
Asasi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA Tanzania) imetoa wito kwa jamii kuendelea kuungana ili katika kupaza sauti kuhusu hali ya usalama barabarani nchini ili kupunguza idadi ya vifo na majeruhi watokanao na ajali za barabarani zinazohusisha kugongwa kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli katika maeneo mbalimbali nchini
Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa RSA Tanzania, Augustus Fungo, alipokuwa akiongea wakati wa kuhitimisha matembezi ya kilele cha Maadhimisho ya Nane ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam na kufadhiliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini (WCF)
Akiongea na watembea kwa miguu na waendesha baiskeli walioshiriki matembezi hayo, balozi Fungo amesema kumekuwa na muamko mkubwa kwa watu kufanya matembezi na kuendesha baiskeli kama sehemu ya mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa kiafya kama inavyoshauriwa, lakini ajali za barabarani zimekuwa kikwazo kikubwa kwa baadhi yao.
“Ajali za za watembea kwa miguu, wafanya mazoezi na waendesha baiskeli ni tatizo kubwa sana kwa kundi hili ambalo limeitikia wito wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuepukana na maradhi yasiyo ya kuambukizwa, hivyo tunapaswa kuendelea kupaza sauti ili mamlaka zinazohusika na usanifu na ujenzi wa barabara, kuzingatia miundombinu itakayowezesja kundi hili la watumia barabara kuwa salama” amesema balozi Fungo

Akiongea baada ya kushiriki matembezi hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Tafiti kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dkt. Abdulssalaam Omar, amesema ajali za barabarani ni janga kubwa kwa taifa na zinapaswa kupaziwa sauti ili kupunguza madhara yake na kustawisha nguvukazi ya nchi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
“Karibu asilimia 55 ya wanufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini (WCF) wafanyakazi waliopoteza maisha au kupata ulemavu kutokana na ajali za barabarani, sasa ukiangalia takwimu hizi zinazoashiria kuwa ajali hizo ni janga lenye kugharimu nguvu kazi ya taifa na hii inapaswa kuwa sababu ya sisi sote kuendelea kuungana katika kupaza sauti ili kuimarisha usalama barabarani na kunusuru maisha ya raia wenzetu na nguvukazi muhimu kwa uchumi wa nchi” almesema Dkt. Omar.
Maadhimisho ya mwaka huu ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani, yalibeba ujumbe wa “Tuwalinde na kuwafanya waendesha baiskeli na watembea kwa miguu wawe salama barabarani” ambapo akiongea katika tukio hilo, muwakilisho kutoka taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), amesema kuwa ajali za barabarani ni janga ambalo limekuwa likisababisha kuzorota kwa huduma za afya nchini kwani idadi kubwa ya majeruhi wa ajali ambao wamekuwa wakipelekwa kwenye hospitali, imekuwa inazidi hata wagonjwa wengine na hivyo kufanya utoaji huduma kuwa changamoto hususan kwenye upatikanaji wa damu salama.

Matembezi hayo yaliandaliwa na RSA Tanzania na huku yakipewa sapoti na WCF pamoja na shirika la Kimataifa la Muungano wa Asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na usalama barabarani Duniani (Global Alliance of NGOs for Road Safety) na yameshirikisha watembea kwa miguu wakiwemo wafanya mazoezi (joggers), waendesha baiskeli huku pia yakihudhurwa na wawakilisho kutoka WCF, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), asasi ya TANCDA inayojihusisha na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) na umoja wa waendesha pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam.
Akiongea wakati wa hafla ya kuhitimisha matembezi hayo iliyofanyika eneo la ufukwe wa Coco, msemaji wa Shirikisho la Waendesha Pikipiki Dar es Salaam, balozi Tito Lazaro, ametoa wito kwa mamlaka za afya nchini kuangalia upya mfumo wa matibabu kwa waendesha pikipiki wanaopata ajali akisema kuwa mfumo wa sasa umekuwa ukiwashawishi kwenda kwa wataalamu wa tiba asililia zaidi kuliko kwenda hospitalini
Amesema kuwa gharama za matibabu kuwa kubwa pamoja na muda wa matibabu kuwa mrefu sana ni sababu zinawafanya bodaboda wengi wakimbilie kwa sangoma badala ya hospitali hivyo kuomba mfumo wa matibabu kwa majeruhi wa pikipiki kuangaliwa upya
“Hospitalini gharama ni kubwa na muda wa kupona pia ni mkubwa, mtu anakaa na POP kwa miezi sita na zaidi, wakati kwa sangoma mtu anapona miezi minne na kwa gharama nafuu na hana tatizo lolote akitoka, sasa hii inafanya wengi tusiende hospitali: amesema balozi Lazaro





