Haya yakifanyika, Morogoro itaibeba sekta ya Utalii nchini

0

Na Syd. Chifu Mussa Bwakila Lukwele IV

UTALII ni sekta inayokuwa kwa kasi Duniani na kuwa tegemeo na muhimili mkuu wa uchumi kwa Mataifa mengi yakiwemo ya Kiafrika. Kila Taifa na kila mji unavyo vivutio vyake vya utalii; jiografia yake, majengo yake, masalia ya makazi, aina za amali zinazofanywa kwenye eneo husika, utamaduni wake, miundombinu yake, amani na utulivu wake n.k.

Nchi yetu ni sehemu ya Mataifa yanayoinukia kwa kasi kiuchumi, huku sekta ya utalii ikipewa kipaumbele cha kipekee kuongeza fedha za kigeni na kuchangia kukuza uchumi. Morogoro ikiwa ni sehemu ya nchi yetu, imekaa kwenye eneo lenye mvuto wa kipekee Kijiografia, ni eneo la kistratejia kiuchumi pia, huku utitiri wa vivutio vya uutalii vikisheheni kwenye mkoa huu.

Mkoa huu una vivutio vingi vya Utalii baadhi vikiwa havipatikani sehemu yoyote Duniani, na vingine ni vile vya kawaida vinavyojengwa na Jiografia yake ikiwemo Milima, Misitu, Vyanzo vya maji, mito, mabwawa, maeneo chepechepe, mapango, miamba, hali nzuri ya hewa na kadhalika; pamoja na viumbe hai wakiwemo binaadamu, wanyama, ndege, wadudu, na mimea.

Lakini, mkoa una vivutio vilivyotambuliwa na kuorodheshwa japo havitangazwi na pia una vivutio vinavyotangazwa (mfano hifadhi za wanyama) sanjari na vile ambavyo bado havijatambuliwa, vinavyoshikika na visivyoshikika, vikiwemo vile visivyotiliwa maanani na vinavyohitaji ubunifu ili kuonekana, kutambuliwa, kuhifadhiwa, kuendelezwa na kutangazwa kwa Dunia.

Kwanza, Mkoa wa Morogoro una karibu makabila yote 130 ya Tanzania, lakini pia unajumuisha jamii zenye asili ya pande zote za Dunia; hivyo kuupa utajiri mkubwa mkoa huu kuwa na ‘bahari ya utamaduni’ na vielezeo vyake anuai (mila na desturi mchanganyiko). Tamaduni hizi ni kivutio kimojawapo muhimu cha Utalii wa Kitamaduni na chanzo kimojawapo cha mapato ya nchi endapo utaratibiwa vema kwa kutambua vituo na vielezeo vyake.

Pili, Morogoro hakuna makumbusho hata moja, japo kuna utajiri mkubwa wa urithi wa kitamaduni na kihistoria unaopaswa kuhifadhiwa, kuendelezwa, na kutangazwa, sio tu kwa faida za kiuchumi bali pia za kijamii (kwa kurithisha ustaarabu wa kipekee wa sekta anuai zinazogusa maisha ya kila siku kwa vizazi vya sasa na vijavyo). Morogoro kwa mfano, inaweza kuwa na aina tofauti za makumbusho yakiwemo ya kisekta, mathalan;-

Huu ndio mkoa ulioweka Historia ya kuasisi timu nne za Soka kwa siku moja katikati ya miaka ya 1960 (yaani Mseto, Shujaa, Jogooo na Nyota Afrika) ambazo zilipewa miaka minne na mamlaka husika za michezo mkoani pamoja na wazee, sio tu zianzie ligi daraja la nne na kufika ligi daraja la kwanza, bali pia zichukue ubingwa.

