‘Kasimamieni kwa weledi miradi ya maendeleo’

0

Na Hilarry Shuma OR-TAMISEMI

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainabu Telack, amewahimiza Maafisa tarafa na watendaji wa kata nchini kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao

Akifunga Mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata leo Julai 22, 2025 mkoani Lindi MheTelack amewataka washiriki kuhakikisha kuwa wanakuwa daraja la kuimarisha imani kati ya Serikali na wananchi, na si chanzo cha migogoro.

“Ni jukumu lenu kusimamia amani na utulivu, kuwa karibu na wananchi, kushughulikia kero zao kwa wakati, na kusimamia vyema mapato na miradi ya maendeleo.

“Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika ngazi ya msingi, hivyo hatutegemei fedha hizo zipotee au zisitumike kwa ufanisi,” amesisitiza
Telack.

Amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuwa vinara wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa njia sahihi na za kidijitali, akieleza kuwa ukusanyaji huo ndio msingi wa utoaji bora wa huduma za jamii.

Aidha, amesisitiza kuwa malalamiko ya wananchi yaangaliwe kama fursa ya kujirekebisha, si mashambulizi, na kwamba viongozi wanapaswa kutoa mrejesho wa hoja za wananchi kwa wakati, kwa uadilifu na heshima.

Aidha, Mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC)

Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa Serikali katika kujenga uwezo kwa watumishi wa umma wa ngazi ya msingi, katika kuhakikisha huduma bora na zenye tija kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here