Na Togolani Mavura
NI kawaida siku hizi kupokea simu, meseji ama ugeni wa ndugu, jamaa na marafiki kukuuliza na kuomba kama unaweza kusaidia kupatikana kwa ajira kwa ajili ya kijana au binti yao ama kufuatwa na kijana au binti mwenyewe. Mara nyingi utaachiwa nakala kivuli za vyeti vya ufaulu kwa ajili ya rejea.
Pale nawe unapojaribu kupigia wenzako wawili watatu kuomba wakusaidie, unakuta na wao wana maombi kama yako mengi na wengine wana wenza wao au wadogo zao nao wanatafuta ajira. Wakati mwingine tunaangukia kwenye lawama kuwa sisi si watu wa msaada kwa kuamini kuwa uwezo wa kusaidia tunao ila tu hatuna nia.
Swali lililonijia haraka haraka mawazoni mwangu ni kwa nini siwaoni Watanzania wenye Asili ya Kiasia na Kiajemi wakitembea na bahasha za khaki zenye nakala vivuli nao wakitafuta ajira? Nikajikuta najiuliza tena, mbona ni kama idadi yao katika Vyuo Vikuu vyetu ni ndogo sana?
Vile vile pale wanapokuwapo hao wachache, mara nyingi huwakuta katika fani fulani fulani tu? Mara nyingi utawakuta kwenye shahada za udaktari na famasia, uhandisi, sayansi ya mifumo ya kompyuta na masuala ya fedha ikiwemo bima, uhasibu, biashara na masoko.
Ni nadra sana kuwakuta wenzetu hawa katika masomo ya fani za historia, mambo kale, sayansi ya siasa na utawala, sayansi jamii na sheria. Juma lililopita nilipata fursa ya kuhudhuria mahafali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika ukumbi ule uliokuwa na wahitimu wapatao 3,000 wa shahada za kwanza, pili na tatu, nilijaribu kuhesabu hawa wenzetu hawakuzidi 10.
Pamoja na kutoonekana kwa wenzetu hawa huko kwenye misururu ya Bodi ya Mikopo, usaili wa ajira Serikalini na mahala pa kutolea nakala vivuli (photocopy), wanaonekana kwa wingi katika foleni za benki, TRA, Brela na Bandarini. Hili linafikirisha na limenipa maswali. Kuna kipi wenzetu wanapatia ambacho sisi tunakosea? Kipi tunaweza kujifunza kutoka kwao?
Bila shaka mimi si wa kwanza kujiuliza maswali haya. Wengi wamekuwa nayo. Hata ukitazama matajiri wakubwa hapa nchini utakuta wanatoka katika jamii hiyo hiyo tu. Karibia kila jamii zilizoko nchini zina bilionea wake walau mmoja anayeibeba jamii yao. Iwe Ismailia, Ithna Asheria, Hindu, Bohora.
Hali kadhalika Waburushi, Washihiri, Wamanga nk, Ni vigumu kuwataja Watanzania Waasia ambao wengi wao pia ni mabalionea wa msimu na wengine huibuka na kuondoka na awamu ya uongozi wa nchi. Wenzetu hawa wapo tu. Hata ukisikia dili kubwa pia utakuta wapo wao.
Binafsi, nimebahatika kuishi, kusoma na kukulia jirani na jamii hizi. Nimejifunza pia mawili matatu kutoka jamii zao ambayo huko awali sikuwahi kuyapa umuhimu mkubwa. Kadri umri unavyokwenda napata ufahamu na uelewa juu ya dhana kadhaa juu yao.
Naweza kusema, wengi wao wana kipato cha kawaida sana tena chini ya kipato cha wengi wa jamii yetu. Isipokuwa, mfumo wao wa maisha na utamaduni wao umejijenga katika taratibu kadhaa za maisha ambazo zinawapa faida kadhaa kushinda sisi. Aidha, muono wao juu ya maisha nao unasaidia kuyatafsiri maisha katika namna tofauti na sisi.
