Maendeleo ya Taifa hayaji kwa majaliwa – Dkt. Mpango

0

Na Mwandishi Wetu, MAELEZO

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip amesema, maendeleo ya Taifa lolote hayaji kwa majaliwa bali kwa fikra bunifu pamoja na jitihada za dhati za vizazi vya Taifa.

Dkt. Mpango amesema hayo leo Julai 17, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Dira hiyo.

“Maendeleo ya Taifa lolote hayaji kwa majaliwa, wala maendeleo hayaji kwa kuachia nguvu ya soko kwamba itafanya kazi yake. Taifa linajengwa kwa fikra bunifu, pamoja na jitihada za dhati za vizazi vya taifa pamoja na kutafsiri fikra hizo kwa vitendo na nidhamu”, alisema Dkt. Mpango.

Ameendelea kusema kuwa, nchi zote zilizofanikiwa kimaendeleo zilifanya mambo matatu, kwanza ziliwekeza katika kuandaa Dira za muda mrefu; pili, zilianzisha taasisi za kutafsiri Dira zao kiuhalisia, lakini walizitegemeza pia taasisi hizo na jambo la tatu ni kufuatilia utekelezaji.

Dkt. Mpango alisema kuwa, Dira ya Taifa ni muhimu kwa sababu ndiyo inayotoa ufahamu wa uwelekeo, lakini pia hatima ya Taifa na kuunganisha nguvu za raia kuelekea kwenye malengo ya pamoja na matamanio.

Aidha, alisema Dira ya Taifa inachochea matamanio ya wananchi, inahamasisha wananchi kuchukua hatua, inaongoza maamuzi ya kisera na hatimaye ndiyo inayoumba mwenendo wa maendeleo ya nchi

“Wakati sasa umefika nchi yetu tuifikishe kwenye nchi ambazo ziko kwenye kipato cha kati ngazi ya juu, na tufanye hivyo sio kwa takwimu tu, lakini tufanye kwa maisha bora ya Watanzania kiuhalisia. Na mimi nina amini inawezekana tukitekeleza Dira 2050 kwa nidhamu,” alisema Dkt. Mpango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here