📌 Fursa lukuki za kiuchumi zaibuliwa
📌 Wananchi waeleza namna maisha yao yalivyobadilika
WANANCHI wa Kijiji cha Mapili Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kubadili maisha yao kupitia mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Wametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti kijijini hapo Agosti 13, 2025 wakati wa kampeni maalum ya uhamasishaji wa matumizi ya umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali kote nchini.
“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kabla ya kupata nishati hii ya umeme mazingira hayakuwa mazuri, usiku hatukuwa na mwanga sasa hivi tunaishi kwa amani na hata baadhi ya shughuli za kimaendeleo zinafanyika hadi muda wa usiku lakini pia tunapata habari kwa kutazama luninga muda wowote tunaotaka pia baadhi ya vijana wamepata ajira kupitia umeme,” alisema Mwalimu Mstaafu, Mkazi wa Kijiji cha Mapili, Amos Katawa.

Mrisho Mussa Fundi Uchomeleaji katika Kijiji cha Mapili alisema kabla ya umeme kufika kijijini hapo walikuwa wakilazimika kufanya shughuli zao maeneo ya mjini ambapo ni mbali na kijijini hapo na hivyo kusababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa walizokuwa wakizalisha pamoja na kutumia muda mrefu kukamilisha kazi.
“Tulikuwa tunalazimika kutengenezea mageti huko Inyonga na kisha tunasafirisha, hali hii ilikuwa ni usumbufu kwetu hadi kwa wateja wetu, lakini sasa mambo yote tunafanya hapa, hakuna haja tena ya kurudi mjini, nawasihi mafundi na wengine wenye fani zao wasipende kukimbilia mijini; Rais Samia ametuona, kila kitu hapa kijijini sasa hivi kinapatikana,” alisema fundi Mussa.
Kwa upande wake Scholastica Kitwewe, Mkazi wa Kijiji cha Mapili alisema umeme umerahisisha maisha ya wanawake kijijini hapo kwani hapo awali walikuwa wakitumia muda mwingi kuandaa mahindi ya unga kwa kutwanga katika kinu lakini sasa mashine za kusaga na kukoboa nafaka zimefunguliwa kijijini hapo jambo ambalo linarahisisha shughuli zao za mapishi ya kila siku na kuwaokolea muda.

Kwa upande wake, Elasto Mwampaya maarufu kama Fundi Lam ambaye ni Fundi Seremala kijijini hapo alisema kuwa umeme umewezesha kukua kwa karakana yake ya useremala na kwamba hivi sasa anatengeneza fenicha zenye ubora na kuuza katika mikoa mbalimbali kote nchini jambo ambalo halikuwezekana hapo awali kabla ya kufikishiwa umeme.
Alisema umeme umemuwezesha kupanua wigo wa ajira na kwamba katika karakana yake ameajiri vijana wengi na pia anatoa mafunzo kwa vijana namna ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme.
Akizungumza kuhusiana na umeme kijijini hapo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mapili Anthony Mwijuma, aliipongeza REA kwa kutekeleza mradi huo ambao alisema umekuwa ni neema kwa wananchi wake ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kufikiwa na umeme.

“Wananchi wa Mapili tunasema asante kwa Rais Samia kwani kupitia umeme vijana wamepata ajira, wengine wamebuni miradi na biashara ndogondogo za vinywaji, vifaa vya simu na wengine sasa hivi na mafundi wa kuchomelea hapahapa kijijini,” alisema Mwijuma.
Akizungumza hali ya usambazaji umeme mkoani Katavi, Msimamizi wa miradi ya REA Mkoani humo, Mha. Gilbert Furia, alisema vijiji vyote vina umeme na kazi inayoendelea sasa ni kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havikufikiwa.
“Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambayo imewezesha kufikisha umeme katika vijiji vyote 49 ndani ya Halmashauri za Mlele na Mpimbwe na sasa tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme vitongojini; hadi sasa katika Hamashauri hizi vitongoji 176 kati ya vitongoji 251 vimefikiwa na mradi unaendelea wa kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyobaki,” alisema Mha. Furia.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu aliipongeza REA kwa kukamilisha mradi wa kufikisha umeme vijijini na alisema kuwa amejionea namna ambavyo kazi ya kufikisha umeme vitongojini ikiendelea kutekelezwa kwa kasi.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia REA; vijiji vyote vimefikiwa; wananchi wa Mlele tunasema asante kwa Serikali maana umeme umeleta fursa, Mlele ya jana sio ya leo, hatua imepigwa,” alisisitiza Mbulu.
