Na William Kapawaga
KLABU ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC) na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, wameunda Kamati ndogo kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia ulinzi na usalama wa waandishi wanapokuwa kazini.
Kamati hiyo yenye Wajumbe sita imeundwa Machi 22, jijini Dar es Salaam kwenye Mdahalo wa majumuisho ya DCPC na Jeshi la Polisi.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), John Malulu ambaye pia ni RPC wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Askofu Emaus Mwamakula na Sheikh wa Wilaya ya Ilala Adam Mwinyipingu.
Wengine ni Wakili Mkumbo Emmanuel, Katibu Mkuu wa DCPC Fatma Jalala na Bakari Kimwanga ambaye ni mwanachama DCPC.
Kuundwa kwa Kamati hiyo ni matokeo ya midahalo mitatu kati ya DCPC na Jeshi la Polisi kuhusu Ulinzi na Usalama kwa waandishi wa habari, pamoja na kusimamia haki na sheria.
Midahalo hiyo iliyoanza Novemba 2023 na kumalizika Februari 2024 iliratibiwa na Muungano wa Klabu za waandishi wa Habari (UTPC) na kudhaminiwa na Shirika la IMS, ilihusisha Kanda Maalum Ilala, Temeke na Kinondoni, ambapo maazimio ya kiutendaji yalifikiwa.