Dkt. Mwinyi aahidi kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo Kusini Unguja

0

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali inakusudia kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tunguu hadi Makunduchi, pamoja na barabara za ndani katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Uwanja wa Michezo wa Paje, Mkoa wa Kusini Unguja leo Oktoba 16, 2025, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kwa lengo la kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa madaraja yatakayounganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, ikiwemo daraja la Unguja Ukuu – Uzi – Ng’ambwa linaloendelea kujengwa, na daraja la Chwaka – Charawe.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa Bandari ya Kizimkazi, sambamba na kuziimarisha bandari ndogo za Mtene, Chwaka na Unguja Ukuu.

Pia Serikali itajenga viwanja vya ndege vya Nungwi na Paje, miradi ambayo itafungua fursa mpya za kiuchumi kwa mikoa ya Kaskazini na Kusini.

Kuhusu sekta ya elimu, amesema Serikali itajenga madarasa 1,000 kwa shule za msingi na 1,000 kwa shule za sekondari, pamoja na shule 4 za msingi na shule 10 za sekondari za ghorofa katika Mkoa wa Kusini.

Katika sekta ya afya, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatarajia kujenga Hospitali ya Mkoa wa Kusini Unguja, huku ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kufundishia Binguni na Hospitali ya Saratani Binguni ukiendelea kwa kasi.

Kuhusu huduma ya maji, ameeleza kuwa Serikali itatekeleza mradi mkubwa wa maji wa dola milioni 55 za Marekani, utakaondoa kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Maeneo yatakayonufaika ni Uroa, Marumbi, Pongwe, Jambiani na Makunduchi.

Vilevile, Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mafunzo, vifaa, mikopo isiyo na riba, na mazingira bora kwa wajasiriamali ili kuendeleza uchumi wa wananchi wa kipato cha chini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here