Tofauti na Watanzania Waafrika, wenzetu hawa kwa sababu za kihistoria wamejikuta wanasukumwa kutafuta maisha katika sekta binafsi zaidi kuliko sekta ya umma. Kwa sababu za kihistoria, baada ya uhuru kulikuwepo wimbi kubwa la kutoa kipaumbele kwa Watanzania Waafrika ambao walionekana kukosa fursa wakati wa uhuru katika utumishi wa umma (africanization). Matokeo yake ilikuwa ni kuzaliwa kwa ‘unyanyapaa bubu’ (silent discrimination) dhidi yao hali iliyowafanya wasitamani kutafuta ajira katika Serikali na taasisi zake.
Hii kwao ilikuwa ni faida ya kwanza kabisa. Kwa mtazamo wangu, hii iliwafanya wasiione hatima yao katika ajira (employment) ambazo nyingi zilikuwa katika sekta ya umma. Wao wakajikita zaidi katika biashara na kazi (jobs) na ajira chache katika shughuli wanazozimiliki ambazo ni biashara. Ndio maana utawakuta zaidi katika ajira za masoko, uhasibu, menejimenti na baadae mifumo ya kompyuta.
Kutokana na mazingira hayo, hali hiyo ikawapelekea pia kuwekeza zaidi katika elimu ya stadi za kazi na vitendo badala ya nadharia na ufahamu. Kwa lugha nyepesi, kwao hakuna umuhimu sana wa kufika chuo kikuu kama huendi kusomea udaktari, ufamasia, uhandisi na kwa kiasi uhandisi wa mifumo ya kompyuta.
Ndio sababu kadiri unavyokwenda kwenye elimu ya sekondari ya juu (Advanced Level Secondary Education) idadi yao inapungua sana. Badala ya kuhangaika na kutegesha michepuo (balancing combination), wao wanaanza kusomea stadi za kazi moja kwa moja. Wengi wanaanza kusomea elimu ya vyeti na utaalam wa masuala mahsusi.
Utawakuta kwenye mitihani ya bodi (chartered institutes) za uhasibu za ndani na nje ya nchi, mitihani ya bodi za mifumo ya teknolojia na mifumo ya computer, masuala ya benki, bima, masoko, menejimenti na rasilimali watu, masuala ya forodha (customs clearing and forwarding) na ualimu wa chekechea (Early Childhood Teachers Training).
Ndio sababu hutawakuta kwenye msururu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi. Kwao, hakuna ufahari kuwa na cheti cha shahada ya kwanza ya Chuo Kikuu (University Degree) bali Cheti cha Stadi.
Kwa kuwa kwao ajira (employment) si hatima yao, bali hatma yao iko kwenye kazi na shughuli za kutafuta rizki na kipato (jobs), hivyo mfumo wao wa maisha umewaandaa kwa kutafuta kipato (income) na si mshahara (salary). Hii inawafanya kuwaandaa watoto wao kutafuta na kuheshimu kipato.
Maana yake, wanawaandaa kwa kazi ama shughuli yoyote. Muhimu kwao ni kupata kipato kuwezesha kuendesha maisha. Tofauti na ajira, kipato si lazima kiambatane na heshima ya kukaa ofisini, kwenye kiyoyozi, kuvaa rasmi sana na kuwa na hadhi.
Mara nyingi, hayo ambayo huambatana wakati mwingine na mshahara duni. Kipato si lazima kiwe cha mwezi na anayetafuta kipato anaweza kupata zaidi ya yule anayepata mshahara wa mwezi. Isitoshe, kuishi na kipato kunahitaji pia nidhamu tofauti kuliko kuishi na mshahara.
Mengi ambayo nimeyaandika hapo juu yaweza yasiwe mapya sana. Tunaweza kutoa mifano mingi ya Watanzania Waafrika ambao nao wanayafanya hayo. Hata hivyo, hayo pekee si yanayofanya wenzetu hususan Watanzania wa jamii ya kiasia kupata matokeo tofauti.