Ni timu hizo pamoja na zile za mashirika ya Umma ndizo zilizoiweka Morogoro kwenye Ramani ya Soka kitaifa na kimataifa, na kuzaa wachezaji mashuhuri waliokuwa tegemeo kwa taifa. Tunaweza kuweka kumbukumbu zao na za viongozi wa michezo, Wazee (waliokuwa wafadhili na wahamasishaji), na wanasiasa waliochangia kuifanya Morogoro ya zama hizo iwe kinara wa soka na michezo mingine ikiwemo masumbwi n.k.

Pia, Morogoro ulisifika kwa Muziki ikiwa na Nguli wenye hadhi ya Kidunia kama Mbaraka Mwishehe Mwaruka na Kulwa Salum (wa Moro jazz na Super Volcano), Issa Mrisho (wa Mzinga Jazz), pamoja na Juma Kilaza (wa Cuban malimba, Less Cuban na TK Limpopo), bila kumsahau nguli Salum Abdallah Yazid (wa Cuban), pamoja na wenzao wengi walioweka alama isiyofutika kuanzia kwenye ‘kizazi chao cha dhahabu’, hadi kizazi cha sasa kinachoonekana kusahau yaliyopita! Watakumbukwaje nguli hawa bila ya kuwepo vielezeo vya kuonekana machoni?

Kwa msingi huo basi, kwa kujenga makumbusho itakayokuwa na historia zao, picha, sanamu, vifaa na tuzo, sio tu kutawaenzi, bali pia kuvutia utalii, na kuleta chachu ya kufufua michezo na burudani zinazojenga badala ya zile za kubomoa zinazoutafuna mkoa na nchi.

Tatu, Utalii wa Maeneo ya Kihistoria. Maeneo ya Kihistoria kama vile majengo ya kale, visima, minara, na hata miundombinu mfano wa barabara, vivuko, madaraja n.k. hayana budi kutambuliwa, kukarabatiwa kama si kujengwa upya, kuendelezwa, na kutangazwa kama vivutio vya utalii.

Nne, Utalii wa Mandhari: – Ni wajibu wa Serikali ya mkoa kushinikiza wilaya zote kuwekeza kwenye mipango miji, kwa kuboresha mandhari na kuwekeza zaidi katika miundombinu hasa barabara na mifereji, majengo muhimu kama hospitali, shule, vyuo, nyumba za wazee, nyumba za mayatima, na hata maeneo ya mapumziko, bustani za miji, na maporomoko ya maji.

Kufanya usafi wa mito na mabwawa pamoja utunzaji wa kingo zake kama zamani, uhifadhi wa maeneo chepechepe, sanjari kuhakikisha mandhari za vituo vya mabasi, reli, na viwanja vya ndege yanavutia. Usafi wa miji na makaazi na uzingatiaji kanuni za mipango miji katika ujenzi na undelezaji miji, ni kivutio muhimu sana cha utalii wa mandhari.

Tano, Utalii wa kwenye maji. Morogoro ni mkoa wenye mito mingi mikubwa na midogo pamoja na mabwawa ambavyo vinaruhusu uwepo wa utalii wa kwenye maji. Kuna umuhimu wa kuvutia uwekezaji ambao utaweka boti za mpira kwa utalii wa mtoni, kuweka mashua zenye hadhi ya Hoteli ya Nyota Nne na tano kwenye Mabwawa makubwa na hata baadhi ya mito mikubwa, na pia kuweka vituo vya michezo ya kwenye maji na vifaa vyake vikiwemo vya usalama kwa ajili ya watoto na watu wazima, sanjari na kuasisi michezo ya kuogelea.

Sita, Utalii wa Milimani. Kwa jiografia ya mkoa wa milima kama Morogoro, ni vema kuhusisha uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya usafiri wa barabara za milimani, na kuweka usafiri wa kwenye waya (Cable Cars), hasa katika meneo tata ya milima yasiyofikika kirahisi ikiwemo vileleni.

Ikumbukwe kuwa, Morogoro hasa milimani ni moja ya maeneo yanayotoa viungo kwa wingi vikiwemo Mdalasini, karafuu, na hata kahawa; sanjari na kilimo cha mboga na matunda vinavyolisha mji na mikoa jirani, na hata baadhi kupelekwa nje ya nchi. Kilimo cha milimani pia ni sehemu ya kivutio cha utalii.

