Na Dkt. Raymond Mgeni
TAFITI zilizoainishwa na Statista 2021, Shirika la Kijerumani la hifadhi data za mwenendo wa matumizi data na masoko mtandaoni kwa takribani nchi 170 Duniani zinaonyesha kuwa, kuna watumiaji Bilioni 4.66 wanaotumia mtandao.
Kwa takwimu hizo, watu hao wana nafasi kubwa ya kushiriki pia katika mitandao ya kijamii. Hii ikiwa ina maana asilimia 59.5% ya idadi ya watu duniani wanatumia mitandao.
Inaelezwa, China, India na Marekani ndizo nchi zinaongoza kwa watumizi wengi wa mtandao au intaneti. Nchini China watu zaidi ya Milioni 854 ni watumiaji mitandao na India inachukua idadi ya watu zaidi ya 560 Milioni wanaotumia mtandao. Hii inaonesha namna isivyo rahisi kukimbia mabadiliko ya kimtandao yalivyokuja kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Unapogusia mitandao ya kijamii ni jumuisho la mitandao kama ‘facebook,’ ‘Instagram,’ ‘telegram,’ ‘We chat,’ ‘twitter’ na ‘Whatsapp’ ambapo imekutanisha watu na kuwafanya wapate taarifa, waweze kusambaza taarifa na picha toka mtu na mtu, mtu na kundi.
Urahisi wa mitandao ya kijamii kutumiana taarifa na ujumbe imekuwa haraka zaidi tofauti na wakati ambao hapakuwa na mitandao ya kijamii na simu za wakati huo kuwa katika mifumo ya kizamani.
Simu janja imekuwa sehemu kubwa ya maisha ya watu ilokuja kuyabadilisha maisha ya karne ya 21 ambapo imechangia pia uraibu wa mitandao ya kijamii kuwa mkubwa ambapo mtu akituma kitu basi anangoja namna wengine watakavyokipa mapendekezo au mwitikio “likes”.
Hivyo, imezalisha tatizo jingine la mtu kurudi rudi mtandaoni kuangalia kama alichotuma kimeonwa na watu wangapi na watu wamekipa maoni gani?
Saikolojia ya kuwavutia watu kuirudia mitandao ya kijamii ni sayansi ya kemikali iitwayo ‘dopamini’ ambayo ni kemikali furaha au zawadi inayompa mtu kujisikia vizuri anapofanya kitu na kujisikia vizuri kunamfanya aitafute hiyo hali tena na tena. Hivyo, kemikali hii inatoka zaidi pale mtu anapojisikia vizuri na hivyo inamuhamasisha kukirudia kitu.
Hivi ndivyo mitandao ya kijamii ilivyofanywa katika kuwanasa watu watume picha, wasambaze kitu na wangoje watu watoe mwitikio ‘likes’. Hili humfanya mtu aendelee kuhamasika kutuma picha iwe ni Instagram au ukuta wa Whatsapp ‘Whatsapp Status’ na kuona watu wangapi wataona.
Kadri watu wanavyotoa mwitikio ndivyo mtu anahamasika zaidi na zaidi kuwa mteja wa mtandao na kujenga matarajio ya wasomaji au wafuasi wa kile anachokituma.
Mitandao ya kijamii imeibua mtindo wa maisha wa watu kutuma upande mzuri tu wa maisha yao kwa kushirikisha picha mbalimbali za matukio au maisha wanavyoishi bila kujua wanachoshirikisha ni sehemu ndogo ya nyuma ya pazia ya maisha halisia.
Ukipita katika mitandao ya kijamii utaona matukio mbalimbali yanatumwa na watu yenye kuonesha maisha yao yanaendelea vizuri.
Watu wengine huingia gharama kuigiza maisha ili mtandaoni mtu aonekane ni wa hadhi fulani au wa maisha fulani kumbe kiuhalisia hayupo hivyo. Wanaoumia ni wale wafuasi wa watu wenye ushawishi fulani kufanya mambo kwa kuiga wasijue kinachooneshwa ni sehemu ndogo ya maisha ya mtu.
Ongezeko la watu kujisikia vibaya au huzuni limekuwa kubwa wanapoona wengine wanashirikisha matukio au picha mambo yanawaendea vizuri huku kwao wanapitia maisha magumu na changamoto nyingi.
Tafiti zinaonesha pia namna mitandao ya kijamii imeongeza watu wanaogua tatizo la sonona linalotokana na msongo wa mawazo wa kujilinganisha maisha kwa kufuatilia maisha ya watu wengine wanayoyashirikisha.
Wengi wanaingia katika kujihisi wao hawana maana ya maisha. Kujikatia tamaa na wengine kujihatarisha maisha yao sababu ya athari za kufuatilia maisha ya watu wengi wanaotuma wamefanikiwa na wana utajiri.
Hutaona mtu anatuma uhalisia wa maisha yake au mchakato wa jambo husika bali matokeo tu ya kitu. Uhalisia unafichwa usionwe na wafuatiliaji
Mbali na kutajwa kuwa mitandao inaficha uhalisia wa maisha ya watu bado ni fursa yenye manufaa makubwa kwa zama tuishizo sasa. Watu wanatumia mitandao ya kijamii kibiashara katika kutangaza biashara na kutafuta wateja, kukuza mtandao wa watu, kutafuta kazi na ajira, kusambaza habari na kusambaza maudhui ya kielimu na maarifa.
Pia, mitandao ya kijamii na mifumo ya interneti imefungua fursa za uchumi wa kidijitali kukua zaidi maana malipo mengi au mihamala mingi inafanyika kwa njia ya mtandaoni.
Mwisho ni muhimu sana kuwa makini na kuchuja taarifa na habari ambazo husambazwa mitandaoni kwa kujihakikishia uhakika wa chanzo cha habari, maudhui ya habari na umuhimu wa kuisambaza kwa wengine.
Kumekuwako na habari na taarifa nyingi zisizo kweli au za kiupoteshaji mtandaoni husambazwa na watu na wale wasojua ukweli wa habari wanaweza kuingia katika mitego ya kusambaza kitu kisicho kweli au kutapeliwa kabisa ikiwa taarifa zilizosambazwa zinagusia fursa za biashara zisizo kweli ila zenye dhima ya kutapeli watu.
Hatuwezi epuka ulimwengu wa mitandaoni hivyo tuishi katika kuangalia mambo kwa uangalifu katika kile kinachosambazwa na tunachokiona.
0676 559 211
raymondpoet@yahoo.com