Mafunzo ya Ufundi Stadi, silaha muhimu kuelekea Tanzania ya viwanda

0

Na Mohamed Wage

MOJA kati ya sababu kubwa ya ukosefu wa ajira katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, ni kuwepo kwa tofauti kati ya elimu itolewayo na taasisi za elimu na hitajio halisi la soko la ajira.

Barani Afrika kumekuwa na wahitimu wengi wa fani za sayansi ya jamii na biashara huku kukiwa na kundi dogo la wahitimu wa fani za uhandisi, Sayansi na ufundi kwa ujumla. Upungufu wa wataalamu katika eneo la Sayansi, Uhandisi na Ufundi maana yake Mataifa haya yanahitaji nguvu kazi kutoka nje ya bara hili ili kuziba pengo hilo.

Nchi nyingi zilizoendelea kama Finland, Ujerumani, Austria, Uswisi na nyinginezo, pengo kama hili la wataalamu limezibwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwekeza katika mafunzo ya elimu ya ufundi kwa vijana wao, mafunzo haya ya ufundi yameleta matokeo ya haraka na kwa muda mfupi.

Kwa bahati mbaya, nchi nyingi zinazoendelea hasa za Afrika, kumekuwa na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya elimu ya mafunzo ya ufundi, hivyo kuwafanya vijana wengi kutovutiwa na kujiunga na elimu ya mafunzo hayo.

Mafunzo ya elimu ya ufundi kwa nchi hizi hayajapewa kipaumbele na yanatazamwa kuwa ni chaguo la pili baada ya vijana kukosa fursa ya kuendelea na elimu ya juu (Njia mbadala ya kuendelea na Elimu).

Moja kati ya tafiti iliyowahi kufanywa kuhusu mafunzo ya elimu ya ufundi barani Afrika, inaonyesha kuwa mafunzo haya yanavutia chini ya asilimia tano ya vijana katika Elimu.

Moja kati ya sababu ya msingi kwa nini udahili wa vijana katika eneo hili ni mdogo; mafunzo haya yananasibishwa na uwezo mdogo wa kitaaluma, pia inaonekana kuwa hakuna muendelezo wa vijana kufikia elimu ya juu kupitia mafunzo hayo (look as Dead End).

Aidha, kumekuwa na mazingira yasiyo rafiki ya kusoma na kujifunzia taaluma hii. Matumizi madogo ya teknelojia na uwepo wa walimu wachache ambao pia hawana mazingira rafiki ya kufundishia ikiwemo miundo mbinu bora na ya kisasa.

Finland ni moja kati ya nchi zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadili mtazamo wa vijana na jamii kuyapa thamani mafunzo haya na kuyafanya yavutie vijana wengi na kupunguza kwa kiasi kikubwa ombwe la wataalamu katika sekta ya Viwanda na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Nchi nyingine zilizoendelea kama Austria na Uholanzi ambazo mafunzo ya elimu ya ufundi yamepewa kipaumbele, zimefanikiwa kuwa na kiwango kidogo cha ukosefu wa ajira kwa vijana wake.

Wakati huu Tanzania inapoelekea kuwa Taifa la uchumi wa kati na Viwanda, hatuna budi kuwa na mikakati ya makusudi sio tu ya kujenga vyuo vingi vya elimu ya mafunzo ya ufundi, bali mkakati wa kubadili mtazamo wa vijana na jamii kwa ujumla kuhusu mafunzo haya.

Ikumbukwe kuwa, Viwanda vitahitaji wataalamu ambao ni zao la mafunzo ya elimu ya ufundi. Ili kuboresha eneo hili la mafunzo kama Taifa tunaweza kufanya yafuatayo;-

Mosi, tujifunze kwa wenzetu waliofanikiwa kubadilika mtazamo wa jamii hasa vijana na kuyafanya mafunzo haya kuvutia vijana wengi, mfano Finland ambapo zaidi ya 50% ya vijana huomba kujiunga na mafunzo haya kila mwaka, huku ushindani wa kupata ukiwa ni mkubwa kulinganisha na mafunzo ya elimu nyingine.

Mafanikio haya ya Finland yana sababu za nje na za ndani moja ni kubadili sera yao ya elimu. Mwaka 2000 mabadiliko ya sheria yalifanyika na kuyafanya mafunzo ya ufundi yapelekee muhitimu kufika elimu ya juu. Kwa maana nyingine, mitaala iliboreshwa ili mhitimu wa mafunzo haya aweze kufika chuo kikuu (Elimu ya juu).

Pili, uwepo wa mafunzo kazini kwa vijana watakaopata fursa ya kujiunga na mafunzo ili kuboresha uwezo wao hasa wakati huu ambao kuna mabadiliko makubwa ya teknolojia.

Vijana wengi wakienda kwenye makampuni, hawapati fursa ya mafunzo ya vitendo, badala yake wamekuwa wasoma magazeti na kutumwa tu, hivyo wanakosa ujuzi.

Tatu, kuwepo mkakati wa makusudi wa kubadili fikra na mtazamo wa vijana kuhusu mafunzo haya na kuonyeshwa kuwa, unaweza kuendelea zaidi na masomo ya juu kupitia mafunzo haya.

Nne, kuwekeza pesa za kutosha katika eneo hili la mafunzo ya ufundi badala ya kutegemea pesa za wahisani ili kuwe na ushindani na mafunzo mengine, hasa ya elimu ya Sekondari.

Tano, pia ni lazima tutengeneze mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishia vijana wetu. Sita, kuwahusisha waajiri, Sekta binafsi katika kupanga na uundaji wa mitaala, mafunzo na hata uwekezaji kwa ujumla.

Saba, kuboresha Sekta ya ukaguzi wa ubora katika mafunzo ya elimu ya ufundi ili kuhakikisha elimu inayotolewa ndio ile inayohitajika katika soko la ajira.

Haya na mengine ni muhimu yakazingatiwa wakati huu ambao jitihada za kuboresha elimu ya mafunzo ya ufundi zinafanyika. Mafunzo ya ufundi yaliyoboreshwa yatatoa nguvu kazi muhimu kufanikisha Tanzania ya Viwanda.

mohamedwage09@gmail.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here