Saba, Utalii wa Maeneo ya Mapumziko (Recreation Centres). Maeneo ya mapumziko hasa bustani kubwa za miji na vituo vya michezo anuai (Amusement parks and mixing sports center) ni sehemu ya utalii wa kimamboleo. Kwa mfano, Mkoa unaweza kutoa amri kila halmashauri kuhakikisha inakuwa na kituo cha michezo anuai, kikiwa na vifaa vyote muhimu kama Gurudumu kubwa (Ferris wheel), Gari Moshi (Fun Train), bembea za aina mbalimbali, Miserereko n.k.

Nane, Utalii wa Matukio. Serikali ya mkoa kupitia Maafisa Utamaduni na Michezo wakishirikiana na wilaya, ni vema wakabuni mbinu mbalimbali za kuvutia utalii kupitia utalii wa matukio, kwa mfano; wanaweza kuandaa matamasha ya kitamaduni ya makabila yote 18 ya asili na ya wahamiaji yaliyoko Morogoro.

Pia, wanaweza kushirikiana na Viongozi wa jadi ambao ni kawaida yao kufanya matambiko ya halaiki, na matukio ya jando na unyago (mfano waluguru huwa na unyago kwa wanawake kila mwisho wa mwaka, na jando la ‘Mgambo’ na ‘Ng’ula’ kila katikati ya mwaka hasa majira ya baridi).

Aidha, kushirikiana na vyama vya michezo mbalimbali ikiwemo kile cha michezo ya jadi, kuandaa matamasha ya michezo hiyo, mfano tamasha la Michezo ya jadi, tamasha la Michezo ya sikukuu za kidini kama Pasaka, X-Mass, Eid kubwa na Ndogo, na Maulid, zikijumuisha michezo pendwa kama soka, mbio za baiskeli, mbio za magari, riadha, kuogelea n.k.

Matamasha ya muziki wa dansi ya mara moja kwa mwaka mfano ya kuwaenzi nguli wa muziki waliotoa michango mikubwa ya kuutangaza mkoa kwa namna moja au nyingine kimataifa kama vile Salum Abdallah Yazid, Waziri Nyange, Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, Lazaro Bonzo, Juma Kilaza, Issa Mrisho, na wengineo.

Vile vile, matamasha ya Tiba za asili kwa kushirikiana na mamlaka husika yaani Wizara ya Afya, Vyuo Vikuu vinavyojihusisha na masuala ya mimea na Tiba, na vyama vya waganga wa jadi n.k. Lakini pia, kuwapa nguvu na mkono wa ushirika wadau wanaoandaa matamasha ya kitamaduni kama lile la ‘Juu Afrika Festival’, ‘Uluguru Cultural Festival’ n.k.

Maafisa hawa wanaweza kushirikiana na wadau kuandaa mbio maalum zenye hadhi ya Kimataifa zinazotaja na kutangaza maeneo ya utalii kama vile Mikumi National Park Marathon, Mount Uluguru Forest Reserve Marathon, Udzungwa National Park Marathon, Nyerere National Park Marathon n.k.

Kwa ufupi wa maneno, Mkoa wa Morogoro katika kila wilaya yake, kunatakiwa kuwepo wastani japo wa tukio moja kila mwezi, litakalotangazwa kitaifa na kimataifa, kuvutia utalii na kuileta Dunia Morogoro. Kwa bahati mbaya, kwa mtazamo wetu, mkoa wa Morogoro licha ya kuwa kwenye eneo la kistratejia ya kiuchumi kutokana na jiongrafia yake ya kipekee, na licha ya kuwa na vivutio vingi vya Utalii wa aina mbalimbali, lakini bado uko nyuma kwenye sekta husika.

Hapa kazi ya ziada inatakiwa kufanyika kuifanya sekta ya Utalii ipate uhai, na sio kubaki kama utajiri uliofukiwa kwenye tabaka la chini la ‘jalala la sahau’ mkoani Morogoro kwa kufanya yafuatayo; – Kwanza, kurejesha Shirika la Maendeleo Mkoani Morogoro MOROGORO DEVELOPMENT COOPERATION (MODECO). Shirika hili ndilo ambalo pamoja na mambo mengine.

MODECO litakuwa mbia muhimu wa Halmashauri na sekta binafsi kwenye uwekezaji, hasa mkubwa wa sekta mbalimbali ikiwemo ya Utalii. Shirika hili pia linaweza kuwa na nguvu ya kisheria, kukopa kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa maendeleo ya sekta tofauti tofauti.

Pili, kuasisi kituo cha habari (Information Center). Kituo hiki ndicho kitakachotoa taarifa na kuutangaza Utalii kwa watalii wa ndani na nje, juu ya vivutio vya utalii vilivyopo, kupitia vyombo vya habari kama Televisheni, Radio, Magazeti na majarida, pamoja na mitandao ya kijamii, halkadhalika machapisho kama vitabu, vipeperushi n.k. sanjari na kutumia matukio muhimu ya ndani na nje ya mkoa, ya Kitaifa na Kimataifa, kama vile mikutano, maonesho n.k. kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko mkoani hapa.

Tatu, kuna umuhimu wa kuunda kikosi kazi kitakachokusanya ubunifu na mbinu za kuving’amua, kuvitunza, kuviendeleza na kuvitangaza vivutio vya utalii kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kupitia njia mbalimbali ikiwemo balozi za Tanzania nje ya nchi, balozi za mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa zilizoko nchini n.k.

Nne, kuongeza Bajeti ya Utalii: – Kuongeza bajeti ya ung’amuzi, utambuzi, uhifadhi na uendelezaji vivutio vya utalii, sanjari na kukithirisha uhifadhi, maboresho, na usafi wa mazingira. Tano, kuboresha miundombinu ya barabara (kujenga, kukarabati barabara, mifereji ya maji taka na taa za kando ya barabara), pamoja na kuhamasisha uboreshaji vituo vya utalii (kama mahoteli na migahawa) n.k.

Sita, kurejesha Shirika la usafiri la Mkoa (MORETCO). Shirika hili ndilo linaloweza kuwa chini ya umiliki wa Shirika letu la maendeleo (MODECO), likiwa na mabasi, ndege ndogo, Treni ya kitalii katika reli ya kati, na hata boti katika mabwawa na mito mikubwa. Kwa kutumia mfumo wa Mfumo wa hisa nafuu kwa kila mwana-Morogoro na mikopo vinaweza kuiwezesha MODECO kuasisi na kumiliki MORETCO.

Saba, kuboresha huduma bora kwa wateja (Customer Service), kwa kujenga kitaaluma nguvu kazi ya kuongoza na kuhudumia watalii, sanjari na kuwajenga kifikra wananchi kuona fursa za kuongeza kipato kupitia sekta ya utalii kwa kuboresha huduma kwa wateja wao (mfano kwa wasanii wa sanaa za maonesho na Sanaa nyinginezo kama wasusi, wachonga vinyago, wafinyanzi n.k). Tunaamini maoni yetu yatazingatiwa na kufanyiwa kazi na mamlaka husika Kimkoa na Kitaifa, kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Mwandishi wa Makala hii ni Mwanahabari kitaaluma na Chifu Mkuu wa Waluguru wa CHOMA (akiongoza eneo karibu lote la kijiografia la Morogoro Manispaa, sehemu ya kaskazini na kaskazini Magharibi ya Mvomero, na sehemu ya fulani ya kusini mwa Morogoro vijijini). Anapatikana kwa simu namba +255 657 185468, na Barua Pepe: lukwelepalace@gmail.com / mussa_ally@ymail.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here