MGOMBEA wa Kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga soko kubwa la kisasa katika eneo la Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dkt. Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 22, 2025, alipokutana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Kinyasini, katika muendelezo wa kampeni za CCM.
Amesema ujenzi wa soko hilo jipya utalenga kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na pia kuandaa eneo maalum la kuegesha magari, ili kurahisisha shughuli za kibiashara.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali ijayo itakayoundwa na CCM itaendelea kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji, mikopo isiyo na riba na kuwahakikishia upatikanaji wa masoko ya bidhaa zao.
Ameongeza kuwa Serikali itaongeza maradufu fedha za mikopo nafuu kutoka Shilingi Bilioni 96 zilizotolewa katika awamu inayoisha.
Akiendelea kuzungumza na wananchi, Dkt. Mwinyi amewaomba kuichagua CCM kupitia kura zao ifikapo Oktoba 29, 2025, ili chama hicho kiendelee kuleta maendeleo zaidi.
Pia, aliwasihi kuwachagua wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM pamoja na kumpigia kura mgombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo, akizungumza na vijana na wajasiriamali wa sekta ya utalii huko Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dkt. Mwinyi alisema Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya utalii kupitia sera ya Utalii kwa Wote.
Alibainisha kuwa Serikali itajenga miundombinu bora ya utalii, kutoa mikopo isiyo na riba na kutoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali watakaonufaika na mikopo hiyo, ili fedha zitumike ipasavyo na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.