Kibaha DC yapaza sauti dhidi ya ukatili kwa watoto

0

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imeungana na Mataifa mengine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuhimiza ulinzi wa haki za watoto na malezi bora katika jamii.

Maadhimisho hayo yamefanyika Juni 16, 2025, katika ukumbi wa NMB uliopo Mlandizi, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wazazi, walimu pamoja na watoto kutoka maeneo tofauti ya Halmashauri hiyo.

Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Halima Jongo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema na mazingira salama ili waweze kuwa nguzo imara ya maendeleo ya Taifa.

“Natoa rai kwa jamii yote kuwajibika katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, elimu sahihi na kinga dhidi ya vitendo vyote vya ukatili. Hili ni jukumu letu sote kama wazazi, walezi na viongozi,” alisema Jongo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Grace Haule, alieleza kuwa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri inapanga kuanzisha Mabaraza ya Watoto yatakayosaidia kutoa fursa kwa watoto kueleza changamoto zao na kushirikiana katika kuzitafutia suluhisho.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo, Yahaya Mbogolume, amesisitiza umuhimu wa malezi yanayozingatia Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, akibainisha kuwa uelewa wa sheria hiyo utasaidia kupunguza ukatili dhidi ya watoto.

Aidha, Afisa Lishe wa Halmashauri, Coletha Chapile, aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kwa lengo la kupunguza viwango vya udumavu vinavyolikabili Taifa.

Nao Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia chini ya Inspekta Tumaini Steven Ulimboka, limewahimiza watoto na wazazi kuripoti mara moja vitendo vyote vya ukatili ili viweze kufanyiwa kazi kisheria.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16, kwa kumbukumbu ya mauaji ya watoto wa Kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini mwaka 1976, waliouawa wakidai haki ya elimu bora.

Umoja wa Afrika ulipitisha maadhimisho haya mwaka 1990 kwa lengo la kuendeleza juhudi za kupinga ukatili na kukuza ustawi wa watoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here