Na Leena Lulandala
TANZANIA ni miongoni mwa nchi chache Duniani zenye vivutio vingi vya kitalii na vizuri mfano Mlima mrefu zaidi wa Volkano barani Afrika ni Mlima Kilimanjaro, hifadhi za taifa zenye wanyama pori pamoja na maeneo muhimu kwa uhifadhi wa ndege.
Nyingine ni hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ruaha na Ziwa Manyara, Milima ya Tao la Afrika Mashariki lenye utajiri mkubwa wa bioanuwai ikiwa ni pamoja na milima ya Uluguru na Usambara.
Sanjari pasipokusahau Pwani ya bahari ya Hindi yenye mandhari na upepo mzuri. Hivyo, imekuwa ikipokea mamia ya watalii kutoka nchi mbalimbali duniani pia na wenyeji ambao idadi yetu imekuwa ikiongezeka kila kukicha.
Makala hii imelenga kukusaidia Mtanzania mtalii wa ndani kukupata ufahamu ni vitu gani muhimu ukiwa navyo au ukivifanya vitakusaidia kufurahia na kuwa na safari nzuri ya Kitalii.
Mosi, ni Taarifa ya eneo husika; kutokana na maumbo tofauti ya uso wa duniani katika nchi yetu pamoja na uoto wake hufanya maeneo haya kuwa na hali ya hewa tofauti vile vile kama mvua wakati sehemu nyingine kunakuwa na baridi kali inayoambatana na upepo.
Katika kutambua hilo, itakusaidia katika uandaaji wa nguo zipi zitafaa kama sehemu ya baridi kuwa na nguo nzito kama sweta. Pia, wakati wa utafutaji wa taarifa ni vyema kujua miundo mbinu iliyopo kama vile hoteli zilizopo na gharama zake ili kujua kama zinaendana na bajeti yako.
Aidha, ni vema ukajua muundo wa barabara na ubora wake kama ni lami au kama ni sehemu ya kupanda mlima kujua njia ya kupandia zilivyo ili kujitathimini kama utaziweza.
Pili, ni uchambuzi wa mavazi (nguo na viatu); kujua taarifa ya eneo husika husaidia uchaguzi wa mavazi kuwa rahisi ukishajua hali ya hewa, umbo la sura ya nchi ya eneo hilo pamoja na shughuli za kutalii zinazofanyika vitakusaidia wewe kufanya uchaguzi mzuri wa nguo na viatu hasa katika urefu, rangi na aina ya nguo.
Kama umeshatambua sehemu hiyo wanafanya shughuli za upandaji wa mlima itakufanya wewe kuchagua raba zitakazokuwezesha kupanda mlima kwa urahisi, kuandaa nguo zenye nafasi kubwa kidogo kama vile tishirt pamoja na suruali zenye kitambaa kilaini kidogo ili kukuwezesha kupata mzunguko mzuri wa hewa na kuufanya mwili ustareheke.
Pia, sehemu za Pwani nyingi zina asili ya joto, hivyo ni vyema zaidi kuwa na viatu vya wazi ‘sendozi,’ pamoja na nguo nyepesi vile vile ili viweze kukusaidia kupata upepo mzuri na kufurahi zaidi.
Mara nyingi inashuriwa zaidi kutovaa nguo zenye rangi ambazo zinang’aa, kwani hufanya uonekane hata ukiwa mbali zaidi kama vile nyekundu, njano, nyeupe, pinki, rangi ya chungwa yenye kukolea.
Tatu, ni vizuri kuwa na vifaa wezeshi kama vile kamera, kofia, miwani, tochi na kiona mbali; kifaa kama kamera na kiona mbali kidogo ni gharama katika ununuzi na sio lazima sana kuwa navyo ila inashauriwa. Utunzaji wa kumbukumbu kwa njia ya picha kupitia kamera huwezesha kupata picha nzuri na zenye ubora japokuwa mtu unaweza tumia kamera ya simu yako.
Kionambali hukuwezesha kuvuta vitu vya mbali na kuviona kwa ukaribu hasa wanyama wakaao mitini pamoja na ndege. Miwani na kofia vitakusaidia kuzuia vumbi, jua na wadudu kuingia machoni na kichwani. Tochi ni vema kuwa nayo hasa wakati wa usiku pia mchana hasa kwenye maeneo yenye mapango au kwenye misitu minene.
