New Delhi, INDIA
KWA watu walioona mchezo wa kuigiza wa televisheni uitwao India; A Love Story ulioonyeshwa duniani kote, wanaweza kukumbuka namna mchezo huo ulivyokuwa ukieleleza namna kundi moja la jamii ya kihindi lililopewa jina Dalit, linavyobaguliwa na kunyimwa nafasi hata mara moja ya kushiriki katika matukio ya jamii kama ilivyo kwa watu wa jamii nyingine.
Wahindu wanaamini kwamba, mtu anapooga mahali inapokutana mito mitakatifu ya Ganges, Yamuna, na Saraswati wakati wa sherehe ya kihindu ya Kumbh Mela, husafishwa madhambi yake yote.
Wahindu wanaamini kwamba, mbali ya kuwasafisha madhambi yao, kuoga kwenye mito hiyo husaidia kuwafikisha wahindu kwenye daraja la kiungu.
Wakati genge la wanawake 100 kutoka kundi hilo linaloaminika kuwa ni la chini kabisa katika jamii ya kihindu, kundi la Dalit lilipopata nafasi ya kuoga kwenye eneo hilo (jambo ambalo si la kawaida kutokea katika jamii ya kihindu), lilitoka kwenye maji likidai dhambi zao zote zimesafishwa na uwepo wao kwao kwenye kundi la Dalit umefutwa.
Dalit ndilo kundi la watu linalobaguliwa kuliko wote nchini India, watu wa kundi hili wakiwa hawaruhusiwi hata kuwagusa watu wa makundi mengine yanayotambulika kuwa ni ya juu.
Watu wa kundi hili, hawaruhusiwi kushiriki kwenye shughuli zote za dini ya kihindu ikiwa ni pamoja na ile ya kuoga kwenye mito mitakatifu ifahamikayo kama Kumbh.
Lakini, katika tukio moja, wakati kundi hilo la watu wanaofahamika kama Dalit au kwa kiingereza ‘untouchable’ ama kwa Kiswahili watu wasio stahili hata kugusana nao lilipotoka kuoga kwa kujisafisha wahindu kutoka makundi mengine, waligoma kuingia kwenye maji hayo na hivyo kushiriki sherehe hiyo ya Kumbh kwa kudai kwamba, maji hayo yametiwa najisi na hayafai kuogwa na watu wa jamii za juu.
Lipo tukio moja ambalo wanawake wa kundi hili la Dalit waliwahi kuruhusiwa na kiongozi mmoja wa dini ya kihindu kuingia kwenye maji wakati wa kuoga Kumbh na walipotoka kiongozi huyo aliwapokea kwa furaha akiongoza nyimbo na dua za kihindu kabla ya kusema kwamba, kwa kuweza kuoga kwenye Kumbh, wanawake hao sasa wanaweza kuingia kwenye jamii ya watu wa hadhi ya juu.
Aliwamwagia majivu matakatifu kwenye mapaji ya nyuso zao na kutangaza kwamba tangu wakati huo, wanawake hao si Delit tena.
“Sherehe hii ya Kumbh yapaswa kuonekana kama hatua moja ya mafanikio makubwa kuelekea kuwarudisha katika jamii wa kundi linalobaguliwa katika dini yetu ya kihindu,” alisema mmoja wa watu maarufu waliokuwepo kwenye sherehe hiyo huku akielekeza ombi lake maalum kwa wanawake wa kundi linalotajwa kwamba ndilo la hadhi ya juu kuliko yote, kundi la Brahmins, kuwaunga mkono na kuwasaidia wanawake hao.
Swami Anand Giri, mmoja wa viongozi wa dini ya kihindu 150 waliokuwepo kwenye sherehe hiyo anasema: ”kuokolewa kwa dalit hao kumeandika historia mpya katika dini ya kihindu. Kufuatia misimamo mipya ya utamaduni wa msimamo wa kati, tunawakaribisha dada zetu hawa katika mkondo wa watu wa hadhi ya juu wa kihindu kuanzia leo hii.”
Sherehe hiyo ya Kumbh ilionekana kuwa na athari kubwa kwa wanawake kutoka kundi la wanawake hawa kutoka jamii inayoonekana hadhi yao ni kuishi maisha yao yote kwa kuokota vyakula majalalani, wanaoonekana kubaguliwa wazi na kundi la wahindi wa kutoka jamii za juu zaidi yao.