Siri kubwa iko katika mfumo wa maisha na mfumo wa mbeleko (social support system) walionao. Hapa ndio tofauti kubwa kati yetu na wao ilipo. Hapa ndio njia panda tunayoachania.
Kutokana na mazingira yao na haja ya kujihami (self-help), pengine kutokana na uchache wao, wamejitengenezea mifumo inayohakikisha ustawi wa jamii zao. Wamehakikisha Jumuiya zao zinakuwa na uongozi na mifumo ya uendeshaji, wanamiliki huduma za jamii ikiwemo shule, hospitali na hata makaburi.
Wamekwenda mbali zaidi kuwa na mifumo inayokusanya na kuhifadhi takwimu na kumbukumbu ya kila mmoja wao (census and data registry), kuwa na mifumo yao fedha na kumiliki mabenki (financial systems), mifuko ya wakfu (endowment funds) wa kusaidia wasiojiweza na mifumo ya usuluhishi wa migogoro na maamuzi (dispute and conflict resolution mechanisms).
Kwa lugha nyepesi ni kama wanazo Mamlaka na serikali ndogo katika jamii zao. Na mifumo yao huwafanya kila mwana Jumuiya kuwa tegemezi zaidi kwa mfumo huo kama ‘samaki na maji’. Kiasi kwamba, kutengwa na jumuiya yako kwa kukiuka miiko na masharti ni jambo ambalo kila mmoja analiepuka.
Kutokana na mifumo hiyo, kila mwana Jumuiya yao, hata kama hana fedha, anajikuta anamiliki mtaji jamii (social capital) mkubwa sana wa kuanzia maisha kuliko wenzetu na sisi. Kwa kuwa tu mwanajumuiya, unaaminika, unakopesheka, unaajirika na unadhaminika popote. Ni rahisi kwa mwanajumuiya kutafuta na kupata kazi.
Kazi itatangazwa kwanza ndani ya Jumuiya yao kabla ya kutangazwa nje. Ukihitaji mkopo, ni rahisi kukopesheka na kuminiwa bila kuwa na dhamana yenye thamani kubwa (collateral). Ukiugua, unayo bima ya uhakika ya matlbabu na pale ambapo kuna tozo za huduma, basi tozo kwa wanajumuiya huwa ya chini kuliko ya wasio wanajumuiya katika shule na hospitali zao.
Aidha, mwanajumuiya anapopata tatizo, Jumuiya inayo wajibu wa kumhangaikia. Ukifiwa, huna sababu ya kuwaza kitapikwa nini na marehemu atazikwa wapi. Wajibu wako ni kulia na kuomboleza maana Jumuiya itashughulika. Hali kadhalika, kijana akihitaji kuoa na kuanza maisha.
Kila mwana Jumuiya ana wajibu kwa wanajumuiya wengine. Haishangazi kuwa ni nadra kuwakuta wamefikishana Polisi na Mahakamani panapotokea kutokuelewana. Na hata anaposhitakiwa na mtu wa nje ya Jumuiya yao, Jumuiya humuwekea dhamana.
Ndio maana hutawakuta wenzetu hawa kwa wingi katika mahabusu zetu. Ukimkuta, ujue hiyo kesi ni ngumu sana.
Mfumo wao huo wa maisha unawafundisha jambo lingine muhimu ambalo sisi tunapungukiwa. Nalo ni nidhamu na utamaduni wa kuweka akiba (saving discipline and culture).
Katika kuishi kwangu nao, nimeona namna ambavyo vipaumbele vyao ni tofauti na vyetu. Mathalan, katika utamaduni na mifumo yetu ya maisha tunafuja na kutapakanya sana mali. Vitu kama ndoa za mitala (polygamy) na ‘nyumba ndogo’ na namna tunavyoendesha ndoa hizo, idadi kubwa ya watoto tunaozaa, matumizi makubwa ya anasa, starehe na ulevi, ufahari katika umiliki wa vitu tusivyovihitaji katika maisha, lakini tunavihitaji zaidi kwa ajili ya kukogana nk.
