Na Veronica Simba – WMA
KAMATI ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imekiri kuvutiwa na utendaji kazi wa Wakala wa Vipimo (WMA) Tanzania Bara na kuahidi kuweka mikakati ya makusudi itakayoisaidia Mamlaka inayosimamia vipimo nchini humo (ZAWEMA) kutekeleza majukumu yake kwa kiwango hicho au zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Aprili 16, 2026 baada ya ziara ya mafunzo katika Kituo cha Vipimo Misugusugu, mkoani Pwani, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Mohammed Ali Suleiman, amesema Wakala wa Vipimo upande wa Tanzania Bara wamepiga hatua kubwa kiutendaji hivyo kuna kila sababu ya Zanzibar kufuata mfano huo.

“Tumeona wenzetu wamefanya kazi kubwa na wana vipimo vya kisasa ambavyo vinawawezesha kuhakiki mathalani kiwango cha maji anachotumia mteja ndicho anacholipia, halikadhalika kwenye umeme pamoja na vipimo vingine.”
Mhe. Dkt. Suleiman ameongeza kuwa, Kamati yake itaishauri Wizara ya Biashara ambayo ndiyo inayoisimamia Mamlaka ya Vipimo Zanzibar, kuweka mikakati ya makusudi ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.

Amesema wataishauri Serikali kuhakikisha ZAWEMA, ambayo ndiyo Mamlaka ya Vipimo kwa upande wa Zanzibar, kwanza inakuwa Mamlaka huru lakini pia ipate mitambo ya kisasa ya uhakiki vipimo na pia ishirikiane kwa ukaribu na WMA ili iweze kutekeleza majukumu yote kwa ufanisi.
“Ukiangalia, Kituo hiki cha Misugusugu kinaipatia Serikali ya Tanzania mapato makubwa sana. Ni muhimu Serikali yetu iwezeshe ZAWEMA kufanya kazi kwa karibu na WMA ili kupata mafanikio kama hapa,” amesisitiza Mhe. Dkt. Suleiman.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, amesema anaamini kwamba, kupitia ziara hiyo ya mafunzo kwa Kamati kutoka Baraza la Wawakilishi, jukumu la uhakiki na ukaguzi wa vipimo linaenda kuwa bora zaidi kwa pande zote mbili; Zanzibar na Tanzania Bara.
“Niwahakikishie tu kwamba tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Zanzibar ili kuhakikisha Mtoa Huduma analindwa lakini pia Mpokeaji Huduma analindwa.”

Akidadavua zaidi kuhusu ushirikiano uliopo kati ya WMA na ZAWEMA, Mtendaji Mkuu amesema Taasisi hizo mbili zilikwishasaini Hati ya Ushirikiano (MoU) kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kushiriki kwenye mikutano ya kikanda na kimataifa pamoja na katika kaguzi za vipimo hususan katika bidhaa zilizofungashwa.
Amesema kuwa, WMA wakiwa ndiyo wenyeji katika ziara hiyo, wamewaonesha wageni wao utendaji kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo uhakiki wa tenki za kusafirishia mafuta, uhakiki wa mita za umeme pamoja na uhakiki wa dira za maji.

Wakala wa Vipimo Tanzania imekuwa ikipokea wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuja kujifunza kuhusu majukumu ya uhakiki wa vipimo.
Aidha, kwa sasa, Wakala wa Vipimo Tanzania ndiye Mwenyekiti wa Jukwaa la Kikanda linaloratibu masuala ya kivipimo (legal metrology) kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCMEL).