Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis ameshangazwa na uwezo kitaaluma wa mwanasheria wa ACT – Wazalendo kufuatia kauli yake kuwa atawashtaki mahakamani wakuu wa wilaya na mikoa.
Mbeto alisema, hajui mwanasheria huyo amesomea wapi fani yake hiyo, kwani kisheria wakuu wa wilaya na mikoa ndio wenyekiti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao na hawawezi kushtakiwa kwa kutekeleza majukumu yao.
Alisema, kisheria kwa mujibu wa katiba, wana mamlaka ya kuchukua hatua pale wanapoona kuna dalili ya uvunjifu wa amani kama alivyofanya Mkuu wa Wilaya ya Kati, Sadifa Juma Khamis.
Alisema, Sadifa alitekeleza majukumu yake kisheria kama mkuu wa wilaya na sio mtu binafsi kama ingekuwa hivyo basi angeenda polisi na kuchukua RB lakini haikuwa hivyo.
“Hakumfunga wala kumpiga mtu, mkuu wa wilaya, katoa maelekezo wakamatwe wakahifadhiwe baadae wakaachiwa, nadhani wenzetu hao hiyo ni hali ya kuchanganyikiwa,” alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa, wanachanganyikiwa kwa kuwa wanaona zoezi linaenda vizuri na suala la uandikishaji si la chama chochote cha siasa na anashangaa wanapodai kuwa watu wao hawaandikishwi.
“Zoezi ni la wananchi wenyewe wametangaziwa kila aliyefikisha umri wa miaka 18 akajiandikishe na wengine kwenda kurekebisha taarifa zao,” alisema.
Mbeto alisema, hakuna anayeenda kujiandikisha amevaa sare za chama cha siasa; hajui wao ACT Wazalendo wamewatambua vipi wanachama wao ambao wanadai hawakuandikishwa.
Alisema, kujiandikisha ni suala la wananchi kwa kuwa ni zoezi la kikatiba, hivyo kila mmoja ni vema afuate utaratibu na kuheshimu sheria zilizopo na kinachofanywa na chama hicho cha upinzani ni kutaka kusababisha fujo.
Mwenezi huyo alibainisha kuwa lazima kila mmoja atambue kuwa kuna maisha baada ya uandikishwaji katika daftari la wapiga kura na pia baada ya Uchaguzi Mkuu.
“Maoni yangu katika hilo ni kuwa Mkuu wa wilaya anatekeleza majukumu yake ya kisheria katika eneo lake la utawala ambalo amekasimiwa kikatiba,” alisema.
Alibainisha kuwa, mkuu wa wilaya ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya husika hivyo ni lazima asimamie usalama katika eneo lake.
Alibainisha Mbeto kuwa viongozi waliopo kwa mujibu wa katiba, wakitekeleza majukumu yao hawawezi kushtakiwa kama watu binafsi.
“Kiongozi ambaye anatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria unamshtaki vipi? Nadhani ni kuchanganyikiwa kwa wenzetu,” alisema.
Mbeto alibainisha kuwa ni vema wakaendelea kuwaelimisha wenzao (ACT Wazalendo) kuwa nchi ni yetu sote na amani ya nchi muhimu kuliko vyama vyetu au jambo lolote.
ACT Wazalendo jana ilitoa taarifa ya kutishia kuwashtaki wakuu wa wilaya na mikoa kwa kile wanachodai kutumia madaraka yao vibaya katika zoezi la uandikshaji katika daftari la wapiga kura visiwani humo.
Taarifa ya ACT Wazalendo kwa wanahabari jana, ilieleza kuwa chama hicho kitawashtaki wakuu wa wilaya na mikoa wanaotumia madaraka yao vibaya katika zoezi hili la uandikishaji.
Chama hicho kilidai watawashtaki kama watu binafsi na sio vyeo vyao na wanaamini wataipata haki yao ndani ya Mahakama Kuu Zanzibar au ya Rufaa ili hata kama wakiondolewa kwenye nafasi zao kesi zitaendelea kuwepo.
Aidha, walidai wanachama wa chama hicho walikuwa wakikataliwa kuandikishwa au kurekebisha taarifa zao katika daftari la wapiga kura.
Tamko hilo la ACT Wazalendo lilitolewa kufuatia hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kati, Sadifa Juma Khamis, kuwakamata na kuwaweka mahabusu vijana waliokuwa katika vikundi nje ya kituo kimojawapo cha kujiandikisha katika daftari la wapigakura, Mkoa wa Mjini.
Kulingana na Sheria namba 4 ya mwaka 2018 ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar mtu asiyehusika anatakiwa akae Mita 200 kutoka kituo cha uandikishaji.
Wanaotakiwa kuwepo ni maofisa wasaidizi wa tume ya uchaguzi Sheha wa Sheia husika, mawakala wa vyama husika, polisi na waangalizi wenye vitambulisho maalum.
Pia, kumekuwa na matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa ACT Wazalendo kuwazuia njiani wananchi ambao wanaenda katika vituo vya kujiandikisha na wengine kutishiwa.