Dkt. Migiro azindua Programu ya Kimataifa ya Uongozi na Utawala

0

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, leo Septemba 10, 2025, amezindua rasmi Programu ya Kimataifa ya Uongozi na Utawala (Mwaka wa Masomo 2025–2026) katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS).

Balozi Migiro, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo, alieleza kuwa programu hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya MJNLS na Chuo Kikuu cha Renmin cha China—ni hatua muhimu katika kuandaa kizazi kipya cha viongozi kwa Afrika, China na Nchi zinazoendelea.

Darasa la kwanza la programu hii linajumuisha wanafunzi 10 wa Shahada ya Uzamivu (PhD) na 22 wa Shahada ya Uzamili, waliotoka katika Vyama Sita vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, jambo linaloashiria mwendelezo na uhai mpya wa uongozi barani Afrika.

Balozi Migiro pia alisisitiza uhusiano wa programu hii na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha nafasi ya wananchi, hususan wanawake, katika kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha, aliwataka Watanzania kudumisha amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akihitimisha hotuba yake, alitangaza rasmi kuanza kwa programu hiyo na kuipongeza Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere (MJNLS) na Chuo Kikuu cha Renmin kwa kuimarisha daraja la mshikamano na dira ya pamoja ya maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here