Tunafanya harusi na misiba ya gharama na ni rahisi zaidi kuchangishana kwa harusi ya siku moja na maziko ya kifahari ya siku moja kuliko kumchangia mtoto wa jamii yetu ada, kuanza maisha ama kumtibu anapoumwa. Sisi vipimio na vigezo (metrics) za mafanikio ni kumiliki nyumba ya kifahari na magari (nyingi ya hizi ni mitaji mfu /dead capital), kwao, ni kumiliki biashara na sifa ya jina la familia.
Mfumo wetu wa familia (extended family) nao ni tegemezi sana kwa watu wachache, ni mfumo unaowaelemea wachache wenye nacho na kuwazuia watu wasiweze kujiwekea akiba. Ni rahisi kukuta mtu mmoja ama familia moja imebeba familia tatu ama ukoo.
Kwa wenzetu utamaduni ni kuungishana. Ukiwa na biashara, wa Jumuiya yako watanunua kwanza kwako kabla ya kununua kwingine na hawatakudhulumu ama kukulalia kwa sababu wewe ni rafiki au ndugu. Sisi ni tofauti. Ukianzisha huduma au biashara, ndugu na marafiki ndio ama hawatanunua, ama wakinunua wanakulalia, ama hawakulipi kwa wakati ama hawakulipi kabisa.
Aidha, wenzetu wanafungua biashara zenye kuongeza mnyororo wa biashara na thamani (value chain) kutoka pale anapoishia mwenzako na si kuigana (copy cut) na kumalizana wenyewe kwa ushindani usio na afya (unhealthy competition). Matokeo yake, sote hatukui na baada ya muda, sote tunakufa.
Nimalizie kwa kusema, mtazamo huu si timilifu wala si utafiti wa kitaaluma. Hata hivyo, unaweza kusaidia wanataaluma wetu kupata kwa kuanzia na sisi wengine kupata kutafakari. Kwa kufanya hivyo, kutatusaidia kuondokana na dhana fulani fulani ambazo tumezikumbatia ambazo hazitusaidii sana.
Ile dhana kuwa wenzetu hawa ni wezi, walibebwa na historia, ni matajiri tu kwa kuzaliwa na wanarithishana utajiri ni dhana ambazo hazitufikishi popote zaidi ya kutujengea chuki, mashaka na kututia ganzi. Jawabu lipo katika kuwasoma na kuwaelewa. Na somo lenyewe ni kuwa nidhamu (discipline) na taasisi imara (robust institutions) ndio jawabu la jamii yoyote yenye mafanikio iwe ya binadamu ama mdudu. Ndio maana nyuki na siafu wanafanya mambo makubwa ya kujenga (constructive) wakati nzi na mbu wanafanya makubwa ya kubomoa (destructive).
Hata katika jamii zetu ambazo zimefanikiwa kiasi kwenye kujenga nidhamu na taasisi imara kama familia na Jumuiya, unaiona tofauti. Wenzetu Wapemba, Wakinga na Wachagga wana kiwango fulani cha nidhamu na wanamifumo yao ingawa si kwa mapana kama ya wenzetu na tunaona ambavyo wanapata matokeo chanya. Vivyo hivyo ukishuka kwa baadhi ya koo na familia ukweli huu unajidhihirisha.
Ndio maana tunayo kwa mfano, familia ya Marehemu Hubert Kairuki wanaomiiki hospitali ya Kairuki na Chuo Kikuu cha Tiba kwa miaka zaidi ya 25, 19 kati ya hiyo, baada ya kufariki muasisi wa hospitali hiyo. Ni moja ya mifano michache tunayoweza kuitoa. Lipo la kujifunza kutoka kwa wenzetu hawa kama tunataka kutoka hapa tulipo. Bahati mbaya haya si mambo wataalam wetu wa uchumi, jamii na biashara wanatafiti wala kuchapisha.