KAMISHNA wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi amesema, wamepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa majukumu yao baada ya kuanza kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Jaji Mwangesi alisema hayo wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, kwenye Kikao Kazi kilichofanyika leo, Mei 30, 2025, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuelezea mafanikio ya Taasisi hiyo.

Alisema, kwasasa kupitia mifumo hiyo ya kisasa, wanapokea kwa urahisi matamko kuhusu mali na madeni ya watumishi wa umma, jambo ambalo limewasaidia kurahisisha utendaji kazi na kuwapunguzia usumbufu na gharama wadau wao.
“Matumizi ya mfumo huu ni hatua kubwa ya maboresho ya utendaji wetu na kuwajali wadau na kuwapunguzia adha na gharama ya kufika kwenye vituo vyetu,” alisema.
Aliendelea kusema, “Mfumo huu umeanzishwa ili kutekeleza sera ya Serikali mtandao, ambapo Serikali imeagiza taasisi zote za umma kutumia mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na kuboresha utendaji.”

Alisema, mwitikio wa wadau katika matumizi ya mfumo huo ni mazuri kwa asilimia 90% na wengi suala la matumizi ya mtandao huo haliwasumbui ni tofauti ya matarajio yao wakati wanaingia kwenye mfumo huo.
“Kwa nafasi hii, nawapongeza watumishi wote wa umma kwa kutupa ushirikiano, pia navishukuru vyombo vya habari kwa kuutangaza mfumo huu,” alisema Jaji Mwangesi.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili Fabian Pokela, akizungumzia umuhimu wa mfumo huo wa TEHAMA alisema, unasaidia kulinda uadilifu, huku akisisitiza kwamba, wanaendelea kuuboresha ili ufanye kazi kwa ufanisi zaidi.