“Ingawa 300 miongoni mwetu watu wa wilaya ya Alwar waliachana na maisha ya kuokota majalalani miaka kumi iliyopita, wengi wa wahindu wa madaraja ya juu zaidi, bado wanatuona bado ni Dalit, wanakataaa kushirikiana nasi kwa kila jambo wala kushiriki kwenye mikusanyiko ya kijamii ambayo nasi tunaalikwa,” anasema mmoja wa wanawake waliowahi kuokolewa katika sherehe hiyo.
“Hivyo licha ya kutagazwa rasmi kwamba sisi si Dalit tena, hususani wakati tulipokula chakula pamoja na viongozi wa dini ya kihindu, kwangu hilo linaonekana bado halijasaidia sana, kwani bado tunatengwa,” anasema Nanda.
Siku zote unapotokea umuhimu wa kupambana na mfumo au utamaduni fulani uliojikita mizizi yake katika imani, inakuwa tabu sana kupambana nao. Imani hizo zinaweza kuwa za kidini, au utamaduni mwingine, kama ilivyo kwa hapa nchini katika mapambano dhidi ya tamaduni kama za kuamini kwamba, binadamu aliyezaliwa albino anaweza kutumika katika kumtafutia mtu mafanikio ya kichawi, au mfumo maarufu miongoni mwa makabila ya wafugaji wa kukeketa watoto wa kike; ni hivyo hivyo kwa mfumo huu wa ubaguzi wa kihindu wa Varna.
Mfumo huu wa Varna ni mfumo wa waumini wa kihindu unaowapanga watu ki-madaraja si kwa uwezo wao wanaoonyesha katika jambo lolote lile, bali kutokana na asili yao tangu kuzaliwa. Ni mfumo unaowagawa watu kwa kuegemea kwenye jamii wanazotoka tangu kuzaliwa, na hiyo kuwafanya watu wa jamii fulani kama waliokuja duniani kuteseka na kubaguliwa.
Ni utamaduni wa kiimani unaowagawa wahindi katika makundi manne ya kimsingi ambapo kundi la juu kuliko yoyote ni la Brahmin au watu wa familia za viongozi wa dini na la chini ni lile la watumishi.
Mfumo huu umedumu kwa zaidi ya miaka 2000 na ndani yake katika kila kundi, kuna mgawanyiko ambapo tunakuta kundi linaloonekana kuwa la juu zaidi na la chini zaidi katika kila kundi.
Ni kutokana na mgawanyiko huu wa ndani ya kundi ndipo ambapo kundi la Dalit, ambalo si moja ya yale makundi manne ya msingi, lilipotokea. Dalit linahesabika kama kundi la chini kuliko yote yale.
Katiba ya India ina kipengele kilichoandikwa kwa lengo la kupiga marufuku mfumo huu wa kibaguzi na imeanza kwa kupiga marufuku kundi la chini kabisa katika jamii, kundi la Dalit, lakini hiyo imesaidia kwa kiasi fulani tu hasa katika maeneo ya mjini, lakini kwenye maeneo mengine na hasa yale ya vijijini, ubaguzi umeendelea katika maisha ya kila siku kama vile hakuna kitu kilichoelekezwa na katiba.
Hata kwa watu wengine walioko mijini, katiba imekuwa ikipewa umuhimu watu wanapozungumza hadharani, lakini ndani ya familia, watu wameendelea kuhamasishana kuwabagua watu wa makundi mengine ya jamii yaliyo chini yao na hasa hili la Dalit.
Katika moja ya sehemu ambazo ubaguzi huu unaonekana wazi ni kwenye kazi ngumu na za watu wasio na elimu ambazo zimeendelea kuwa haki ya watu wa makundi ya chini kabisa, hata kama wana elimu ya juu; kazi kama kuondoa kinyesi cha binadamu kutoka kwenye vyoo ambavyo mfumo wake wa kusukuma kinyesi kwa maji haufanyi kazi, pamoja na kazi nyingine za aina hiyo.
