Maajabu ya Simba wawili wa Tsavo mwaka 1898

0

Na Igamanywa Laiton

GAZETI la ‘The Expectator’ la Machi 3, mwaka 1900 lilikuwa limebeba makala yenye kichwa kinachosomeka ‘Simba wazuia ujenzi wa Reli’. Gazeti hilo lilikuwa likiwarejea Simba wa hifadhi ya Tsavo.

Simba hawa wawili wachanga walikula wapagazi, watumwa na wajenzi wasiopungua 50 (ukijumlisha na wenyeji idadi ilikuwa ikikaribia 130) kwa muda mfupi.

Hawakuwa Simba wa kawaida, kwani kabla ya kumla mtu waliyemuua walimchuna ngozi kwanza, ni Simba pekee wa kwanza wa aina yake kuwinda wawili kwa kushirikiana. Ilikuaje?

Mwaka 1895 bunge la Uingereza lilipitisha mswada juu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa reli kati ya Pwani ya Mombasa hadi katika ziwa Viktoria.

Reli hiyo ilikuwa ya kimkakati na muhimu kwa kuwa miaka hiyo Afrika ilikuwa katika kumegwa na kupiganiwa na Mataifa komavu ya kibepari baada ya ule mkutano maarufu wa Belini.

Reli hiyo ingesaidia katika kusafirisha wanajeshi na maafisa ili kulitawala zaidi Afrika kwa niaba ya Muingereza. Ujenzi ulianza rasmi mwaka 1896 chini ya Injinia kiongozi aitwaye George Whitehouse.

Zaidi ya watu 35,000 waliletwa kutoka India kufanya kazi kama vibarua na mafundi. Na kufanya karibu asilimia 95 ya wafanyakazi katika mradi huo. Kumbuka Wahindi hawa walikuwa hawana uzoefu wowote na mapori ya Afrika.

Kwa kuwa reli hii ilikuwa lazima ifike Uganda, njia rahisi ilikuwa kupita katika mbuga ya Tsavo. Hifadhi ya Taifa ya Tsavo Magharibi (Tsavo West National Park) iko katika Mkoa wa Pwani ya Kenya.

Mbuga hii ina upana wa eneo la eneo wa Kilomita 9,065. Barabara ya A109 barabara ya Nairobi – Mombasa na reli hugawanya mbuga katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi.

Sehemu ya Magharibi ni maarufu zaidi kutokana na mandhari yake yanayovutia zaidi kama vile Chemichemi ya Mzima, wanyamapori mbalimbali, mfumo mzuri wa barabara, hifadhi ya vifaru, uwezo wa kupanda mwamba na wageni huongozwa wakati wanatembea kando ya mto Tsavo.

Mbuga hii inaendeshwa na Shirika la Huduma kwa Wanyama Pori la Kenya (maarufu kama Kenya Wildlife Service). Ni mbuga yenye mto maarufu wa Tsavo, mbuga yenye historia mbaya kwa kuwa misafara ya Utumwa ilikuwa ikipita katika mbuga hii na mara nyingi wale watumwa dhaifu walikuwa wakiachwa waliwe na wanyama wakali, kiasi simba katika mbuga hiyo, kuzoea ladha ya nyama ya binadamu.

Wenyeji wa maeneo haya waliwinda wanyama pori, walivua samaki na pia kufunga wanyama wa kinyumbani. Kwa sababu ya upungufu wa maji kutoka mto Galana, makazi ya binadamu katika Tsavo yalilenga maeneo yanayomiliki bonde hilo na katika eneo wazi ukielekea upande wa Magharibi.

Wafanyabiashara waswahili walifanya biashara na wenyeji wa Tsavo kwa kuuza na kununua pembe za ndovu, ngozi za wanyamapori, na pengine watumwa mnamo miaka 700 baada ya kifo cha Kristo (na pengine mapema).

Hakuna ushahidi wa moja kwa moja ya kuonyesha kwamba, waswahili walikuwa wakoloni wa eneo la Tsavo. Badala yake, biashara iliimarishwa kwa kupelekwa kwa bidhaa kwenda na kutoka Pwani ya Swahili.

Karne ya 19, Wapelelezi kutoka Uingereza na Ujerumani walidai, watu ambao sasa tunawaita Orma na Waata wakati wa safari zao kupitia ‘nyika,’ walionekana kama maadui katika maslahi yao.

Tsavo ilibakia ya nchi kwa wafugaji wa Orma na Wamasai na wawindaji na wakusanyaji wa Waata hadi mwaka wa 1948, wakati ilikubaliwa rasmi kama Mbuga ya Kitaifa. Wakati huo, idadi ya wazawa ilihamishwa kwa maeneo ya Mtito Andei na Voi na vilevile maeneo mengine karibu na Vilima vya Taita.

Kufuatia uhuru wa Kenya mwaka wa 1963, uwindaji ulipigwa marufuku katika mbuga hii na usimamizi wa Tsavo ulisalimishwa kwa mamlaka ambayo hatimaye ikawa Kenya Wildlife Service. Tsavo sasa huvutia watalii wanaopiga picha kutoka kote duniani wenye riba ya kushauku upana wa jangwani na Mandhari ya ajabu.

Tukirejea nyuma, Machi 1898 kipande cha reli kilifika katika Mto Tsavo. Kwa kuwa mto ulikuwa mkubwa, ilihitajika kujenga daraja kubwa, hivyo ikalazimu kupiga kambi pembezoni mwa mto.

Kwa muda mfupi, vifaa na vibarua kutoka kambi kuu iliyokuwako Kilindini wakamiminika Tsavo. Kelele za nyundo, mashine zikisaga kokoto na miamba, misumeno ikikata mbao na za vibarua zikatawala na kuzima ukimya uliokuwa ndani ya mbuga hiyo.

Mwandishi wa kitabu ‘The Man Eaters of Tsavo’ Lutenanti Kanali John H Patterson (ambaye alikuwa Injinia mkuu wa ujenzi wa daraja) anaandika: “Baada ya kazi kuanza tu, simba wawili wala watu walijitokeza, na kwa miezi tisa (kufikia Disemba 1898), Simba hao walifanikiwa kusimamisha kabisa ujenzi wa reli baada ya wafanyakazi wote kukimbia kambi na kutekeleza kila kitu”.

Patterson anasimulia kuwa Simba hao walivamia kambi moja baada ya nyingine na kuburuza watu mmoja mmoja kuelekea vichakani na kisha kuwachuna ngozi na kula baadhi ya viungo na kutekeleza miili huko huko porini.

Kutokana na werevu na upekee wa Simba hao wawili katika namna walivyokuwa wakivamia na kutoroka na watu. Ilianza kuaminika kuwa Simba hao ni mizimu iliyokuwa imekasirishwa na ujenzi wa reli na daraja katika ardhi ya Tsavo.

Simba hao wawili walizidi kuwa tishio zaidi baada ya kuanza kuwafuata majeruhi hadi katika vituo vya afya na kushambulia tena.

Lutenanti Patterson alijiona mwenye deni kubwa juu ya mashambulizi ya simba hao, kwanza kwa kuwa Simba hao walianza kushambulia baada ya Patterson kuwasili na pili ni Patterson aliyekuwa na jukumu la kusimamia usalama.

Hivyo, akiwa peke yake akaanza kazi ya kuwawinda simba hao na hatimaye Disemba 9 akafanikiwa kumuua Simba wa kwanza na kisha asubuhi ya Disemba 29, akammalizia wa pili, lakini ikiwa imebaki chupu chupu na yeye kuuliwa.

Ni baada ya Simba huyo aliyemjeruhi kumgeukia na kuanza kushambulia, inasemekana kila Simba alikuwa na urefu wa futi tisa na ililazimu watu nane kumbeba Simba mmoja kumrudisha kambini.

Baada ya hapo shughuli za ujenzi zikarudi katika hali ya kawaida na hatimaye daraja lilimalizika Februari 7 mwaka 1899. Japo miundombinu yake ilikuja kuharibiwa na majeshi ya Ujerumani katika vita ya kwanza ya dunia msingi wa daraja hilo uliendelea kusimama na kukarabatiwa tena.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here