, Dkt. Tjitunga Elijah Ngurare, amewataka wanasayansi wa Afrika kuchunguza maarifa ya asili na kujiuliza kama yanaweza kutoa mwanga wa kubuni teknolojia zitakazotengenezwa barani humo.
Akifungua Jukwaa la Washirika wa Mpango wa Kuimarisha Taasisi za Ufadhili wa Utafiti Afrika (SGCI) mjini Windhoek, Septemba 30, 2026, Dkt. Ngurare alirejea simulizi za Kiafrika kuhusu kusafiri usiku na kuwasiliana kutoka maeneo yaliyo mbali.
Alisema, baadhi ya watu wanaweza kuyapuuza mawazo hayo au kumwona anayeyaibua kuwa hajastaarabika, lakini aliwataka wanasayansi kuwa tayari kuuliza maswali na kufanya uchunguzi.
“Ikiwa nimekosea, mababu zetu watanısamehe,” alisema, akitoa mfano wa mawasiliano ya jadi na kuhoji ni maarifa gani yanaweza kuchunguzwa kwa kutumia sayansi ya sasa.
Dkt.Ngurare hakusema kuwa simulizi hizo zimethibitishwa kisayansi kuwa teknolojia za mawasiliano.
Alizitumia kuwahamasisha watafiti kufikiria zaidi ya yaliyozoeleka na kuchunguza mawazo ambayo huenda yakapuuzwa kabla ya kufanyiwa utafiti.
Kisha akaelekeza hoja yake kwenye bidhaa na mifumo ya teknolojia inayotumiwa Afrika. Alihoji kwa nini sehemu kubwa ya programu na vifaa vya kompyuta hutengenezwa nje ya bara hilo, licha ya Afrika kuwa na wanasayansi na vijana wenye uwezo wa kubuni.
“Samsung ya Afrika itakuja lini? Apple ya Afrika itakuja lini?” aliuliza.
Waziri Mkuu huyo alizitaka serikali kusikiliza watafiti wa Afrika, kutumia utaalamu wao na kuwapa vijana nafasi ya kukuza mawazo mapya.
Alisema utafiti unapaswa kutoa majibu kwa changamoto za chakula, afya, nishati, maji, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia za kidijitali.
Tanzania iliwakilishwa katika ufunguzi huo na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, aliyetoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa SGCI.
Dkt. Nungu alisema, taasisi zinazofadhili utafiti zinatambua wajibu wao wa kusaidia tafiti zinazojibu mahitaji ya jamii.
Alisisitiza kuimarisha taasisi na ushirikiano ili maarifa yanayozalishwa yachangie sera bora, suluhisho zinazotumika na maisha bora kwa wananchi.
Ushirikiano wa utafiti barani Afrika tayari una mfano nchini Tanzania. Kupitia mpango wa O.R. Tambo Africa Research Chairs, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kina kiti cha utafiti wa milipuko ya magonjwa ya virusi kinachoongozwa na Prof Gerald Misinzo.
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) nayo ina kiti cha utafiti wa sayansi na teknolojia ya kiwango cha nano. COSTECH ni mshirika wa utekelezaji wa mpango huo nchini.
Jukwaa la Windhoek linawakutanisha viongozi wa taasisi za ufadhili wa utafiti, watafiti na washirika wa maendeleo wakati SGCI ikiingia awamu yake ya tatu.
Kaulimbiu yake, From Commitment to Action, inazitaka taasisi hizo kugeuza makubaliano ya ushirikiano kuwa kazi yenye matokeo kwa wananchi.