Nne, ni Vifaa vichache muhimu vya huduma ya kwanza; ni vema zaidi kuandaa vifaa vyako vichache vya huduma ya kwanza hii itakusaidia hata ikitokea chochote unaweza jipa mwenyewe huduma kuliko kusubiri kutoka kwa mwenyeji wako au zahanati na wakati kina kukuta kitu unaweza ukawa mbali napo.
Vifaa hivyo ni pamoja na wembe, kitambaa kidogo au kanga/mtandio kwa wanawake, Pedi, dawa chache za kutuliza maumivu, dawa za kujipulizia kuzuia wadudu warukao kama mbung’o pia kama inawezekana kuwa na dawa za kupunguza hewa tumboni.
Tano, Vitambulisho; ni vyema zaidi kusafiri na vitambulisho (Cha utaifa, bima ya afya kama unayo, cha kupigia kura pamoja na namba za mawasiliano za watu wa karibu) vyako kila mahali unapokuwa hasa ukiwa katika maeneo ya utalii.
Unaweza kuacha sehemu ya kulala au ukatembea navyo hata unavofanya safari hii itakusaidia kutambulika kwa uharaka zaidi na kama itatokea shida yoyote utasaidika kwa uharaka mfano umeumia unahitaji kutibiwa bima ya afya itakusaidia.
Wakati mwingine sio watu wote hutoa taarifa za kiafya hasa yale magonjwa ambayo mtu anayo yanayohitaji uangalizi wa karibu kama wenye shinikizo la damu, pumu, nk kuna dawa zenye hutuliza pale shida inapojitokeza lakini wengine huwa na dawa ambazo miili yao huendana nazo hivyo, kujua hivyo mara nyingi ni kupitia watu wa karibu.
Sita, ni Uchambuzi wa chakula na vinywaji; ukiwa safarini ni vyema zaidi kuchagua chakula ambacho unajua hakina shida na mwili wako kwa wale ambao baadhi ya vyakula huwakataa hivyo huwafanya kutapika au kuharisha na kufanya safari isiwe nzuri.
Kwa wale watumiaji wa pombe ni vema zaidi ukatumia pombe kwa kiasi ili kukuwezesha kujitambua hata kama kitu kinatokea unakuwa na ufahamu ni kipi ufanye au ujisaidie kabla wengine hawajafika. Kwa wapanda milima ni vema zaidi ukawa na maji yako hii itakusaidia kupoza mwili na kulainisha Koo.
Saba, ni Daftari, penseli/peni, kitabu chochote cha kujisomea, simu, kompyuta pamoja na chaja zake. Sio kumbukumbu zote huchukuliwa na kamera, nyingine ni lazima kuziandika kwa urahisi wa utunzaji wako kwa sababu sio rahisi kukumbuka vitu vyote.
Kama ni mpenzi wa kusoma ni vyema kutembea na kitabu chako kwenye simu/kompyuta au kwa nakala ngumu hii itakusaidia wakati unasubiri maelekezo au unasubiri usafiri au unapumzika kuwa na kitu cha kufanya na kujiongezea maarifa. Pia, kuangalia filamu kwenye kompyuta au kufanya kazi zile za muhimu.
Nane, ni kuiandaa akili kisafari; hapa ni vema zaidi kutambua unaenda eneo lipi, kufanya shughuli ipi ya kitalii kwa muda gani na ukiwa na lengo gani. Utambuzi wa eneo unaloenda hukupa urahisi wa kupanga malengo ya safari, kwa wapenda ndege hukufanya upange aina ngapi za ndege unataka kuziona, wanyama gani unataka kuwaona au shughuli gani unataka kuzifanya.
Kama unakuwa umeziandika kwenye daftari yako ni rahisi kufatilia na kuona kama malengo yako yametimia. Katika kuandaa akili kisafari hii huambatanisha na kupata utulivu wa akili kwa muda na kupokea vitu vipya, kufahamiana na watu wapya na kusoma tamaduni za watu. Maana yake katika kusafiri unapata muda mzuri wa kutafakari na kupanga malengo mapya ya maisha.
Tisa, kuwa na pesa za ziada; ni vizuri zaidi wakati unaandaa na kupanga bajeti ya safari yako ni vyema kuwa na pesa za ziada ambayo unaweza ukatumia kufanya malipo kama sehemu imekuvutia na umetamani uendelee kukaa kwa siku kadhaa, pia kwa ajili ya kutoa shukrani kwa waliokuhudumia. Kuwa na pesa ya ziada hukusaidia kustareheka kiakili.
Naamini umejifunza na kutambua vitu gani vya kujiandaa ili kuiwezesha safari yako iwe yenye uzuri na kukufanya ufurahie zaidi.
0755 369 684.