WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea Muundo unaopendekezwa wa Shirika la Uzalishaji Mali wa Jeshi la Polisi kutoka kwa timu ya Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiongozwa na Prof. John Kafuku.
Shirika hilo la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi lilianzishwa Machi, 29, 2013 kupitia Agizo la Rais namba 66 la kuboresha miundombinu na kujenga uwezo wa kiuchumi wa Jeshi la Polisi baada ya Serikali kupitisha Mkakati wa Maboresho wa Jeshi la Polisi wa miaka mitano unaolenga kujenga usasa, ushirikiano wa jamii na utaalamu.
Akizungumza wakati wa wasilisho hilo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alisema, adhma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuona vyombo vya ulinzi na Usalama vikibakia katika majukumu yake ya msingi ambayo ni ulinzi wa raia na mali zao, huku Mashirika ya uzalishaji mali yaliyopo katika vyombo hivyo yakiachwa yafanywe shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, uzalishaji wa fenicha, ushonaji wa nguo na utengenezaji wa viatu.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalikua wazi na yalilenga kuyafanya majeshi yetu yawe na Mashirika ambayo yako katika ushindani katika sekta husika ikiwa ya kilimo au viwanda na akataka mapato yanayotokana na Mashirika hayo yatumike kuimarisha vyombo hivyo vya ulinzi na usalama,” alisema Waziri Masauni.
Pia, aliwapongeza wataalamu hao kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wasilisho la muundo pendekezi, huku akiwaomba kujumuisha na maoni yaliyotolewa na wajumbe wa kikao hicho kuhakikisha wanarejesha muundo huo wa mwisho ili Shirika liweze kuingia kwenye utendaji wa miradi mbalimbali iliyopo mbele yake ikiwemo mradi wa miji salama.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ally Senga Gugu, Naibu Katibu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi, Kaimu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna wa Polisi, Liberati Sabas na Wakurugenzi wa Idara zilizopo chini ya Wizara hiyo.