Kwa mtu anayetazama, anaweza kuona wazi kwamba kuna dalili fulani ya kuwalazimisha watu hawa kufanya kazi hizi za hovyo kwani wapo wanaoamini kwamba, wakati mwingine mtindo wa kuwatengea kazi ngumu za mikono watu wa kundi la Dalit, ulipigwa marufuku na serikali mwaka 1993 hasa baada ya kugundulika kwamba watu wa kundi hili, wamekuwa wakilazimika kufanya kazi hizi hata kama nafasi nyingine zipo kutokana na utamaduni wa kuwabagua.
Ipo dhana pia kwamba, huenda kazi hizi wakati mwingine hutengenezwa kwa makusudi ili kuwatesa watu hawa. Maana yake hii ni kwamba hata kama kazi hizi zingeweza kufanywa kwa kutumia vifaa vingine, ama kama vifaa hivyo vipo, hutangazwa kwamba ama havifanyi kazi au havipo ili mradi watu wa kundi hili waweze kufanya kazi hizi katika ugumu wake unaofanana na wa kitumwa.
Hata hivyo, si watu wote wa jamii ya kihindi wanaokubali kwamba kitendo cha kumkosha mtu wa kundi la Dalit au makundi mengine ya chini kwenye maji matakatifu wakati wa sherehe takarifu ya Kumbh, kunasaidia kumsafisha kutokana na nuksi ya kuzaliwa aliyo nayo na kumfanya awe sawa na watu wa makundi mengine ya juu.
Kwa bahati mbaya, licha ya kwamba wengi wa wasioamini hivi ni wale wa makundi ya juu, lakini hata miongoni mwa watu wa makundi ya chini, nao huona hiyo haisaidii na hivyo kuendelea kuishi katika kukata tamaa.
Ni kutokana na hilo, ndipo mwanaharakati wa haki za kijamii nchini India, S. R. Darapuri amekiita kitendo cha kuwakosha watengwa kijamii nchini India kwenye sherehe za Kumbh kama njia ya kuwapandisha daraja, kuwa ni makafara yasiyo na maana yoyote.
“Watu wanaojulikana kama wa daraja la juu waliotawala kwa karne zote hizo jamii ya kihindi, wataendelea kuwaona hawa wengine kama watu wa chini kabisa hata kama wataendelewa kuoshwa nuksi kwenye sherehe hizi za Kumbh.
Dhana na fikara za jamii inayojiona ndiyo jamii kuu, haiwezi kubadilika ili kuwakubali hawa wengine kirahisi” alisema Darapuri: “Hivyo, huu ukoshaji wa Kumbh hauna chochote zaidi ya kuwa ni igizo la watayarishaji lisilo na ukweli wowote.
Naye mwanaharakati na mwandishi Madhu Kishwar anakubali kwamba kunahitajika kufanyika mengi zaidi ya sherehe za Kumbh ili kubadili mitazamo ya watu zaidi ya bilioni 1.2 wa India kwamba kinachoendelea katika mfumo wa jamii, si kitu sahihi kabisa, lakini akapongeza hatua ya kuanzishwa kwa ukoshaji huu wa Dalit kama moja ya jitihada za kuondoa dhana za kuwadharau na kuwaona wengine kama wala takataka.
“Udhalilishaji na unyanyapaa unaojengeka nyuma ya ufanyaji kazi za udhalilishaji uliopo kwenye jamii, huondoka kwakasi mara jamii inapoamua kujenga mfumo wakueleweka wa vyoo na taratibu nyingine za usafi na hivyo kuondoa kazi za kidhalilishaji zinazomlazimisha mtu kushika vinyesi vya wengine ili kuweza kupata njia ya kuishi.
“Si rahisi kumkuta mtu akinyanyapaliwa kwa kuwa ni mfanyakazi wa usafi kwenye uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa kwani hiyo inafahamika kuwa ni kazi ya heshima,” anasema Kishwar, kutoka Kitivo cha Siasa kwenye Chuo Kikuu cha Delhi.
“Kumpa mtu kazi ya kusomba vinyesi kwenye choo kichafu kupindukia, kunamfanya mtu anyanyapaliwe popote duniani na si India pekee, kwani inamfanya aonekane ni mtu wa kuchezea vinyesi kila siku ya maisha yake na ndiyo hadhi yake” anasisitiza.