Kituko cha Mahakama na Tume ya Afrika ya haki za raia

0

Na Yahya Msangi

KUNA video inasambaa kwenye mitandao ya kijamii inayomuonyesha kiongozi mmoja wa kiroho akiilaumu Serikali kwa uamuzi wake wa kujitoa kwenye mahakama ya Afrika ya haki za raia.

Kiongozi huyo na baadhi ya wanasiasa wa hapa nchini ambao wanamuunga mkono, hawajui historia ya mahakama hii na mauzauza yake.

Nilibahatika kuongoza kikundi cha waangalizi wa kiraia (civil observers) wakati mjadala wa kuanzisha mahakama hii na tume yake miaka ya 1980.

Nilishiriki kushinikiza vyombo hivi viwili vianzishwe pamoja na Tume ya Afrika ya Kusimamia Uchaguzi (PAN AFRICA UNION ELECTORAL COMMISSION) na fuko la kugharamia Uchaguzi (PAN AFRICA ELECTORAL FUND).

Baada mjadala wa takriban miaka saba, wakuu wa nchi (Head of States) wakakubali iundwe Tume ya Haki na mahakama yake. Tume na fuko la kugharamia uchaguzi vikakataliwa pamoja na pendekezo la kuweka ukomo wa kuwa mkuu wa nchi.

Ukaanza mjadala wa wapi yawe Makao Makuu ya tume ya haki za raia na wapi yawe Makao Makuu ya Mahakama. Kuhusu mahakama, Jumuiya ya SADC na EAC vikapendekeza Arusha Tanzania.

Mwenyekiti wa wakati wa SADC wakati ule Hayati Robert Mugabe alisema wazi, hakuna nchi nyingine ingestahili kuliko Tanzania. Kwa maneno yake “Tanzania ndio nyumba ya Haki Afrika”! Hakuna nchi hata moja ilipinga.

Tatizo lilikuwa kuhusu Tume ya haki. ECOWAS walipendekeza Gambia ya enzi za Yaya Jammeh. Baadhi ya nchi za Kifaransa zilipinga. Nchi nyungine zilikuwa zinajua Gambia haina historia nzuri ya haki za raia ziliamua kwa makusudi kujiunga mkono Gambia. Hawakutaka waburuzwe na Taifa la nje ya Afrika. Makao Makuu ya Tume yakawa Banjul.

Ili lesi ziweze kupelekwa kwenye Tume na mahakama nchi mwanachama AU lazima iridhie, lazima iandike kutoa ruksa raia wake au Taasisi nchini mwake kupeleka kesi. Bila hivyo, Mahakama na tume haitakuwa na Mamlaka juu ya nchi husika.

Kichekesho kikaja hivi; nchi nyingi zikagoma kutoa hicho kibali, baada ya muda mfupi, zikatokea nchi 11 tu kati ya 55 ndipo zikatoa kibali. Tanzania ikiwa nchi ya mwanzo kabisa kutoa kibali. Ni enzi ya utawala wa Jakaya Kikwete.

Katika ukanda wetu wa SADC na EAC hakuna nchi nyingine. Licha ya mikutano na majadiliano nchi nyingine zikakataa katakata kujiunga na mahakama hiyo.

Kikaja kituko kingine, ukaanza mtindo wa NGOs za Kenya kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuishitaki Serikali ya Tanzania kwenye mahakama ya Afrika! Yaani nchini kwao hawawezi kuishitaki Serikali yao, lakini kwa kupitia mgongo wa NGO’s na vyama vya upinzani wanakuja kuishitaki Serikali ya Tanzania!

NGO’s za Tanzania zenyewe haziwezi kuishitaki Serikali ya Kenya kwa kigezo kuwa Kenya hajatoa idhini ya kushitakiwa! Ndipo waliojiunga na mahakama kwa kutoa kibali wakaona sasa ni hii biashara kichaa. Yale yale ya kujiunga ICC huku wengine wamebinya! Tunajikaanga kwa mafuta yetu wenyewe kwa nini?

Mmoja mmoja akaanza kujitoa. Mpaka mwanzoni mwa Mwaka huu, nchi nne ikiwemo Tanzania zikaamua kujitoa! Sasa nadhani zimebaki nchi saba, nazo zimeshatoa kusudio la kujiondoa. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ndiye aliyeamua tujitoe. Kwa hili alikuwa sahihi. Tusirudi Mpaka mahakama ifanye kazi kwa wote.

Punde tunaweza kuwa na Mahakama ya Afrika yenye majaji waliobobea, lakini hawana kesi ya kuamua. Tanzania na wenzake wanataka ama iwe lazima kwa kila mwanachama, ama ibaki bila kazi. Haiwezekani iwepo mahakama inayofanya kazi kwa wachache na wengine wawe huru kufanya watakavyo.

Naamini kiongozi huyu wa kiroho na wanaomshabikia hawajui, kwamba msimamo wa Tanzania ni kutaka mahakama hiyo ifanye kazi kwa wote, maana ilianza kutumiwa vibaya kuihujumu nchi yetu. Kwa hili, Seriklai isiyumbe. Msimamo uendelee kuwa huo huo, vinginevyo isiwepo kabisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here